4. Jamii

Ushirikiano Ndiyo Msingi Wa Uhusiano Na Wengine

S hukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu na rehema na amani zimfikie Mtume wa Mwenyezi Mungu na jamaa zake na Swahaba zake na wote wanaomfuata. Ama baada ya utangulizi huu mfupi, ili dunia ipate amani na ushirikiano hapana budi dira ya Uislamu itumike kwani Uislamu hujali uhusiano na wengine. Ushirikiano unaozungumziwa hapa lazima ulenge kuja na mfumo na muundo unaohakikisha amani na uhusiano mwema wa kuishi na wengine unafikiwa. Na ukweli wa mambo ulivyo ni kwamba pamoja na kuwa watu na mataifa tunatofautiana kifikra, kimwenendo na kiitikadi, ni lazima ipo sehemu tunayoweza kukutana na kuweza kuwasiliana na hatimaye kushirikiana kwa pamoja kwa maslahi ya wote. Na sehemu ya makutano, huu ni mkusanyiko wa tunu nyingi za kiutu ambazo hakuna mtu mwenye akili anayeweza kuzipinga. Tunu hizo ni kama busati linalowakusanya wote mahali pamoja. Ni vema tukasimama kidogo ili tuone baadhi ya tunu hizo za kimaadili na jinsi zilivyo na mchango muhimu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Uislamu na watu wa dini nyingine, uhusiano wenye msingi wa kiutu. Haki Haki ndiyo msingi wa uongozi. Sharia na kanuni zote za Mungu zinasisitiza haki kwani lengo la dini ni kuleta uongofu na kueneza wema, uadilifu na huruma. Haki kwenye mizani ya Mwenyezi Mungu ni pacha wa kumpwekesha Mungu. Na dhuluma kwenye mizani ya Mwenyezi Mungu hukaribia kuwa pacha wa shirki. Haki ni mhimili muhimu wa kuwepo kwa umma wa Kiislamu na ndiyo chanzo cha kuitwa umati bora. Ili kuimarisha uhusiano na wengine, haki inahitajika. Katika zama hizi katika uhusiano wa kimataifa, haki ni msingi wa mikataba na makubaliano yote. Mikataba hii huhakikisha haki inatendeka kwa makundi yote, bila ubaguzi. Vilevile, ni lazima sheria hizo zilenge kuimarisha uhusiano na watu wengine, sawa watu hao kama watakuwa katika mfumo wa taifa, vyama au ushirika au mtu binafsi. Lengo la wote hao ni lazima liwe ni kutenda haki.

Usawa, undugu na utu

Na miongoni mwa kanuni za Uislamu zitakazopelekea dunia kuwa na amani ni usawa kwa wote pasipo kujali jinsi, tofauti za lugha na mazingira. Asili ya watu wote ni kama matawi ya mti mmoja. Baba yao ni Adamu na Adamu anatokana na udongo. Kwa mantiki hiyo, hakuna mbora kati ya mweupe juu ya mweusi, lakini ubora wao ni katika imani, uchamungu na matendo yanayoihudumia jamii ya wanadamu. Ni mara ngapi tofauti hizi za kutengeneza zimesababisha majanga, kuzusha vita, umwagaji damu, ukiukwaji haki kunasababisha ghasia, na kuifanya dunia ishindwe kuishi katika maisha utulivu, furaha na amani. Hakika usawa na hatimaye amani haviwezi kufikiwa isipokuwa kwa kuzing’oa hizi desturi angamizi kutoka shinani. Na ndiyo maana Qur’an Tukufu inazungumza na watu wote na si waumini pekee kwa lengo la kutokomeza mawazo haya. Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni” (Qur’an, 4: 1). Pia Mwenyezi Mungu anasema kwenye Aya nyingine: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanaume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari,” (Qur’an 49:13). Na watu wanaofanya kampeni ya kujenga mahusiano mema na wengine wanatakiwa, wasisitize na waoneshe kwa roho safi dhana ya kuishi kwa amani na wengine na kuitekeleza kiuhalisia kwenye jamii ya Kiislamu ili uwe mfumo wa kuigwa na wengine. Wakati huohuo, wanaotaka mahusiano wabainishe dhana ya usawa feki inayohimizwa na wengine, kwani usawa unaohimizwa na wengine ni butu na hulenga tamaa na maslahi binafsi.

Ahadi na makubaliano

Uislamu unayaangalia makubaliano na ahadi kwa jicho la kiimani zaidi. Sanjari na hilo, Uislamu unaeleza uharamu wa kukiuka ahadi na maagano kwani suala la ahadi na makubalino ni la wajibu wa kisharia unaosisitizwa na Uislamu. Qur’an inasisitiza sana suala la kutekeleza ahadi. Allah anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka,” (Qur’an, 16:91). Mtazamo wa Uislamu katika suala la usaliti na hiyana upo wazi mno na umelikataza. Mtume alifanya makubaliano na kujenga uhusiano bila kufanya usaliti na hiyana. Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) pia alikuwa analiusia jeshi lake kwa wasia mbalimbali, huku wasia wake mkuu ikiwa ni kutofanya hiyana na usaliti. Imepokewa na Suleiman bin Bureydah kutoka kwa baba yake akisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani ya Allah imshukie) alipokuwa anamuamrisha Amiri kwenye jeshi au kikosi maalum alikuwa anamuusia heri na kumchamungu yeye binafsi na Waislamu anaofuatana nao. Kisha husema, ‘Piganeni kwa jina la Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, muuweni anayemkufuru Mwenyezi Mungu, msifanye hiyana na wizi, wala msiwakatekate (mtakaowaua) na wala msiwauwe watoto wadogo’” (Muslim).

Ushirikiano na kutegemeana

Kwenye Qur’an Tukufu, limekuja agizo la kusaidiana na ambalo msingi wake ni kuhimiza maadili bora na yenye lengo la kuwahakikishia heri wanadamu wote na kuwafanya wawe karibu na Mwenyezi Mungu, kama ambavyo limekuja katazo la kusaidiana kunakopelekea katika ukiukaji wa maadili unaolenga kusababisha uadui au madhara kwa wengine. Mwenyezi Mungu anasema: “Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu” (Qur’an, 5: 2).

Yatokanayo na aya

Aya inawaamuru wasemezwao kwa tamko la wingi na kuwataka washirikiane kwenye mema, hali inayoonesha suala la ushirikiano ni amri. Aya haimkutaja huyo wa kushirikiana naye jambo linalodhihirisha kuwa hilo ni tamko linalowahusu watu wote wenye utayari wa kushirikiana kwenye mambo mema na ya kumchamungu, na pasipo kuangalia dini, itikadi ya mtu na mawazo yake. Pia Aya haikumtaja huyo anayestahiki kutendewa wema, hali inayoonesha viumbe vyote kuanzia binadamu, wanyama na mazingira vinastahiki kutendewa wema.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close