4. Jamii

Tuwafundishe watoto kutoa sadaka

Dini ya Kiislamu inasisitiza sana watu kutoa mali katika vile ambayo Allah amewaruzuku. Utoaji huu ni pamoja na zaka au sadaka kwa ajili ya kutaka radhi za Allah. Kwa jumla, utoaji ni katika ibada muhimu zilizohimizwa katika dini yetu tukufu ya Uislamu.

Yapo malipo makubwa sana kwa mtu anayedumu katika ibada ya kutoa mali yake katika njia za kheri. Aidha, utoaji sadaka umehimizwa kwa kuwahumkinga mwanadamu na mabalaa mbalimbali ya kimaisha na kwa kuwa ni njia nzuri ya kumuweka karibu mwanadamu na Muumba wake (Taz: Qur’an, 2:272 na 33:35).

Pamoja na ukweli huu, bado watu wengi hawaoni umuhimu mkubwa wa kuishi katika ibada hii. Kukosekana kwa watoaji kumesababisha watu wengi ndani ya jamii zetu waishi katika lindi la umasikini, huku kula yao ikiwa ya kubahatisha na wakikosa mavazi ya uhakika na nyumba yenye hadhi.


Kwa upande mwingine, wapo watu wachache katika jamii yetu wanaoogelea katika maisha ya raha, na hawaoni haja ya kuwasaidia masikini. Kutoa ni tabia ambayo bila shaka inapaswa kujengwa na kulelewa. Wazazi, walezi, walimu, masheikh na jamii tunapaswa kushikana pamoja na kuhakikisha kuwa tabia hii tunailea katika maeneo yetu. Aidha, tunapaswa kushiriki kwa mifano katika kuijenga tabia hii muhimu ya kutoa.


Kwa upande wa wazazi na walezi, nyie ni wadau muhimu sana katika ujenzi wa tabia hii. Zipo njia nyingi zinazoweza kutumika kuijenga tabia hii hasa kwa watoto na wanafamilia wengine. Hapa tutaja baadhi ya mambo hayo:

Kwa kuanzia, jenga utamaduni wa kuwapa watoto sadaka kwa ajili ya Swala za Ijumaa. Utaratibu huu ni mzuri kwa kuwa unalenga kuwaonesha watoto umuhimu wa kutoa kwa ajili ya Allah. Mpe mtoto kiasi chochote cha fedha na uhakikishe anakitoa siku ya Ijumaa. Pia, hakikisha mara zote unampa mtoto sadaka bila kukosa ili kujenga mazoea. Ni wazi kuwa, mtoto aliyelelewa katika utaratibu wa kutoa sadaka kama hizi atapenda kutoa pindi atakapokuwa mtu mzima.


Jenga utamaduni wa kuwasaidia majirani zako wenye uhitaji. Katika maeneo yetu tunamoishi, wapo watu wengi wenye shida mbalimbali. Ni jambo zuri kuwasaidia kutatua matatizo yao mbalimbali ikiwemo ada za shule, chakula, mavazi n.k. Hali hii kama itaratibiwa vizuri inaweza kuwa na athari nzuri kwa tabia za watoto wetu huko mbeleni.


Jenga utamaduni wa kwenda na watoto kutembelea vituo vya mayatima. Katika miji yetu wapo wadau ambao wamewakusanya mayatima kwa lengo la kuwasaidia. Katika vituo hivi kuna changamoto nyingi za kiuendeshaji; chakula, malazi, mavazi, mahitaji ya shule n.k. Watoto wetu wanapaswa kujua hali hii. Baada ya kujua hali hii, shirikiana nao, kuonesha namna wazazi na jamii inaweza kusaidia kuondoa changamoto hii.


Wazoeshe watoto kuchangia watu waliopatwa na majanga kama mafuriko, matetemeko, ajali mbalimbali na vimbunga. Watoto kama sehemu ya jamii wanapaswa kufundishwa kutoa kwa ajili ya kuwasaidia watu waliopatwa na majanga. Hali hii itaimarisha sana tabia yao ya kuguswa na matatizo ya watu. Michango inayohusiana na majanga kama haya inaweza kukusanywa kupitia kupitia shuleni, taasisi binafsi, serikali na madrasa. Kama michango hii itaratibiwa vizuri watoto wengi watajifunza umuhimu
wa kuwachangia watu wenye shida.


Kwa jumla, suala la utoaji wa sadaka ni ibada kubwa na ni tabia inayopaswa kuwafunza kwa watoto. Ibada hii inaweza kushamiri katika jamii yetu kama wazazi na walezi watakuwa mfano kwa watoto. Watoto wanapaswa kujua umuhimu wa kutoa kwa watu wenye shida, na kama watazoeshwa kutoa katika umri mdogo watakuwa watoaji wazuri watakapoku-
wa watu wazima.

Tags
Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close