2. Ncha ya Kalamu4. Jamii

Tutumie ujana kama neema siyo laana

 “Na bila shaka tumewaelezea watu namna kwa namna katika hii Qur’an kila mfano lakini mwanadamu amekizidi kila kitu kwa ubishi.” [Qur’an, 18:54]

Katika moja ya matoleo ya nyuma ya gazeti hili, kuliandikwa makala yenye kichwa cha habari “Vijana wetu hazina yao.” Nilipenda sana kichwa cha makala hii iliyozungumzia namna vijana wanavyotumikia mifumo inayochochea uvunjifu wa  maadili ya dini yetu ya Uislamu.

Kila mwaka August 12, dunia inaadhimisha Siku ya Vijana Duniani, hii ni siku iliyopitishwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa ajili ya kuangazia masuala ya kuhusu vijana. Siyo lengo la makala hii kuzungumzia historia ya siku hii, bali kuleta mtazamo wa Kiislamu katika mijadala iliyotamalaki kuhusu masuala ya vijana wakati huu.

Tunapomtaja kijana, tunazungumzia wa jinsia zote mbili wa kiume na wa kike, wenye umri kuanzia miaka 18. Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vijana katika ulimwengu wa sasa wanakumbana vishawishi vingi vinavyowapelekea kumusi Mola wetu Aliyetukuka. Mimi naita vishawishi hivi mabalaa kwa sababu aliyezama katika hayo, aghlabu, hana mwisho mwema. 

Kuna mabalaa mengi, lakini tutataja manne ambayo yanatafuna vijana wa Kiislamu, na ambayo inabidi tujichunge nayo. Vijana hufanya mabalaa haya kwa sababu huu ndiyo umri wa matamanio makubwa. Ni umri pia ambapo wanahisi wana uwezo wa kufanya kila kitu, wakisahau taathira yake hayo wayafanyayo.

Kamari

Katika maeneo tunayoishi, kuna michezo mingi ya kamari ambapo walengwa wakubwa ni vijana. Hivi sasa Tanzania, vijana hutumia muda mwingi kucheza kamari kuliko kujishughulisha na kutafuta shughuli za kujitafutia riziki za halali. Hali hapa Tanzania na kwa majirani zetu inasikitisha. 

Kamari au michezo yote ya bahati nasibu hairuhusiwi katika Uislamu; na hivyo vijana wanapaswa wajiepushe nayo. Qur’an inasema: “Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet’ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa…” [5:90].

Zinaa

Wakati duniani ikiadhimisha Siku ya Vijana Duniani, ni vema kutambua kuwa uzinzi (zinaa) una madhara kiafya na kijamii. Madhara ya kiafya ni pamoja na maradhi ya kuambukiza. Madhara ya kiijamii ni pamoja na kuibuka tatizo la watoto wanaozaliwa nje ya taasisi ya ndoa na hivyo kukosa malezi ya wazazi wawili.

Katika jamii iliyofisidika, hufikia hatua ya wazazi kuisifia zinaa na kuona ni jambo la kawaida huku wakipeana majina eti “boy friend’ na ‘girlfriend.’ Ni kwa sababu hii ndiyo maana Uislamu umeharamisha zinaa, kama alivyoikemea: “Wala msikaribie zinaa hakika hiyo zinaa ni uchafu mkubwa na ni njia mbaya kabisa.” [Qur’an, 17:32].

Saidi Khamis Mkama katika kitabu cha, ‘Madhara ya Zinaa Duniani na Akhera,’ anasema kijana akishajiingiza katika zinaa, kinachotarajiwa ni ukosefu wa adabu, huenda kijana huyo akakosa kuaminika hata kwa ndugu au katika nyumba za majirani na marafiki zake.

Ulevi

Hatari nyingine inayotafuna vijana ni kujihusisha katika masuala ya ulevi. Ulevi unazalisha maasi mengine lukuki kwa sababu pombe hushawishi mtu afanye maasi mengine kadhaa wa kadhaa ikiwemo zinaa, ubakaji, uporaji, ugomvi, matusi, mauaji na kutembea uchi.

Ulevi pia umekatazwa vikali katika Qur’an katika Aya ile ile iliyokataza kamari, pale Mwenyezi Mungu aliposema “Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet’ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa…” [5:90].

Kuacha sala

Kutekeleza nguzo ya sala tano ni mtihani mzito kwa vijana wengi, licha ya Mwenyezi Mungu kusema katika Qur’an: “Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.” Sala ni nguzo ya pili katika nguzo tano za Uislamu, ikitanguliwa na Shahada. Nayo ni nguzo muhimu kwa sababu Mtume, katika Hadithi tofauti tofauti, amesema tofauti baina ya Uislamu na ukafiri ni sala na kwamba asiyesali amelaaniwa.

Sala ina faida nyingi ikiwemo kuzuia machafu. Mwenyezi Mungu anasema: “… Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.” [29:45]. Ukichunguza utagundua kuwa si rahisi mtu akawa anasali halafu akaendelea na ulevi, kamari na zinaa.

Sala pia inafuta dhambi, inatufanya tuwe wanyenyekevu na pia inaunganisha Waislamu wakutanapo msikitini kwa ajili ya sala na hutuondolea shida zetu, kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu: “Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri. Ni mengi ambayo yanaweza kuzungumzwa kuhusu siku ya vijana duniani na mustakabali mzima wa vijana lakini sisi tutamatishe kwa kwa kunukuu maneno ya Mwenyezi Mungu: “Na ambao wanafanya uharibifu katika ardhi hao ndiyo watakao pata laana na watapata nyumba mbaya.” [Qur’an, 13:25].

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close