4. Jamii

Tunao wajibu wa kuwalinda watoto walemavu

Watoto walemavu ni sehemu muhimu ya jamii yetu hivyo wanayo haki ya kufurahi na kujumuika katika familia. Watoto hawa wana ndoto kama watu wengine. Wapo wanaotamani kuwa Masheikh, madaktari, walimu, wahandisi, wafanyabiashara, wakulima nk.

Ili kuzifikia ndoto hizi ni jukumu la jamii kuwatengenezea mazingira rafiki. Mazingira hayo yatawarahisishia kupata huduma muhimu kulingana na ulemavu wao. Kwa kuanzia, ni jukumu la wazazi/ walezi na ndugu wa karibu kuwathamini watoto walemavu sawa na watoto wengine.

Ni makosa makubwa kwa wazazi kuwaona watoto hawa kama mzigo au laana kutoka kwa Mungu. Imani hizi huwadhoofisha watoto hawa na kuwanyima fursa ya kutimiza ndoto zao. Ni muhimu kufahamu kuwa, watoto walemavu wanahitaji msaada maalum kuanzia katika ngazi ya familia ili kufanya maisha yao kuwa ya furaha sawa na watoto wengine.

Aidha, msaada huu unatakiwa kulenga kuwafanya watoto hawa waweze kujitegemea wao wenyewe badala ya kusubiri hisani ya wanafamilia.

Katika jamii yetu kuna walemavu wa namna mbalimbali. Miongoni mwao ni walemavu wa viungo. Katika makala hii tutajikita zaidi katika kuwazungumzia walemavu hawa. Watoto hawa wanakabiliana na changamoto nyingi. Kwa sababu hiyo basi, ili kuonesha kuwa watoto hawa wanathaminiwa, ni muhimu kufanyike mambo yafuatayo katika ngazi ya familia.

Kuwarahisishia mijongeo

Jambo kwa kwanza la kufanya ni kuwarahisishia mijongeo yao. Hapa tunazungumzia kuwawezesha kutoka sehemu moja hadi nyingine. Hii inaweza kufanyika kwa kumnunulia baiskeli maalumu na kuhakikisha nyumba ina sehemu [ngazi] maalum inayowezesha mtoto mwenye ulemavu kupita bila usumbufu. Hali hii itamuwezesha kujitegemea na kufanya mambo yake kwa haraka bila kuhitaji usaidizi wa mara kwa mara.

Mazingira rafiki chooni

Pili, kwa upande wa chooni, hakikisha mazingira ya chooni na bafuni ni rafiki kwa mtoto wako, ikiwezekana kuwe na choo na bafu maalumu kwa ajili ya mtoto mlemavu. Hii itamuepusha na hatari ya kupata maradhi kutokana na hali yake.

Mahali salama pa kulala

Hakikisha unampatia mtoto wako mahala salama pa kulala. Ni muhimu kimo cha kitanda kiwe cha kawaida ili aweze kupanda na kushuka bila matatizo. Ni muhimu pia, katika chumba chake kusiwe na vitu vingi.

Ni ukweli kuwa, katika baadhi ya nyumba zetu huwa tunatumia vyumba vya watoto kama sehemu ya kuhifadhi vitu mbalimbali, jambo ambalo ni hatari kwani vitu hivyo vinaweza kuwasabibishia majeraha watoto kwa kuangukiwa na vitu hivyo.

Michezo na burudani

Ni wajibu wa familia kumuwezesha mtoto mlemavu kushiriki katika shughuli za kimichezo na burudani. Hali hii itamchangamsha na kumfanya mwenye furaha muda wote. Kwa kuzingatia kuwa watoto walemavu hawawezi kushiriki katika michezo kama watoto wengine, ni jukumu la familia kuwanunulia vifaa maalumu vya michezo ili na wao waweze kushiriki bila vikwazo.

Kuwachanganya na ndugu na marafiki

Watoto wengi walemavu hunyimwa fursa ya kushiriki katika shughuli za kijamii. Kwa sehemu kubwa, watoto hawa hufichwa ndani kwa sababu mbalimbali zisizo na msingi, ikiwemo familia kuona aibu kuwatoa hadharani. Hali hii huwanyima fursa watoto kuchanganyika na wenzao kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali. Hivyo basi, ni jukumu la wazazi, ndugu na familia, kuhakikisha watoto walemavu wanaruhusiwa kushiriki katika mambo yote ya kifamilia bila kubaguliwa.

katika baadhi ya nyumba
zetu huwa tunatumia vyumba vya watoto kama sehemu ya kuhifadhi vitu mbalimbali, jambo ambalo ni hatari kwani vitu hivyo vinaweza kuwasabibishia majeraha watoto kwa kuangukiwa na vitu hivyo.

Kuwapatia elimu

Ni jukumu la familia kuwapa watoto walemavu fursa ya kusoma kwani ni wazi kuwa, watoto hawa wana uwezo kama watoto wengine. Pamoja na jukumu la wazazi, pia ni jukumu la shule zetu kuwajengea mazingira mazuri ili waweze kusoma bila vikwazo. Kama ilivyotajwa katika ngazi ya familia, tunategemea pia shule ziweze kujenga miundombinu rafiki inayowezesha watoto hawa kusoma bila vikwazo.

Tunahitimisha kwa kusema kuwa, watoto walemavu wana haki kama walivyo watoto wengine. Familia na jamii kwa jumla, ina wajibu wa kuwalinda na kuwawezesha kufikia ndoto zao. Tunao wajibu wa kuwahimiza wazazi kuwajengea mazingira mazuri kuanzia katika ngazi ya familia. Mazingira haya, yatawasaidia watoto walemavu kuishi kwa furaha na amani. Pia, yatawarahisishia watoto hawa kuzifikia ndoto zao.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close