4. Teknolojia

Wajasiriamali wanawake na fursa za mitandao

Kutokana na utandawazi na maendeleo ya tekinolojia mambo mengi yamekuwa mepesi zaidi sasa, mfano mzuri ni mambo ya kuonekana mwezi na upashanaji habari. Ufikishianaji wa taarifa umekuwa mwepesi mno kiasi kwamba mtu anaweza kupata habari ya kuonekana mwezi kutoka popote duniani.

Mwanamke wa Kiislamu, kaa, jitathmini, jipange ujue utafaidikaje na mitandao ya kijamii na uachane na fikra potovu za kujua kuwa mitandaoni ni sehemu ya kupiga stori na kujianika kwa picha zisizo na maadili.

Mitandao ya kijamii inasaidia watu waliyo maeneo mbalimbali kupeana taarifa kwa wepesi. Kupitia mitandao ya kijamii, mijadala huendeshwa badala ya vijiweni na mitaani. Watu huungana katika makundi ya Whatsap, Facebook au instagram, hali ya kuwa kila mtu yuko kwake.

Uislamu na mwanamke
Uislamu ni dini inayomlinda, kumtunza na kumpa heshima kubwa mwanamka kwa taratibu mbalimbali zilizoainishwa toka kwa Allah na Mtume wake. Mwanamke wa Kiislamu hapaswi kutoka hovyo nyumbani; na akitoka basi kwa ruhusa maalumu na awe ndani ya stara ili asije kupata madhara yoyote kutokana na machafu yaliyosheheni barabarani.

Mwanamke wa Kiislamu vilevile hapaswi kusafiri peke yake safari ndefu bila ‘mlinzi’ (mahram aliye baleghe), hata akitaka kwenda kufanya ibada ya hijja.

Tukirudi katika mitandao ya jamii, tunaona imekuwa wazi mno, ni jinsi wewe mhusika utavyoweza kuitumia. Ukiweza kuwa mtu mwema na kusambaza mema basi mtandao pia utakusaidia na ukiamua kuwa mtu muovu; na kuusambaza uovu wako bado mtandao wa kijamii utakusaidia katika kuitafuta laana hiyo.

Mitandao kwa dada zetu wa Kiislamu
Leo nilitaka tugusie kidogo umuhimu wa kuitumia mitandao vizuri hususan kwa dada zetu wa Kiislamu. Mwanamke wa Kiislamu anayejitambua anaweza akakaa ndani kwake amesitirika vema na bado akapata faida sana kupitia mitandao ya kijamii. Unaweza ukawa mjasiriamali mkubwa tu kwa uweza wa Allah kupitia hii mitandao tunayoijua.

Uzuri wa mitandao ni kwamba, unaweza ukaanza muda wowote kuuza huduma au bidhaa yako bila kubugudhiwa na mamlaka yoyote ili mradi unachokiuza hakivunji sheria za nchi. Mathalan, kupitia mitandao ya Youtube, kuna wadada wanaofundisha mapishi na kila watu wanavyozidi kutembelea kwenye chaneli yake,wahusika hujiongezea kipato.

Na siyo lazima ujipige picha (ambayo ukifa hakuna wa kuweza kuifuta)ili kupata faida. Kinyume chake, unaweza kuanzisha jambo lolote halali au huduma yoyote njema kwa jamii na ukakuta jamii inakukubali na kuhitaji huduma yako kokote nchini. Hivyo dada wa Kiislamu kaa ujifikirie na uamue kubadilika.

Dada wa Kiislamu, jiulize, tangu uanze kujipiga picha na kujianika mitandaoni umefaidika na nini? Je, dini yako inakuruhusu kujianika hadharani kama unavyofanya kupitia ‘status’ za whatsap  au Facebook? Hivi unajua kuna wakina dada wanaingiza pesa kwa kutengeza pilipili, achali au siki nyumbani kwao na kuuza kupitia mitandao ya kijamii. Maa shaa Allah, hao ni wakina dada wanaojitambua, walioona fursa na kuzitumia, bila kuvuka mipaka ya kisharia. Waligundua kuwa, siyo lazima kukodi fremu ili uanze kuingiza pesa. Wakinadada hawa, walichofanya ni kusajili bidhaa zao, mamlaka zikawakagua na kuwapa maelekezo yote ya kutengeza bidhaa zao kwa ubora.

Ninamjua dada aliyeanza taratibu kuuza keki mitandaoni, akaanza kuboresha vifungashio na muonekano, na sasa anapokea oda kubwa kutoka maeneo mbalimbali kupitia mitandao, hususan mtandao wa Instagram.

Alianza na ‘oven’ ndogo kwa ajili ya kuoka keki zake; na sasa Alhamdulillah, wakati mwengine huomba kutumia jiko la kampuni ya utengezaji mikate iliyo karibu naye. Huyu dada ana ndugu wa kiume anayehusika na kusafirisha bidhaa mpaka eneo husika, kadri oda zinavyotoka.

Wakati huyu akifanya hivyo, we dada mwengine unaweza kutengeza vitafunwa, ubuyu nk na kwenda kupeleka kwenye migahawa mbalimbali iliyoenea kila kona za majiji yetu, ukiwauzia kwa bei ya jumla. Ukiweza kujiendeleza na kuithamini kazi yako, unaweza kuanza kupata oda kutoka migahawa mikubwa zaidi. Jifunze utengenezaji wa chochote ukipendacho hata kupitia mitandao hiyo hiyo kama wa Youtube na ukishaiva kwenye utengenezaji wake anza kuuza huduma yako.

Lenga kwenye kufikisha huduma kwa watu wengi zaidi, na hela itakufuata kwa kukukimbilia kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kuna wanawake wananunua  nguo za watoto kutoka duka la jumla na kuwafikishia wengine kwa rejareja kupitia mitandao ya kijamii.Ukiweza kujizatiti
na kujitangaza kila siku kupitia mitandao mbalimbali, unaweza kuingiza pesa nzuri kwa mwezi kuliko mfanyakazi wa ofisini. Mtaji wako mkubwa ulikuwa ni ile simu uliyoacha kurusha picha zako mitandaoni na kifurushi cha intaneti tu.

Kuna wanawake wamejiunga pamoja kuwa washonaji kwa kutumia mashine tu za vyerehani lakini kwa uwezo wa Jalali  na kutumia mitandao vizuri, sasa wana wateja wengi zaidi. Mwengine anunue mashine ya kudarizi, atenge chumba kwa kazi hiyo nyumbani kwako anaweza akawa mtu tofauti kimaisha. Ukijitangaza kuwa unadarizi nguo za makampuni, kuremba au kutia maua shuka,unaweza kuwa mjasiriamali mkubwa na kubadili maisha yako.

Ushawahi kujiuliza kwenye jiji lako kuna mabanda mangapi ya chipsi kuku. Umeshawahi kufikria kuanza ufugaji wa kuku ili uwe msambazaji mkubwa wa kuku au mayai? Unapenda kazi za bustanini? Kama una eneo kubwa la kutosha nyumbani kwako, unaweza kuwa tajiri kwa kuuza maua ndani na nje ya nchi? Hizi zote ni kazi ambazo unazoweza ukajifungia ndani tu na ukaingiza pesa nzuri. Kwa biashara zote hizi unaweza
kutumia mitandao ya kijamii kupata wateja.

Kifupi kupitia matumizi mazuri ya mitandao kuna fursa za faida nyingi mno, lakini muhimu zaidi, hakuna biashara bora kuliko kumuamini Allah na Mtume wake, na kisha kupigania dini ya Allah kwa mali zetu na nafsi zetu. Alhamdulillah sasa kuna hadi chuo kikuu cha dini mtandaoni. Mwanamke unaweza ukakaa ndani na kuendelea na shughuli zako huku unasoma dini na ukimaliza unapata cheti chako.

Ukishasoma na kumtambua Muumba wako na Mtume wake, fikisha kwa wengine kupitia mitandao ya kijamii. Usisahau sadaqa iliyo bora ni kujifunza Qur’an na kuifundisha. Mwanamke wa Kiislamu, kaa, jitathmini, jipange ujue utafaidikaje na mitandao ya kijamii na uachane na fikra potovu za kujua kuwa mitandaoni ni sehemu ya kupiga stori na kujianika kwa picha zisizo na maadili.

Show More
Back to top button
Close