4. Teknolojia

Tupige vita tamthilia zinazoharibu watoto wetu

Miaka 30 liyopita, inawezekana hakukuwa na mtu aliyeweza kutabiri mabadiliko hasi tunayoshuhudia sasa katika sekta ya sanaa ya maigizo inayojumuisha filamu, tamthilia na michezo ya jukwaani.

Hivi sasa filamu na tamthilia nyingi zinazokodishwa au kuuzwa mitaani kwa njia ya flash na ‘CD’ na zile za kulipia zinazorushwa na visimbuzi (decoder) mbalimbali kwa kiasi kikubwa zimejaa maudhui yanayoshawishi zinaa, ulevi na ushoga. Hili ni jambo mbaya na la fedheha kwa taifa letu ambalo kihistoria limekuwa likijivunia maadili yake mema yenye msingi katika dini, hususan Uislamu.

Wazazi wanahusika mporomoko huu wa maadili kwani wao ndio wanaowaruhusu watoto kutazama tamthilia na wakati mwingine huwakodishia ‘CD’ za Kikorea, Kichina, Kihindi, Kijapani na Kifilipino, pamoja na filamu za Kitanzania maarufu kama ‘Bongo movie’ na kuwapa wazitazame pasipo kujali madhara yake kimaadili, kitaaluma na kiakili.

Ikumbukwe kuwa msingi mzuri wa taifa lolote hujengwa kuanzia katika ngazi ya familia. Tukiharibikiwa huko, hatuna chetu tena. Tutaishia kuwa na taifa la wazinzi waliokubuhu, walevi wa kupindukia, mashoga kila kona, vijana wacheza kamari saa 24!

Kwa hali hiyo, sisi Imaan Gazeti twashauri tusilifumbie macho jambo hili vinginevyo katika siku za usoni tutakuwa katika wakati mgumu sana. Bahati mbaya sana ni kuwa uharibifu huu wa maadili ukienea, hakuna atakayesalimika.

Jamii ya sasa iliyopanuka kimawazo kutokana na kukua kwa teknolojia katika kila sekta haitegemei tu elimu aliyoipata mtu shuleni bali hata mazingira anayoishi. Mazingira anayoishi mtu yanatoa fursa nzuri ya kujifunza na kuelewa wajibu wake kwake na kwa wengine.

Kwa mantiki hiyo, wazazi wanapaswa kutafakari upya majukumu yao kwa watoto ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na changamoto zake. Sababu ni kwamba, ustawi wa taifa unaanzia nyumbani, na kinyume chake ni kuporomoka kwa taifa kunakoanzia nyumbani.

Wataalamu wa saikolojia wanasema kwamba akili ya mtoto ni rahisi kushika chochote – kiwe kizuri au kibaya ni lazima tu kitakaa akilini mwake. Kama tujuavyo, watoto ndio ambao wanategemewa kuwa wazazi wa kesho. Swali na mjadala unaobaki ni je, tunavyozidi kuwaruhusu watoto kutazama filamu au tamthilia upeo wao wa akili utakuwaje hapo baadae?

Ifahamike wazi kuwa watoto ni mtihani ambao Mola Muumba atautolea majibu Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’ an:

“Na jueni ya kwamba, mali zenu na watoto wenu ni fitna (mtihani), na kwamba kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.” [Qur’an, 8:28].

Hivyo, ni lazima tutafute suluhu ya kadhia kwa kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza kwa miaka ijayo. Endapo watoto wataendelea kuangalia tamthilia zinazoshawishi ngono, basi kuna hatari ya mila, desturi na maadili ya Kiislamu na Kitanzania kupotea kabisa na watoto kuishi kama wanyama.

Rai yetu kwa wazazi na walezi ni kwamba wawajibike kuwalea watoto wao katika mwenendo mzuri na wa uadilifu; pia kuwasimamia watoto katika utekelezaji wa kiibada. Kutofanya hivyo ni kufeli (kuanguka) mtihani.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close