4. Teknolojia

Tudhibiti matumizi ya vyombo vya habari kwa Watoto

Radio, televisheni, majarida, sinema, mitandao ya kijamii, simu za mkononi ni teknolojia zenye manufaa makubwa kwa watu.

Kupitia teknolojia hizi za mawasiliano, watu hupashana habari. Pia watu hujifunza mambo mapya na pia kuburudika.

Kwa watoto wa rika tofauti, teknolojia hizi zinaweza kutumika katika mchakato wa kutafuta elimu. Njia hizi za mawasiliano zinaweza kufundisha watoto nguzo za Imani ya dini yao tukufu ya Uislamu, maadili ya kidini na vilevile namna ya kutekeleza ibada mbalimbali. Elimu ya mazingira pia inaweza kufikishwa kwa teknolojia hizi.

Kuna watu wanaoona ubaya tu wa teknolojia hizi za mawasiliano. Yaani wanaamini kuwa zimejaa upotofu tu na hazina manufaa!

Lakini watu hawa wanapaswa kuangalie namna zilivyoleta manufaa wakati maradhi ya Covid -19 yalivyoshamiri!

Nchi zilizoendelea zote zilifunga shule lakini masomo yaliendelea kama kawaida kupitia teknolojia mbalimbali kama vile Moodle na nyinginezo. Walimu waliendelea kufundisha siyo kwa kutuma notsi tu bali uso kwa uso. Wanafunzi nao walipata fursa ya kuuliza maswali, kama vile wapo darasani.

Na waliofaidika siyo nchi za kikafiri pekee bali hata pia nchi za Kiislamu. Nilipata bahati ya kukutana na wanafunzi wa Kitanzania waliorejea nchini kutoka Saudi Arabia kwa ajili ya likizo, wakanieleza namna masomo yalivyokuwa yakiendelea hata wakati wa maradhi ya Covid -19 kupitia teknolojia! Kumbuka kwamba, wengi wao walikuwa wakisomea fani za dini!

Hata hapa Tanzania, masomo yaliendelea katika shule mbalimbali, hususan za binafsi, kwa kutumia teknolojia tofauti tofauti kulingana na uwezo wa shule husika.

Wapo waliotumia Moodle. Wapo waliotumia video iliyorekodiwa mapema na kutumwa kwa wanafunzi. Wapo waliotumia mitandao ya kijamii. Wapo waliotumia barua pepe… alimradi kila shule ilijikuna mpaka pale mkono ulipofikia.

Nadhani ni shule za serikali pekee ambazo hazikufanya chochote, lakini wanafunzi wao bao walinufaika kupitia mipango mingine ya kitaifa.

Mathalan, tunajua kuwa taasisi nyingi za vyombo vya habari zilianzisha vipindi vya elimu vya ngazi mbalimbali, ambapo walimu walikwenda studio na kurekodiwa wakifundisha mada mbalimbali!

Si hivyo tu, shule mbalimbali ziliandaa mitihani na notsi na kuzirusha mitandaoni, hususan kupitia makundi mbalimbali ya WhatsApp ya wazazi na wanafunzi. Mitihani hiyo haikuishia kwenye makundi hayo tu ya wazazi. Kama kawaida ya ukarimu wa kitanzania, nao wakawatumia ndugu zao, hatimae ikaenea kila mahali. Haya ni matumizi mazuri ya teknojia.

Nasikia, kutokana na balaa lile la Covid – 19, hatua za muda mfupi zilizochukuliwa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kusoma kama kawaida zimezalisha athari na mabadiliko chanya ya muda mrefu.

Moja ya athari chanya itakayobaki baada ya kwisha kwa Covid-19, ni taasisi kuja na mipango ya kuanzisha kozi nyingi zitakazofundishwa kupitia mtandaoni. Covid -19 imetufundisha kwamba, kumbe inawezekana masomo kuendeshwa kwa teknolojia bila ya mwalimu na mwanafunzi kuwa pamoja na kuonana uso kwa uso darasani. Covid-19 pia imetufundisha kuwa, hatutumii teknolojia za mawasiliano ipasavyo.

Lengo la mifano yote hiyo ninayoitoa ni kujenga hoja kuwa teknojia za mawasiliano – radio, televisheni, simu za mkononi ikiwemo janja, intaneti na vikorombwezo vyake kama vile mitandao ya kijamii, ni upanga wenye ncha mbili – vinaweza kutumika kufaidisha jamii na inaweza kuleta hasara.

Na katika mifano hiyo, sijataja vyombo vya habari vya Kiislamu. Majarida kama vile Gazeti Imaan, pia radio kama vile Radio Imaan na televisheni kama TV Imaan na Mahaasin TV vimeleta faida kubwa ya kuwaongoa watu.

Kwa hivyo basi, si sahihi kupambana na teknolojia hizi, bali mapambano yetu yalenge kupinga matumizi mabaya ya vyombo hivi ambavyo ni Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliyetubariki akili ya kuviunda lakini akatuwekea mipaka katika matumizi.

Teknolojia za mawasiliano katika muktadha wa familia

Baada ya kueleza yote niliyoyaeleza, naleta hoja kuwa ni muhimu sana Waislamu tutafute pesa ya kununua na kumiliki vyombo hivi na kuvitumia katika namna inayompendeza Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na bila kuchupa mipaka yake.

Kwa watu wazima, baleghe, tunaojitegemea, kwa kuwa tunajitambua ni wajibu wetu kujidhibiti ili tusichupe mipaka ya matumizi ya teknolojia hizi.

Lakini, hali ni tofauti kwa watoto. Ni wajibu wetu wazazi kudhibiti matumizi ya teknolojia hizi kwa watoto ili kuwalinda wasiathirike. Zipo tafiti nyingi zilizofanyika zinazoonesha namna watoto wanavyooathirika kwa namna hasi au chanya (kutegemeana na maudhui) kwa kutumia teknolojia hizi ikiwemo utazamaji televisheni na kuperuzi mitandao ya kijamii.

Sio siri kwamba, katika vyombo hivi, hususan mitandao ya kijamii, kuna maudhui mengi yasiyofaa, ikiwemo picha za utupu, matusi, miziki, video zinaozonesha ukatili, mienendo isiyokubalika katika Uislamu na hususan inayopingana na Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Tunawajibika, kama wazazi, kuwalinda watoto na maudhui haya kwa sababu watoto wenyewe hawana uwezo wa kupembua jema na baya, na kila waonacho basi wao huiga tu.

Kwa kuliona hilo ndiyo Waswahili wakasema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Maana yake ni kwamba, ni muhimu sana sisi wazazi tuishi vile ambavyo tungependa watoto waishi kwa sababu wao hujifunza kwetu kwa kutuiga.

Kuna jirani zangu ambao walikuwa wakiishi maisha yasiyo na maadili, lakini wakiwasukuma watoto wao waende madrasa wakitumaini watakuwa watu wazuri, lakini haikuwezekana. Wengi kati ya watoto wao wameishia kuwa wezi, makahaba, wavuta bangi na kadhalika. Hii ni kwa sababu wazazi wao hawakuwa mfano mwema.

Nikirejea katika mada ya teknolojia za mawasiliano, kwa kuwa wazazi tuwe wa kwanza kuepuka maudhui yasiyo na maadili. Isiwe mzazi anamtoa mwanawe kwenye TV ili yeye apate kuangalia yasiyofaa peke yake.

Kwa hiyo, udhibiti wa watoto dhidi ya kuangalia mazudhui yasiyofaa isiwe tu kwa kuwafukuza watoto lakini pia kwa wazazi kutoangalia hayo wasiyotaka watoto wayaone. Vinginevyo, ujumbe wanaoupata watoto ni kuwa, ukiwa mkubwa kuangalia maudhui yasiyofaa ni ruhusa. Hii si sahihi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close