4. Teknolojia

Teknolojia ni neema ikitumika ipasavyo katika malezi ya watoto

Teknolojia ni sehemu ya maisha yetu. Karibu nyanja zote za maisha zimenufaika kwa namna moja au nyingine na teknolojia. Kwa mfano, ukigusa sekta ya mawasiliano utaona wazi mchango wa teknolojia, hivyo hivyo, katika usafiri, afya, elimu, kilimo, ufugaji na ujenzi. Kwa jumla, teknolojia imerahisisha maisha yetu.

Fursa kubwa inayoletwa na teknolojia ni neema kubwa kwa watoto kama itaweza kutumika vyema hasa katika sekta ya elimu na malezi. Wataalamu wengi duniani wamekuwa wakiumiza vichwa ili kuunganisha sekta ya elimu na teknolojia. Leo hii tunazo kazi nyingi sana za kielimu zinazomlenga mtoto ambazo zipo katika mifumo mbalimbali ya kidijiti.

Baadhi ya kazi maarufu za watoto zilizopo katika mfumo wa kidijiti ni vibonzo jongevu (katuni-hai). Hizi ni filamu fupifupi zenye maudhui mbalimbali yenye malengo ya kufundisha na kutoa burudani kwa watoto. Huko nyuma, filamu hizi zilionekana kama burudani tu, lakini siku hizi, vibonzo jongevu vinatumika sana katika uga wa taaluma.

Mfano, kupitia filamu hizi, watunzi wamekuwa wakipitisha maarifa muhimu kwa watoto kama vile Hisabati, Sayansi, Lugha (hasa lugha za kigeni kama Kiarabu, Kiingereza, Kichina na kifaransa), Jiografia, Uhandisi n.k. Filamu hizi zimethibitika kuwa, moja kati ya mbinu bora za kufundishia. Teknolojia imerahisisha sana upatikanaji wa kazi hizi ambazo zinaweza kutazamwa kupitia televisheni, simu za mkononi, vishkwambi (tablet) na kompyuta. Hii ni kusema kuwa kazi hizi zinaweza kutazamwa mahali popote na kwa namna mbalimbali. Pamoja na kuwa watumiaji wa mjini ndiyo wanufaika wakubwa, hata wale wa vijijini wanayo fursa ya kutazama kazi hizi. Licha ya vibonzo jongevu, wataalamu pia wamekuwa wakibuni michezo ya compyuta (games) mbalimbali kwa malengo ya kuwafundisha watoto. Ipo michezo inayowafunza Hisabati, matamshi, uandishi, usomaji wa herufi, utambuzi wa maumbo na rangi, aina za wanyama n.k.

Swali la kujiuliza ni je, vibonzo jongevu na michezo (games) vina msaada gani kwa watoto? Kwa hakika kuna faida nyingi kwa mtoto anayepata fursa ya kuona kazi tajwa. Baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo:

Mosi, mambo mengi yanayoonekana katika kazi tajwa ni darasa la ziada kwa watoto. Mambo haya hufundishwa madarasani kwa namna tofauti. Kitendo cha kuyaona katika sura nyingine huwapa watoto fursa ya ziada ya kujifunza zaidi.

Pili, kazi hizi hujikita zaidi kuwafunza watoto namna ya kutatua matatizo (problem solving), yaani zimetengenezwa kuonesha tatizo na ufumbuzi wake kwa namna iliyo bora. Mbinu hii ni njia nzuri ya kumuandaa mtoto kukabiliana na changamoto za kimaisha na kuzitatua kirahisi. Pia, njia hii inakuza ubunifu kwa mtoto kwa kuonesha namna mbalimbali za kufanya jambo hilohilo moja.

Tatu, kazi hizi huhimiza ushiriki wa mtoto kikamilifu (active participation). Ruwaza za kisasa zinahimiza sana ushiriki wa mtoto katika zoezi la ujifunzaji. Kwa mfano, katika michezo mtoto ndiye mtendaji mkuu. Teknolojia ipo tu kwa lengo la kumuongoza na kumsaidia pale anapokwama. Kwa hali hii, mtoto huwa mshiriki rasmi katika zoezi la ujifunzaji. Aidha, kuna matumizi makubwa ya viungo vya mwili na akili kwa pamoja katika mchakato wa ujifunzaji.

Nne, njia hizi za kujifunza zinakuza matumizi ya teknolijia kwa watoto. Hakuna ubishi kuwa mzazi/mlezi anapowaruhusu watoto kutazama vibonzo jongevu na kucheza michezo (games), huwaongezea watoto wake uwezo wa kutumia vifaa vya kidijiti kama vile simu, kompyuta na televisheni. Vifaa hivi ni sehemu ya maisha, hivyo mtoto anapoweza kuvitumia katika umri mdogo hurahisisha maisha yake kwa kiasi kikubwa.

Tunahitimisha kwa kuwakumbusha wazazi kuwa, pamoja na faida za teknolojia tulizojadili hapo juu, bado kuna changamoto nyingi katika maisha ya teknolojia. Ni muhimu mzazi kuwa makini kwa kuhakikisha kuwa, teknolojia inatumika kwa namna chanya.

Upo ushahidi mwingi unaoonesha kuwa, kama teknolojia haitatumika vizuri, inaweza kuleta maafa makubwa katika jamii. Ndiyo maana nchi mbalimbali duniani zimeweka sheria na kanuni nyingi zinazodhibiti matumizi yasiyofaa ya teknolojia. Wazazi mnapaswa kujifunza namna nzuri na inayofaa ya matumizi ya teknolojia kwa namna itakayowanufaisha watoto.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close