4. Teknolojia

Nguvu zaidi ziwekwe kudhibiti utapeli wa mitandaoni

Wizi wa fedha mitandaoni sasa ni janga la taifa na kilimwengu kwani matukio ya wizi yanaongezeka kwa kasi sio tu hapa nchini bali duniani kote. Pamoja na usajili wa laini za simu kupitia kitambulisho cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), bado watu wameendelea kupokea ujumbe mfupi (SMS) wa kuwataka watume fedha kupitia namba fulani.

Mbali na hao, pia wapo walioibiwa kwa hadaa ya kuulizwa maswali na kujikuta wakitoa namba zao za siri kwa matapeli waliovaa joho la watoa huduma za mawasiliano ya simu husika. Vilevile kuna wanaojifanya ndugu au jamaa wanaotuma ujumbe mfupi wa maandishi wakiomba msaada wa haraka kukabiliana na dharura fulani.

Wengine hukijifanya wametuma ujumbe kimakosa ambao ndani yake una maneno ambayo kama mpokeaji asipokuwa makini anaweza kujikuta ‘ameingizwa mjini’. Ujumbe huo, aghlabu, hugusa mambo ya tiba za kienyeji au mradi fulani wenye faida kubwa.

Ripoti ya kitengo cha uchunguzi wa makosa ya mtandao inaonesha ongezeko la matukio mengi ya uhalifu wa mitandaoni yanayoripotiwa polisi na kufanyiwa kazi lakini kuna matukio yanayotokea mitaani hayaripotiwi.

Swali la kujiuliza ni je, imekuwaje matapeli wa mtandaoni wazidi maarifa na ujanja mamlaka zetu ambazo tunaamini ziko vizuri kiteknolojia, kiasi cha kugeuza akiba za Watanzania shamba la bibi.

Kinachoshangaza ni kwamba kila tukio la wizi au utapeli linapofuatiliwa hugundulika kitambulisho kimoja cha NIDA cha mteja A na alama zake za vidole zimetumika kusajili vitambulisho vya watu ambao hana nasaba nao na hawafahamu!

Pengine hili ndilo lililomfanya Rais Samia Suluhu Hassan ahoji juu ya vitendo vya utapeli wa fedha mitandaoni vinavyoendelea kushamiri hapa nchini.

Mwezi Mei mwaka huu akiwa katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha ushonaji katika Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.

Rais Samia alishangaa wizi mitandaoni unaendelea licha ya kuwepo kwa sheria ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

“Kuna mambo huwa yanatushangaza. Kwa mfano mtakumbuka kulikuwa na sheria iliyotutaka sote tusajili namba zetu za simu na tuweke alama za vidole ili ijulikane ni nani anatumia hiyo namba, lakini bado vitendo vya utapeli na wizi wa kimtandao unaendelea na hatusikii watu wamefikishwa mahakamani,” alisema Rais Samia.

Kufuatia hali hiyo, Rais alilitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kumaliza wizi na utapeli mitandaoni.

Kwa kuzingatia kuwa tatizo la wizi wa kimtandao limeota mizizi katika nchi yetu, ipo haja kwa TCRA, Jeshi la Polisi, kampuni za mawasiliano ya simu na wataalamu binafsi wa Tehama kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha vitendo hivyo viovu vinakomeshwa.

Tusingependa kuwafundisha wataalamu wetu ndani ya TCRA, kampuni za simu na Kitengo cha Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Unit) cha Jeshi la Polisi namna ya kukabiliana na wimbi hili, lakini ifike mahali tuseme imetosha kutapeliwa

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close