4. Jamii

Taswira zetu katika tabia za watoto wetu

Watoto ni neema na dhamana kutoka kwa Allah. Ni jukumu  la lazima kwa wazazi, ndugu na jamaa kusimamia malezi yao. Namna watoto wanavyolelewa huchangia sana katika utu wao. Watoto wanaolelewa katika tabia njema kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na tabia njema. Wale wanaolelewa katika tabia za hovyo, vilevile wana uwezekano mkubwa wa kuiga tabia zisizofaa.

Wazazi na ndugu wa karibu wanao  mchango mkubwa katika kuathiri tabia za watoto. Hii ni kusema, watoto hupenda kuiga mambo mengi wanaoyaona kutoka kwa ndugu wa karibu. Tabia zinazoigwa kutoka kwa ndugu huweza kuwa mbaya au nzuri.  Uigaji huu wa watoto kutoka kwa ndugu wa karibu (hasa wazazi), ni jambo la kiasili kwani huakisi taswira za kitabia wanazoziona mara kwa mara kutoka kwa ndugu.

Kadhalika, watoto wana imani kubwa kwa ndugu zao wa karibu. Pamoja na kuwa wapo watu wengine wanaoweza kuwashawishi watoto kuiga tabia mbalimbali, bado ndugu wa karibu wana ushawishi mkubwa zaidi katika tabia za watoto. Dunia ya watoto huanzia nyumbani. Watoto huamini kuwa kila wanachokiona kinafanywa na ndugu ni sawa na kinafaa kuigwa.

Kwa kawaida, watoto huzibeba tabia nyingi zisizofaa zinazofanywa nyumbani kama zilivyo na kuishi nazo katika maisha yao yote. Baadhi ya tabia hizi huonekana ni za kawaida au pengine hudogoshwa, lakini ni tabia mbaya.

Aidha, tabia hizi huota mizizi na kukua. Athari zinapoanza kuonekana, wazazi na ndugu wa karibu huanza kunyoosha vidole kwa watu wengine, mfano marafiki na walimu, huku wakisahau kuwa kinachoonekana katika tabia za watoto wao ni taswira ya maisha yao kutoka nyumbani.

Baadhi ya tabia zisizofaa ambazo  hujitokeza sana katika maisha yetu ya nyumbani ni hizi zifuatazo:

Kusema uongo

Kusema uongo ni tabia isiyofaa. Kwa bahati mbaya tabia hii imeshtadi katika nyumba zetu. Wazazi na ndugu wa karibu tumeshiriki sana kuwafunza watoto tabia ya kusema uongo kwa namna mbili.

Kwanza, tumekuwa tukiwaongepea kwa namna mbalimbali. Namna maarufu ambayo karibu kila mtoto amepitia ni ile ya kuwadanganya kuwa utawaletea zawadi lakini haufanyi hivyo.

Pili, ni kule kusema uongo kwa watu wengine wakati ukiwa na watoto. Utamsikia mtu anapokea simu akiwa Dodoma lakini anasema: “Eeh sipo nyumbani bwana nipo Arusha na nitarudi wiki ijayo.” Hali hii hujitokeza sana na kwa bahati mbaya  watoto wanaona na kujifunza kuwa,  kusema uongo ni jambo la kawaida.

Matusi na maneno yasiyofaa

Matusi na kusema maneno yasiyofaa ni tabia nyingine inayolelewa sana kutoka nyumbani. Watu hawajizuii kuongea maneno yasiyofaa mbele ya watoto. Kwa hali hii watoto wetu wanakua na kuzoea kutumia maneno haya kama maneno ya kawaida.

Aidha, wazazi wengi wanapoudhiwa na watoto hupenda kuwaita kwa majina mbalimbali yasiyofaa. Utasikia mtu anamuita mtoto ‘mbwa weee’, ‘paka wewe,’ ‘shetani mkubwa,’ ‘nyang’au wewe’ nk. Matokeo ni jambo la kawaida kabisa mtoto huyu atakapoudhiwa kujibu mapigo kwa kumuita majina hayohayo aliyosikia  nyumbani.

Kusengenya na kujadili siri za watu.

Kwa sehemu kubwa, tumekuwa tukisengenya na kujadili siri za watu  mbele ya watoto wetu. Katika dini yetu tukufu ya Kiislamu usengenyaji na kujadili siri za watu ni mambo yanayokatazwa. Ubaya wa kusengenya  ni kuwa, baadhi ya watu tunaowajadili  ni watu wetu wa karibu ambao watoto wetu wanafahamu.

Kitendo hiki kinawavunjia heshima mbele ya watoto na kutishia uhusiano wetu na watu hao. Hatari ya kusema aibu za watu mbele ya watoto ni kwamba, ni rahisi maneno haya kuwafikia walengwa waliosengenywa na kuleta tafrani baina ya pande husika.

Ugomvi na kupigana

Wapo wazazi na ndugu wa karibu ambao maisha yao yamejaa magomvi. Matendo haya hufanyika wazi mbele ya watoto. Utakuta baba anazozana na mama mbele ya watoto.  Wengine huenda mbali na kuwapiga wake zao mbele ya watoto.

Matendo haya kama yatajitokeza kwa  kurudiarudia huganda katika ubongo wa watoto. Watoto wanaolelewa katika familia hizi mara nyingi huwa na mkono mwepesi katika kuwapiga watoto wenzake.

Tunaweza kulaumu sana kitendo cha watoto kuwa wakorofi na kudhani kuwa wamejifunza kwa watu wengine tabia hizi, ilhali tabia zao zinaakisi waliyojifunza kutoka kwa wazazi.

Tunahitimisha makala yetu kwa  kuwaasa wazazi na ndugu wa karibu  wawe makini na tabia wanazozidhihirisha mbele ya watoto. Tunapaswa kufahamu kuwa, tabia za ndugu wa karibu zina mchango mkubwa katika muonekano wa watoto tunaoishi nao.

Tags
Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close