1. Fahamu Usiyoyajua4. Jamii

Samaki salmon: Anaishi maji baridi na chumvi

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Mjuzi wa kila kitu na Mwenye uwezo juu ya kila kitu, ameumba viumbe vyake ili tuwaidhike kwavyo na kupata mazingatio. Naye Mwenyezi Mungu humpa elimu amtakaye katika viumbe vyake na anamnyima amtakaye. Atakayepewa elimu amshukuru Allah na atakaye nyimwa pia amshukuru.

Juma hili katika ukurasa huu, tutajifunza mambo kadhaa kuhusu samaki maarufu duniani aitwaye Salmon ambaye siyo tu ana maajabu makubwa. Pia, kutokana na maisha ya samaki salmon tunapata mafunzo makubwa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa elimu ya viumbe, ukiacha kuwa na minofu mitamu, mafuta ya samaki huyu ni muhimu sana katika kulinda afya ya miili yetu dhidi ya maradhi. Pia, mafuta yake yanasaidia ukuaji mzuri wa mwili na akili hususan kwa watoto wadogo.

Samaki huyu anapatikana kwa wingi zaidi kwenye mito iliyopo Amerika ya Kaskazini (North America). Kuna takriban aina saba za salmon wapatikanao katika Bahari ya Pacific, ambapo watano hupatikana katika maji ya America ya Kaskazini wakiwemo chinook, coho, chum, sockeye, na pink. Aina mbili masu na amago wanapatikana katika bara la Asia. Pia, kuna aina moja hupatikana katika bahari ya Atlantic.

Katika aina hizo, chinook au king salmon ndiyo wakubwa zaidi ambapo wale wakubwa zaidi huweza hufikia urefu wa hadi mita moja na nusu na uzito wa hadi kilogramu 50. Pink salmon ndiyo wadogo zaidi ambapo wakubwa zaidi huweza kufikia urefu wa sentimita 76 na uzito wa hadi kilogramu 5.4.

Kuhusu rangi, salmon wanakuwa na muonekano tofauti kutegemeana na aina. Wapo wenye rangi ya fedha au kijani na vidoti au mistari myeusi na kadhalika.

Maisha ya samaki hawa yanaanzia pale jike anapotaga mayai maeneo ya juu ya mto, sehemu yenye maji ya baridi (yaani yasiyo na chumvi), kisha dume huyarutubisha mayai hayo.

Baada ya kutotolewa, samaki hawa hukaa mtoni kwa muda kadhaa mpaka wanapokuwa kiasi cha kuweza kujitafutia chakula wenyewe na kujilinda. Kuanzia hapo wanaanza safari yao ya maajabu makubwa.

Baada ya kukua na kukomaa, samaki salmon huanza kusogea karibu na bahari. Katika kipindi hiki, mabadiliko kwenye mwili wake huanza kutokea ili kumuandaa aweze kuishi kwenye maji ya chumvi.

Baada ya mabadiliko ya mwili kukamilika na kuwa sasa anaweza kuendana na mazingira ya maji ya chumvi na hali ya hewa ya baharini, salmon huanza safari yao ya kuelekea baharini ambapo hukaa huko kwa muda mrefu sana.

Safari ya samaki hawa inaweza kuwa na umbali wa kuanzia kilomita 1600 mpaka kilomita 4000, kutegemeana na aina yao. Inakadiriwa kuwa wakati wa safari yao, salmon huweza kutembea kwa umbali wa kilomita sita mpaka saba kwa siku.

Baada ya kizazi hiki kuhamia baharini na kukaa kwa muda wa miaka kadhaa, samaki hawa wanapotaka kutaga ili kuendeleza kizazi, hurudi kule walikozaliwa yaani mtoni, katika safari ambayo pia ina maajabu tele.

Na ajabu ni kuwa huwa na uwezo wa kukumbika mahali alipozaliwa kule mtoni kupitia harufu, hata kama ameishi baharini kitambo kirefu sana.

Kwa kuwa maji ya mto yanaelekea baharini na samaki hawa wanarudi mtoni walipozaliwa basi safari yao huwa ngumu kwa sababu inakinzana na maji ya mto, kiasi kwamba wakati mwingine wanapokutana na maporomoko ya maji watalazimika kuruka.

Safari yao hii inataka uvumilivu wa hali ya juu kwani kuna wanyama walao samaki huwa wanawasubiria katika maeneo yenye maporomoko ili wawakamate na kuwala pale wanaporuka. Samaki hawa wanatufunza binadamu kuwa wastahamilivu katika kuliendea jambo lenye changamoto ili kufikia mafanikio.

Mamb usiyoyajua kuhusu samaki salmon

  • Samaki salmon huweza kuishi kuanzia miaka miwili hadi saba, kutegemeana na aina.
  • Samaki salmon hubadilika rangi katika hatua mbalimbali za ukuaji wake. Mfano, anaweza kuzaliwa akiwa na rangi nyeupe na madoa meusi, kisha wakiwa wakubwa kule baharini huwa na rangi ya fedha na bluu kwa mbali na kisha wakati wa kutaga hugeuka huwa wekundu na kichwa cha kijani.
  • Akiwa safarini, samaki salmon hulazimika kuruka katika maeneo ambayo maji yamekauka. Kama hawezi, hulazimika kusubiri mpaka maji yarejee ili aendelee na safari.
  • Katika safari yao ya kurejea mtoni alipozaliwa, salmon hawali kitu chochote. Safari ndefu zaidi ya samaki hawa iliyowahi kurekodiwa ilikuwa ni salmon aina ya chinook ambaye alisafiri umbali wa kilomita 3,845 (sawa na maili 2,389) akielekea mtoni kwa ajili ya kutaga.
  • Salmon ana uwezo wa kuishi mazingira yote ya maji chumvi na maji baridi.
  • Akiwa safarini, mwili wa salmon hupitia mabadiliko ambayo yatamfanya aweze kuishi kwenye maji ya baridi. Hii ni tofauti na samaki wengine ambao ukimtoa katika maji ya baridi na ukamtia maji ya chumvi hufa hapo hapo.
  • Baada ya safari ndefu na ngumu ya kurejea mtoni alipozaliwa, salmon hutaga mayai. Salmon jike wa aina ya chinook huweza kubeba hadi mayai 4,000. Dume la salmon hufanya kazi ya kurutubisha mayai yanayotolewa na jike.
  • Samaki salmon wengi hufa baada ya kutaga mayai kwa sababu ya uchovu. Wachache hupona na kutaga kwa mara kadhaa zaidi katika kipindi cha uhai wao.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close