1. Fahamu Usiyoyajua4. Jamii

Nyoka anayepaa (FLYING SNAKE) Mpole, anayevutia kumtazama

Hakika Allah ni Mkubwa Mwenye utukufu na utakatifu kuliko chochote. Anatukuzwa na kuheshimiwa katika nyoyo za vipenzi na wandani wake. Katika nyoyo za vipenzi na wandani wake hao, kumejaa utukufu wake na utakatifu wake; na hivyo vipenzi vyake hao wananyenyekea na kudhalilisha nafsi zao mbele ya ukubwa wa Allah.

Allah, Mbora wa uumbaji ndiye aliyeumba viumbe vinavyoonekana na visivyoonekana, tunavyovijua na tusivyovijua. Ameumba wanyama wakali na wapole kadhalika ndege na wadudu. Hakika, hakuna aliyewaleta viumbe wote wa baharini na ardhini ila Yeye, Mfalme wa Wafalme

Katika viumbe wake, wapo nyoka. Kuna aina nyingi za nyoka. Wataalamu wa elimu ya viumbe wanakadiria kuna aina za nyoka zaidi ya 3600. Lakini je, umewahi kusikia kuhusu ‘nyoka anayepaa!?; Ungana nami katika safu hii leo nikikuletea mambo mbalimbali za undani wa nyoka huyu. Kwa kiingereza nyoka anayepaa anaitwa ‘flying snake’, lakini kwa lugha ya kitaalamu katika somo la viumbe hai, nyoka huyu anaitwa ‘chrysopelea’ akipatikana katika familia ya nyoka waitwao ‘colubridae.’

Ni kawaida ya nyoka wengi kuwa na sumu ila hutofautiana tu ukali wake. Kiwango cha sumu aliyonayo nyoka huyu wa ajabu anayepaa ni ndogo mno kiasi kwamba inaweza tu kuwadhuru viumbe wadogo tu. Sumu yake haiwezi kumdhuru binadamu, ingawaje kwa upande mwingine hakujawahi kuripotiwa tukio la nyoka huyu kumuuma binadamu.

Nyoka huyu anapatikana kusini kwa Bara la Asia katika nchi za Vietnam, Cambordia, Laos, India, Indonesia, Sri Lanka na kusini mwa China, akitwajwa kuwa na urefu wa futi mbili, akiwa mdogo, na futi nne akiwa mkubwa.

Allah amemjaalia nyoka huyu uwezo wa kupaa na hivyo kuonekana kuwa ni nyoka wa pekee. Kwa sababu ya hali yake hiyo, nyoka huyu anawavutia wengi kumsoma au kumtazama katika picha za mnato na video, hasa pale anapopaa. Nyoka hawa wanaoruka wapo aina tano.

Mbali na kupaa, nyoka huyu pia ni mkweaji miti mzuri. Anapotaka kukwea juu ya mti, kwanza anaanza kujirusha na kupaa. Anapotaka kupaa hujikunja kwa mtindo fulani, ila ajabu ni kwamba, kabla hajapaa au kujirusha huwa anapima kwanza kwa macho sehemu ya kutua. Baada ya kupima, atajirusha angani mpaka pale alipopapimana, mara nyingi hutua katika mti.

Wakati mwingine, samaki huyu anapopaa hujikunya na hujiweka katika umbile linalofanana na herufi J. Pia arukapo juu hujitanua sehemu ya mbavu, halafu chini anakuwa bapa. Pia, nyoka huyu ana kasi kama ya ndege. Licha ya kwamba hana miguu wala mbawa, nyoka huyu anapaa hewani vizuri na kwa urahisi.

Wataalamu wanasema, nyoka huyu anaweza kupaa mpaka mita 100, jambo ambalo hata wataalamu wa Fizikia limewashangaza. Moja ya idara za ulinzi za Marekani, inasemekana bado wanafanya utafiti kujua nyoka huyu anawezaje kuruka kwa kiwango kile! Ila sisi tunatakiwa kusema, Mungu Mwenyewe ndiye anajua zaidi.

Utafiti unaonesha kuwa nyoka wakiwa wadogo wana uwezo mzuri wa kupaa kuliko wakubwa. Mtaalamu mmoja aitwaye Jake Socha amesema, nyoka huyu akipaa hubadilisha hadi umbo lake ili apate uwezo fulani wa kupaa.

Mambo matano usiyoyafahamu

  • Nyoka huyu anayepaa anawinda chakula muda wa mchana. Chakula chake kikubwa ni mijusi, panya, chura, ndege na popo.
  • Katika aina tano za nyoka wanaopaa, yupo mkubwa wao anaitwa ‘golden tree snake,’ na huitwa hivyo kwa sababu wana rangi ya dhahabu. Hata hivyo, wapo wengine wa aina hiyo wana rangi tofauti.
  • Bado elimu ya tabia zao haijapatikana vya kutosha kwa hiyo ni mnyama ambaye wataalamu bado wanamtafiti.
  • Nyoka hawa wamejaaliwa kuwa na meno, lakini cha ajabu ni kuwa yapo nyuma na sio mbele.
  • Pamoja na ushujaa wake wote huo wa kupaa, huyu ni miongoni mwa nyoka wapole.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close