4. Jamii6. Malezi

Njia za kuwa mama bora

“Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima.” [Qur’an, 17:23].

Aya hii ya Qur’an inaonesha namna Uislamu unavyowapa nafasi ya kipaumbele wazazi. Amri ya kuwatendea wema wazazi wawili, imefuatanishwa na ile ya Tawhid, yaani kumuabudu Yeye Mwenyezi Mungu Mmoja na wa Pekee bila kumshirikisha na chochote.

Hata hivyo, kati ya wazazi wawili, mama ana uzito wa kipekee. Hilo linadhihirika wazi katika Aya nyingine, ambapo Mwenyezi Mungu baada ya kuwataja wazazi wote wawili, akaendelea mbele kwa kumsifu mama kwa kuhimili mtihani mzito wa kubeba mimba.

Allah anasema: “Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia), ‘Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.’”

Katika Hadithi ya Mtume, iliyopokewa na Imam Ahmad na Nasai amesema pepo ipo chini ya nyayo za mama. Katika Hadithi nyingine, mtu mmoja alimuendea Mtume akasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nani katika watu anastahili niwe karibu naye?” Mtume akamjibu: “Mama.” Yule mtu akauliza: “Kisha nani.” Mtume akamjibu: “Mama.” Akauliza tena: “Kisha nani.” Mtume akajibu tena: “Mama.” Ni mara ya nne alipouliza: “Kisha nani,” ndipo Mtume alipomjibu: Baba.”

Nafasi hii kubwa aliyopewa mama haijaja hivihivi bali inatokana na wajibu mkubwa wa kimalezi anaoutekeleza. Ni mama ndiye anayembeba mtoto tumboni kwa miezi takriban tisa. Ni yeye mama pia ndiye anayehangaika kumyonyesha, kumuogesha, kumvesha, kumlisha, kumbeba na kumbembeleza katika hali ya uchanga.

Mara ngapi wanaume tunawaona hawajui hata namna ya kumbeba mtoto mchanga? Hajui amshikeje ndiyo hatimaye atatandaza mikono awekewe mtoto. Kwa wanawake wana uasili fulani katika kazi hiyo. Ni zawadi ya kimaumbile waliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Sisemi kuwa, hakuna kabisa wanaume wanaofanya kazi hizi, bali inajulikana kuwa aghalabu wanawake ndiyo hufanya hivyo, tena kwa ufanisi mkubwa. Zipo kesi za wanaume wanaofanya kazi hizi saa 24, lakini ni wachache mno na ni katika mazingira maalumu ya udharura. Na hata mwanamume akifanya hayo, mengine hatayamudu kwa sababu za kiumaumbile, ikiwemo kunyonyesha.

Umama unaanzia katika malezi ya mimba

Licha ya ukweli kuwa, kiasili, wanawake ni walezi wazuri, hii haifuti ukweli kuwa nao wanapaswa kujiendeleza katika kujifunza zaidi elimu ya malezi, hasa katika ulimwengu wa leo wenye changamoto nyingi zaidi za kimalezi.

Jambo la kwanza na la msingi kabisa katika dhana ya ‘umama’ ni kuelewa kuwa jukumu hili tukufu linaanza pale ujauzito unapotunga na kisha mama akajua kuwa ana ujauzito. Hali ya mama katika hatua hii ya ujauzito ina athari ya moja kwa moja kwa hatua za mbele za makuzi ya mtoto.

Ijulikane kuwa, mtoto anaumbika tumboni kwa miezi yote tisa kutokana na vitu anavyopokea (ikiwemo lishe) kutoka kwa mama yake, na si vinginvyo. Mama ndiyo daraja pekee la ustawi wa mtoto. Mama akistawi, mtoto naye atastawi; akinyondea au kuumwa, mtoto naye atapata shida. Kwa msingi nilioutaja hapo juu, mama anapaswa ajitahidi achunge ustawi wake kiujumla kiafya, kijamii, kiakili, kisaikolojia, kiroho nk.

Utafiti mmoja uliofanywa katika chou cha Cambridge huko Uingereza na kuchapishwa mwaka jana unaonesha kuwa, mtazamo (attitude) wa mama juu ya ujauzito inaweza kuathiri maendeleo ya mtoto, kwa namna moja au nyingine. Matokeo haya yanazidi kuonesha umuhimu wa kipindi nyeti cha ujauzito katika maendeleo ya mtoto.

Ushauri kwa mama kipindi cha ujauzito

  • Jambo la kwanza na la msingi kwa mama baada ya kujijua kuwa yu mjamzito, ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuchagua kuwa miononi mwa aliowaruzuku zawadi hii kubwa. Wangapi wanahangaika kutafuta mtoto, wakimuomba Mwenyezi Mungu kila uchao lakini hawapati? Bila shaka ni wengi. Hivyo, shukuru kwa zawadi hii.
  • Pili, hebu fanya siri kwa walau miezi mitatu ya mwanzo. Usikaribishe husuda kwa kutangaza kwani hata Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema katika Hadithi: “ Ficheni (neema) ili mfanikiwe kwani kila aliyebarikiwa huhusudiwa.”[Tabaraani na Abu Nu’aym]. Inasikitisha kuona baadhi ya watu hupeleka habari hizi hadi kwenye mitandao ya kijamii! Ataweka hadi cheti kinachosema yu mjamzito ili walimwengu wote waone! Jambo la tatu muhimu ni kumuombea dua mtoto. Katika dua tatu ambazo Mtume alizitaja katika Hadithi iliyopokewa na Imam Timidhiy kuwa hazikataliwi ipo ya mzazi kwa mwanawe. Nyingine ni ya msafiri na aliyedhulumiwa. Hivyo, mama muombee dua mtoto anayekua katika tumbo lako. Muombee afya, omba salama yenu katika ujio wake. Pia muombee awe kijana mwema na dua nyingine kadhaa wa kadhaa.

Moja kati ya dua ambazo mama anaweza kuomba mara kwa mara ni ile iliyooombwa na Nabii Zakaria, inayopatikana katika Qur’an [3:38], alipomuomba Mola wake: “Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi.”

Show More

Related Articles

Back to top button
Close