2. Ncha ya Kalamu

Viongozi wa dini fanyieni kazi maoni ya Mzee Mwinyi

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema Tanzania bado ina deni la kupambana na rushwa, na akashauri njia mojawapo ya kupambana na rushwa iwe ni kutoa elimu kuhusu rushwa na madhara yake katika shule na vyuo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa kupambana na rushwa kwa kuwatumia vijana wa skauti nchini, Rais Mstaafu Mwinyi mkakati huo wa kutoa elimu kwa vijaa unaweza kusaidia kumaliza rushwa, iwapo jamii itatoa ushirikiano.

“Kuna aina nyingi za rushwa mfano wizi, ufisadi na hongo. Hivyo, ni vema kupambana nazo,” alisema Mzee Mwinyi na kuongeza kuwa mkakati wa kutoa elimu utasaidia kubadilisha mitazamo ya watu wangali wadogo.

Mzee Mwinyi, kwa umri wake na uzoefu wa uongozi bila shaka ameona rushwa inavyoathiri maendeleo ya nchi na kudidimiza haki na ustawi wa raia, hususan wanyonge na ndio maana alitoa wito huo.

Wote tunajua umuhimu wa umuhimu wa viongozi wa dini. Basi, kwa kuwa rushwa inafanyika katika jamii ambazo Waumini wa dini wanaishi ni vema viongozi wa dini wakatumia nafasi zao kikamilifu kukemea rushwa.

Kama wadau muhimu katika jamii, viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa. Tunasema hivyo kwa sababu viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa kwa Waumini wao na jamii inayowazunguka, hivyo wito wao kwa jamii katika kujiepusha na rushwa una nafasi kubwa ya kuleta matokeo chanya.

Sisi Gazeti Imaan, tunawapongeza viongozi wote wa dini na serikali wanaopaza sauti zao kukemea rushwa. Ni imani yetu juhudi zao hizo zitaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu.

Uislamu unakemea rushwa

Na hili suaa la kula/ kupokea rushwa limeshazungumzwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an [2:188], pale aliposema:

“Wala msiliane mali zenu kwa batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua.”

Na katika hadithi iliyopokewa na Thawbaan (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Allah amemlaani mtoa rushwa, mlaji rushwa na tarishi baina yao.” [Ahmad na Haakim].

Hivyo basi, jamii isikae pembeni na kuliona suala la kupamabana na rushwa ni la serikali na viongozi wa dini tu kwani wanaoathirika na rushwa ni sisi wenyewe.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close