2. Ncha ya Kalamu

Uislamu na adhabu ya viboko shuleni

Wiki iliyopita mjadala juu ya matumizi ya adhabu ya kuchapa wanafunzi viboko shuleni ulitawala mitandao ya kijamii. Mjadala ambao si mpya, umechochewa na kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bwana chalamila kuwachapa viboko wanafunzi wa shule ya Sekondari Kiwanja iliyoko mkoani Mbeya waliotuhumiwa kuchoma moto mabweni ya shule hiyo.Je Uislamu unasema nini kuhusu adhabu ya viboko kwa ujumla na husuusan shuleni au madrasa? ….Sasa endelea.

Adhabu ya viboko katika vitabu vya dini

Kutoa adhabu ni njia mojawapo ya kupambana na maadili mabaya katika jamii na ni jambo kongwe la enzi na enzi na lipo katika vitabu vyote vya dini kuanzia Taurati, Zaburi, Injili na hatimaye Qur’an Takatifu.

Katika Biblia, ambayo chimbuko lake ni mafundisho ya Injili ya Nabii Isa (amani ya Allah imshukie), tunakuta andiko hili: “Usimnyime mtoto wako mapigo maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo na kuokoa nafsi yake na kuzimu.” [Mithali: 13 na 14].

Katika Uislamu, kutoa adhabu ya viboko kwa ujumla imetajwa kama njia ya kuwarekebisha watenda maovu kama vile uzinifu. Allah anasema: “Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamme wachapeni mijeledi mia moja kila mmoja wao…” [Qur’an 24: 2].

Lakini kwa watoto, adhabu ya kuchapwa bakora imetajwa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) katika Hadithi kutoka kwa Abdillahi ibn Amr ibn Al’aas (Allah amridhie), kwamba Mtume wa Allah amesema: “Waamrisheni watoto wenu kwa ajili ya sala tano wakifikisha umri wa miaka saba na wachapeni bakora kwa ajili ya kuacha sala wakifikisha miaka kumi.” [Ahmad, Abuu Dawud].

Kwa hiyo suala la watoto kuchapwa bakora kwa mujibu wa mafundisho ya dini halina mjadala. Kinachobaki ni kiasi cha hizo bakora ambacho katika Uislamu kimeelezwa kuwa ni kipigo kisichoacha alama mwilini.

Jamii inapolalamikia adhabu ya viboko shuleni

Katika miaka ya hivi karibuni, tangu kuingia kwa kile kiitwacho watetezi wa haki za binadamu na haki za watoto, kumezuka mijadala mikali kupinga matumizi ya adhabu ya viboko shuleni. Kwa mujibu wa sheria za adhabu shuleni chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, viboko ni miongoni mwa aina za adhabu zitolewazo kwa wanafunzi kwa makosa mbali mbali.

Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 umetoa utaratibu mzima wa kutoa dhabu ya viboko kwa mwanafunzi. Pamoja na mambo mengine, waraka huo umeeleza kuwa kiwango cha juu cha viboko anavyoweza kuchapwa mwanafunzi mmoja kwa wakati mmoja ni viboko vinne tu.

Hali kadhalika, waraka huo umeeleza maeneo ya mwili ambayo mwanafunzi anaweza kuchapwa viboko ambayo ni makalio (wavulana) na viganja vya mikono kwa (wasichana).

Utovu wa nidhamu ni jambo baya kuliko uchungu aupatao mwanafunzi anapochapwa viboko kwa kosa alilolitenda kama lile la wanafunzi kuchoma moto mabweni ya shule yao. Jambo la kusikitisha, jamii yetu imeathirika na umagharibi kiasi kwamba kila kinacholetwa kutoka huko tunakivamia na kukikumbatia utadhani kimetoka kwa Mola Muumba wa mbingu na ardhi.

Kampeni ya kupinga uchapaji viboko mashuleni na kwa ujumla utoaji adhabu kwa wanafunzi ilianzia Marekani na nchi za Ulaya na hatimaye kuenea katika nchi zetu.

Enzi tukiwa watoto wadogo, katika jamii nyingi za kiafrika mtoto akitenda kosa aliadhibiwa kwa kuchapwa viboko tena na mtu mzima yeyote yule kijijini au mtaani na wazazi wake walimpongeza aliyemwadhibu mtoto wao.

Jamii ilitambua jukumu la kukemea maovu na kuamrisha mema kwa watoto ni jukumu la kila mmoja katika jamii. Na ndiyo maana kiwango cha uhalifu na uharibifu wa maadili kwa ujumla kilikuwa kidogo sana. Kadiri jamii inavyokwepa kutoa adhabu kwa watoto na hususan wanafunzi shuleni ndivyo inavyoruhusu uharibifu wa maadili na kurithisha zao la tabia ya kuvumilia uharibifu wa maadili.

Sababu za kupinga adhabu ya viboko shuleni

Sababu zitolewazo kupinga adhabu ya viboko isiendelee kutolewa shuleni ni kwamba adhabu hiyo inamdhalilisha mtoto na kumuathiri kisaikolojia na pia si adhabu yenye faida na pamoja na kuwepo kwake bado watoto wanatenda makosa tu.

Sababu hizi hazina mashiko kwa sababu kama ni hoja ya kumwathiri mtoto kisaikolojia athari hiyo imeanza kwa watoto wa zama hizi tu? Adhabu ya viboko kwa watoto wakitenda kosa stahiki kuadhibiwa kwa viboko ilikuweko tangu zama za Manabii. Watoto walichapwa viboko na hakuna aliyeathirika kisaikolojia. Nadhani ni sisi ndiyo tunaowaathiri watoto wetu kisaikolojia kwa kuwajenga waamini kwamba kuadhibiwa kwa viboko wanaonewa.

Suala la kudhalilishwa mbele ya wanafunzi wenzake pia si hoja kwa sabbau lengo la adhabu si tu kumkanya mtoto asirudie kosa husika bali pia ni kuwakanya watoto wengine wasiige mfano huo mbaya.

Wanafunzi wakorofi wanapoadhibiwa mbele ya darasa au mbele ya wanafunzi wote, ndiyo lengo la adhabu linapotimia kwa kuwa kizuizi (deterrence) kwa wengine.

Ama hoja kwamba pamoja na uchapwaji viboko bado watoto wanaendelea kutenda makosa nayo ni hoja mfu kwa sababu mbona madereva wanatenda makosa kila siku barabarani na hata kusababisha ajali lakini jamii haijaacha kutumia barabara na vyombo vya usafiri?

Itaendelea…

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close