2. Ncha ya Kalamu

Tuipe njia haki zake

Kutoka kwa Abu Huraira (Allah amridhie) amesimulia kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu mmoja alipita njiani akakuta tawi la mti katikati ya njia akasema: ‘Wallahi nitaliondoa tawi hili lisiwaudhi Waislamu. Mtu huyo akaingizwa peponi.” [Bukhari na Muslim].

Riwaya nyingine ya Bukhari na Muslim inaeleza kuwa, mtu mmoja alipokuwa akitembea njiani, alikuta tawi la mti wenye miba njiani, akaliweka nyuma. Allah akamridhia na akamsamehe (madhambi yake).

Mafunzo ya tukio hili Kuondoa maudhi njiani Miongoni mwa mambo ambayo watu wengi wameyadharau ni kuondosha maudhi au madhara kwa watu wanaotembea barabarani. Badala yake watu wamekuwa mstari wa mbele kusababisha maudhi na bughudha kwa njia mbalimbali.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amebainisha kuwa kuondosha maudhi njiani ni sehemu ya imani.”Imani ina zaidi ya matawi sabini, tawi la juu kabisa ni neno ‘Laailaha illallah,’ na tawi la chini kabisa ni kuondosha maudhi njiani.” [Muslim].

Udogo wa wema haulingani na malipo yake

Wakati mwingine hutokea mtu akaacha kufanya jambo la kheri kwa kuona kuwa ni dogo kumbe ni jambo lenye malipo makubwa mbele ya Allah. Mfano wa amali zenye malipo makubwa mbele ya Allah ni kuondosha maudhi njiani. Zimepokewa Hadith mbalimbali kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) zinazoonesha fadhila na malipo ayapatayo mtu aliyeondosha maudhi njiani.

Miongoni mwa hadith hizo ni ile iliyopokewa na Ibn Hibbaan kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) ambaye amesema: “Mtu mmoja aliondosha tawi la mti katika njia waliyokuwa wanapita watu akasamehewa madhambi yake yaliyotangulia na yaliyofuata baadae.”

Na katika riwaya nyingine Mtume amesema: “Mtu mmoja alikuwa anatembea njiani akakuta tawi la mti, akaliondoa. Allah akamridhia na akamsamehe.” [Bukhari].

Na imethibiti kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) akisema kwamba alimuona mtu akigeukageuka peponi kutokana na mti alioukata njiani. Mti huo ulikuwa unawaudhi watu, [Muslim].

Kuepuka kukaa njiani

Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) aliwaambia Maswahaba zake (na sisi sote): “Tahadharini kukaa njiani.” Maswahaba wakamwambia: “Ewe Mjumbe wa Allah! Hatuna budi (kukaa njiani) kwani hayo ndio maeneo yetu, tunakaa na kuzungumza ndani yake.” Mtume akawaambia: “Ikiwa mtakataa basi ipeni njia haki yake.” Wakauliza: “Ni ipi haki ya njia?” Mtume akasema: “Ni kuinamisha macho (kutotazama yaliyoharamishwa), kuondoa udhia, kujibu salamu, kuamrisha mema na kukataza mabaya.” [Bukhari na Muslim].

Hivyo, mwenye kupita ama kukaa njiani anawajibika kutekeleza mambo yote yaliyoorodheshwa katika hadith tuliyoitaja hapo juu.

Aina za maudhi

Kuna aina nyingi za maudhi ambayo tunapaswa kuyazuia au kuwaondoshea Waislamu. Mengi ya maudhi hayo ni yale yanayohusiana na maneno, yaani matusi na kejeli. Yote haya yanapaswa kuondoshwa na kuzuiwa ili yasiwadhuru Waislamu kwani mengine yanaharibu imani zao na kuporomosha ibada zao. Ubaya unaofanywa na baadhi ya watu

Baadhi ya watu wanakiuka taratibu na adabu za njia, utawaona baadhi yao hawana ari ya kuondosha maudhi njiani. Si hivyo tu, bali watu hao wanahusika kwa kiasi kikubwa kutupa takataka na masalia ya vyakula, kujisaidia hovyo pembeni ya barabara na kupora mali za watu.

Mbali na hao, pia kuna baadhi ya watu wasio waaminifu ambao huharibu vituo vya kupumzikia wasafiri, kukata miti iliyopo pembezoni mwa njia kwa maslahi yao binafsi, kuwatusi watu na kutazama wanawake wapitao njia kwa matamanio.

Kama ambavyo mtu hupata malipo (thawabu) kwa kufanya mambo mema, vilevile mtu hupata thawabu kwa kuzuia shari na maudhi kwa watu. Imepokewa kutoka kwa Abu Dharri (Allah amridhie) kwamba siku moja alimuuliza Mtume (rehema za Allah na amani imshukie):

“Unaonaje ikiwa nitakuwa nimedhoofika, nikashindwa kufanya baadhi ya matendo?” Mtume akamwambia: “Utazuia shari zako kwa watu, na ukifanya hivyo utakuwa umeitolea sadaka nafsi yako.” [Bukhari na Muslim].

Kutekeleza ibada ya sala, funga na nyinginezo bila kujizuia na uadui na maudhi kwa watu, ni dosari kubwa katika mfumo wa ibada ya Muislamu. Mmoja wa Maswahaba alipata kumwambia Mtume:

“Ewe Mjumbe wa Allah! Hakika fulani anatajwa kwa wingi wa sala zake na funga zake na utoaji wake wa sadaka isipokuwa huwa anamuudhi jirani yake kwa ulimi wake.” Mtume akasema: “Hakika yeye atakuwa mtu wa motoni.” [Ahmad].

Hadith hii inaonesha wazi kuwa, suala la kuzuia maudhi na uadui kwa watu ni katika ibada ambazo watu wengi wamegafilika nazo. Watu watambue kuwa, pamoja na kutekeleza mambo mengi ya kheri, kuna sehemu ya pili ya ibada ambayo ni kujizuia na yale yote yenye kupelekea maudhi katika maisha ya watu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close