2. Ncha ya Kalamu

Tudhamirie kuboresha hali za walimu wa dini shuleni

Ni ajabu iliyoje kuona kwamba hata walimu wanaojitolea kufundisha masomo ya dini shuleni hatuwajali. Hili ni jambo la kusikitisha kwa sababu, walimu wa dini ni nguzo muhimu katika mchakato mzima wa kuwafunza watoto tabia na mwenendo anaouridhia Mwenyezi Mungu.

Katika ngazi zote anazopitia mwanafunzi, kuanzia hatua ya makuzi ya kimwili, kiroho na kiakili, walimu wa dini wana nafasi ye kipekee. Ni majununi pekee ndiye anayeweza kupuuza nafasi hii waliyonayo walimu wa dini.

Kwa bahati, sisi Waislamu, walau katika maeneo ya mijini tu, tunao wasomi wengi wa dini ambao kama tutawatumia vema wanaweza kujenga kizazi bora chenye hofu ya Mungu.

Lakini ajabu ni kwamba, wengi wetu tumeshindwa kabisa kuwajali na kuwathamini walimu wa dini, hususan katika maeneo ya vijijini. Matokeo yake kila ikifika siku ya kwenda kufundisha masomo ya dini wanashindwa kufika shuleni kutokana na kukosa huduma ya usafiri na mahitaji mengine ya msingi.

Umuhimu wa walimu wa dini

Umuhimu wa walimu wa dini unadhihiri zaidi pale yanapojitokeza matatizo makubwa yanayoisumbua serikali kama vile ufisadi, matumizi ya dawa za kulevya, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa mali za umma, na mengineyo. Serikali inatumia nguvu kubwa sana kupambana na uovu huu, lakini walimu wa dini wanaweza kufanikisha hili kirahisi kwa kuwajengea Waumini hofu ya Mwenyezi Mungu.

Bahati mbaya sana, watendaji na watunga sera hawayapi kipaumbele masomo ya dini shuleni. Katika shule nyingi, hasa za serikali, masomo ya dini yamekuwa ni kama hiyari kwa wanafunzi na hayafundishwi kwa kutiliwa mkazo kama masomo mengine.

Hali za walimu wa dini nchini

Ni dhahiri kuwa, elimu ya dini katika miaka ya kabla ya uhuru wa Tanganyika ilikuwa na ubora wa aina yake ambapo vijana wengi walipata elimu ya dini na ile ya mazingira, ingawa hata sasa baadhi ya shule za Kiislamu hufanya hivyo kwa kusomesha watoto elimu ya dini na mazingira kwa wakati mmoja.

Kwa sababu hiyo, kuna haja ya kurudi nyuma na kuangalia upya mifumo ya uendeshaji wa shule zetu kwani kinachoonekana tatizo si uwezo wa walimu kushindwa kumudu kufundisha bali tatizo ni wazazi na walezi kushindwa kuthamini elimu ya dini kutokana na kutoipa kipaumbele.

Kwa hili, Waislamu tusitafute mchawi aliyeturoga. Ni makosa yetu. Kama tunashindwa kuwathamini walimu wa dini, ni kipi tunachotegemea katika suala zima la malezi na maadili ya dini kwa vijana wetu?

Kushindwa kuwathamini walimu wa dini ni sawa na kuitupa dini kwani walimu ndio warithi wa Mitume, hivyo tunapaswa kuwangalia kwa ukaribu. Walimu wanapaswa kuwa watu wa tabaka la juu.

Mwenyezi Mungu anawasifu watu wenye elimu iliyoambatana na Imani na itikadi sahihi ya dini pale aliposema ndani ya Qur’an:

“Mwenyezi Mungu atawainua walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu.” [Qur’ an, 58:11].

Enyi Waislamu, tambueni kuwa elimu ni zawadi na urithi bora wa watoto. Elimu ndio kitu pekee kinachoweza kumjengea mtoto wako moyo wa imani na uchamungu, kujua utu sambamba na kumtukuza Mola wake mlezi, jambo ambalo kama mtoto akishikamana nalo atakuwa mtu mwema katika jamii.

Nani awafadhili walimu wa dini?

Suala la kufadhili mishahara ya walimu wa dini linabaki kwa Waislamu wenyewe na sio tajiri mmoja. Hili linathibitika tukirejea historia ya Uislamu ambapo Maswahaba wa Mtume (Allah awe radhi nao), walijitolea kwa hali na mali katika kuitumikia dini na hatimaye kutufikia sisi hii leo.

Kimsingi, walimu wa dini ya Kiislamu hapa nchini wamesahauliwa kabisa na wameachwa katika hali ya upweke kiasi cha kuona ugumu wa kuendelea na kazi hiyo. Na hali ikiendelea kuwa hivyo, walimu watashindwa kabisa kwenda shuleni kufundisha.

Kwa jinsi hali ilivyo, ni vigumu kumaliza changamoto za walimu wa dini kwa kutegemea nguvu ya kundi moja la watu ambao ni Masheikh na wazazi pekee, bali hili ni tatizo linalopaswa kumgusa kihisia kila Muislamu.

Ni kweli kwamba elimu ya dini ina umuhimu na mchango mkubwa katika kuandaa wanaharakiti wazuri watakaouendeleza Uislamu. Hivyo, kama tutawapuuza walimu wa dini tutakuwa tunaandaa mazingira ya kushindwa kuzalisha kizazi bora cha Kiislamu kwa siku za usoni.

Leo hii, jamii kwa kiasi, fulani huwachukulia walimu wa dini kama watu wa daraja la chini sana kimaisha. Wengi wanawaona walimu hawa kama watu madhalili wanaopaswa kuwafundisha vijana masuala ya dini lakini hawapaswi kuthaminiwa muda wao wanaoutumia.

Ni aibu kuwaona walimu wa dini pamoja na familia zao wakiishi kiudhalili, wakati kuna matajiri wengi wa Kiislamu ambao hutumia neema ya mali waliyopewa na Mwenyezi Mungu katika mambo yasiyo na manufaa na dini huku wengine wakiishia kufadhili mashindano ya muziki, ulimbwende (umiss), soka na mambo mengine ya kishetani.

Wakati watu hawa wanatumia neema ya mali kusaidia mambo yaliyoharamishwa, inaonekana hakuna wa kuthubutu ama kudiriki kuwaonya wasifanye hivyo.

Ili kuondokana na changamoto za walimu wa dini, ni lazima tuwawezeshe kiuchumi ili wafanya shughuli zao kwa ufanisi huku wakitekeleza majukumu yao ya kuwapatia elimu ya dini watoto na vijana wetu. Kama tunataka maendeleo ya kweli hatuna budi kuboresha hali ya walimu kwani wao ndio chachu ya kuwawezesha watoto kuwa na tabia njema.

Hivyo ni jukumu letu kuwaangalia walimu wa dini kwa jicho la tatu kwani hata wao wanaweza kuwa na shughuli mbadala za kujitafutia riziki isipokuwa wanaziacha na kufanya kazi ya kufundisha wakitafuta radhi za Muumba wao.

Kilicho muhimu ni sisi kujenga ustawi mzuri kwa kuboresha mazingira ya kazi na maisha yao kwa ujumla. Walimu wa dini ni sehemu ya maisha yetu, hivyo ni lazima tuwajali, tuwapende na kuwathamini.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close