2. Ncha ya Kalamu

Tuache ubinafsi ili kudhibiti migogoro misikitini

Kukithiri kwa migogoro ya uongozi ndani ya misikiti ni jambo mashuhuri kwa siku za hivi karibuni. Uchu wa madaraka, elimu duni ya dini na uwezo mdogo wa kiutawala kwa baadhi ya viongozi ni baadhi ya mambo yanayochangia kuwapo kwa migogoro hii ndani ya misikiti.

Swali ni je, kwa nini migogoro hii hujitokeza misikitini? Kwa nini Waislamu wanagombea madaraka katika nyumba za ibada?

Hapa pana tatizo kubwa kinadharia maana tunavyofahamu Uislamu ni kujisalimisha kwa Allah na kufuata amri zake sambamba na kuacha makatazo yake katika kila nyanja ya maisha.

Kwa msingi huo, mtu aliyejisalimisha kwa Allah, daima atakuwa mchamungu, mwema, mpole, mtenda haki, muadilifu, mvumilivu na mwenye huruma. Hata hivyo, mwanadamu ni kiumbe dhaifu, anaweza kupotoka aidha kwa kufanya ugomvi, hujuma, au jambo jingine lolote. Lakini mchamungu anapogundua kuwa amekosea hujilaumu nafsini na
kwa haraka hutubia na kumuomba msamaha Mola wake ili abaki kwenye njia ya sawa.

Huu ni ushahidi kuwa, palipo na dini na watu wakizitendea haki dhamana walizokabidhiwa, hutawala amani, maelewano, na kuheshimiana. Kuwepo kwa migogoro ya uongozi au kugombea madaraka ni dalili ya kukosekana kwa dini. Dini ni kama mwanga, na migogoro ni kama giza. Penye mwanga hapana giza. Ndio maana tunasema, penye dini hapana migogoro wala ugomvi.

Katika hili, yapo mengi ya kumuiga Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa kuwa yeye ndio Mwalimu wa dini hii. Mtume alitanguliza busara, hekima na maneno mazuri na laini katika kutatua migogoro baina ya Maswahaba zake (Allah awaridhie wote).

Kinachoonekana hivi sasa ni viongozi kujihusisha zaidi na kutibu vidonda na vipele na sio chanzo halisi cha ugonjwa. Kama tunataka kuondokana na migogoro ya uongozi misikitini ni lazima tuandae mafunzo ya uongozi wa dini juu ya nadharia, dhana, imani na kanuni za msingi zinazochangia kuwaunganisha Waislamu badala ya kuwagawa.

Endapo viongozi wa misikiti wataendekeza tabia za kupenda kujinufaisha na kufanya maamuzi ya kidikteta bila ya kuwashirikisha Waumini, basi migogoro ya uongozi ndani ya misikiti haitokwisha na imani ya Waumini kwa viongozi hao itapungua kwa kiasi kikubwa kama si kutoweka kabisa.

Tumalize kwa kuwakumbusha viongozi katika misikiti kuwa uongozi ni dhamana. Imepokewa na Ibn Umar (Allah amridhie) kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Nyote ni wachunga, na kila mchunga ataulizwa kuhusu, alichokichunga, Imamu ni mchunga, naye ataulizwa kuhusu alichokichunga, mwanaume ni mchunga wa familia yake, na ataulizwa kuhusu alichokichunga, na mwanamke ni mchunga kwenye nyumba ya mumewe, na ataulizwa kuhusu alichokichunga, na mtumishi ni mchunga wa mali ya bwana wake, naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake…”[Bukhari]

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close