2. Ncha ya Kalamu

Tatizo la wizi wa mitihani lipatiwe ufumbuzi wa kudumu

Jumatatu ya wiki iliyopita, wanafunzi wa kidato cha nne nchini Kenya na Tanzania walianza kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne ikiwa ni hatua ya kutamatisha ngazi ya pili ya safari yao ya elimu.

Watahiniwa wengine ni wale ambao hawakufanya vizuri mtihani wa kidato cha nne wa miaka ya nyuma na watu wazima wanaotaka kujiendeleza ambao wanafanya mtihani huo kama watahiniwa wa kujitegemea yaani ‘private candidates’.

Kama ilivyo desturi, kila msimu wa mitihani unapowadia Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) hutoa muongozo kwa watahiniwa na walimu wanaosimamia mitihani ya taifa kutojiingiza katika tamaa na udanganyifu ambao utapelekea kuharibu taswira nzima ya mtihani, kama ilivyojitokeza katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana.

Jambo la kutia moyo ni kuwa baada ya tukio hilo, wizara iliwawajibisha baadhi ya maofisa elimu na walimu kwa uvujishaji wa mtihani. Hata hivyo inasikitisha kuona kuwa wadau wakuu wa elimu ambao ni walimu, wazazi na wanafunzi ndiyo wahusika wakuu wa tabia hii.

Licha ya Serikali kuonya na kukemea tabia hii mara kwa mara, tatizo la udanganyifu kwenye mitihani kwa miaka mingi limekuwa likishika hatamu.

Ni nini chanzo cha udanganyifu huu? Kuna mambo kadhaa yaliyokwishabainishwa huko nyuma ambayo yanachangia tabia ya udanganyifu au wizi wa mitihani kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari na hata vyuoni.

Jambo la kwanza ni msisitizo wa kuufanya mtihani kuwa ndiyo kigezo pekee cha kuamua hatima ya mwanafunzi kuendelea na masomo ya juu, kupata kazi au kubaki nyumbani. Hii ni moja ya sababu kubwa zinazofanya wizi au ulaghai kwenye mitihani uendelee.

Jambo jingine ni kuwa elimu yetu haina mkazo kwenye kufundisha maarifa. Kinachotiliwa mkazo zaidi ni kuwafundisha watoto kukariri masomo na kufaulu mtihani pekee.

Hali hii imefanya wazazi na walimu kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mtihani kwa njia yoyote ile hata kama hawajui kusoma na kuandika. Kungekuwa na vigezo vingine vya kuwapima wanafunzi wetu uwezo wao, vitendo hivi vingepungua kama si kuisha kabisa.

Wakati tunatafakari kuhusu wale wanaojihusisha na wizi wa mitihani, ni vema pia tujiulize, ni lini mtihani ndiyo utakuwa kigezo pekee cha kuwapima wanafunzi?

Pia jambo jingine linalosababisha kudumu kwa tatizo hili ni maagizo na amri kutoka kwa viongozi wa kisiasa wanaosisitiza walimu wakuu kuhakikisha watoto wanafaulu ili mkoa au wilaya isishike nafasi za mwisho kimkoa au kiwilaya. Hili nalo ni tatizo linalochangia wizi wa mitihani.

Aidha, baadhi ya maofisa elimu pia wamekuwa na tabia ya kuwaamuru walimu wakuu wajieleze kwa nini watoto hawajafaulu mitihani. Kutokana na shinikizo hilo, walimu wakuu wamekuwa na woga wa kushushwa vyeo endapo shule zao zitafanya vibaya kwenye mitihani.

Hali hiyo inachochea walimu wakuu kutumia njia zozote ikiwamo udanganyifu ili kulinda nafasi zao. Athari za wanafunzi kufaulu kwa njia za ujanjaujanja ni mbaya kwa taifa kwani inapelekea kuzalishwa wasomi wasiojiamini na wasiokuwa na maarifa wala ujuzi ambao ungeweza kuwasaidia katika maisha yao na taifa kwa jumla.

Hivyo, Serikali na vyombo husika vinapaswa kulipa suala hili kipaumbele, kwa kulikemea na kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayehusika katika udanganyifu wa mitihani kwa njia yoyote ile.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close