2. Ncha ya Kalamu

SHAIRI: NAWASHUKURU WAZAZI

Nawashukuru wazazi, wawili mlonizaa,
Pamoja nanyi walezi, wote mlionilea,
Kunipa mema malezi, na kunionyesha njia,
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Mmefanya kubwa kazi, hadi leo kufikia,
Kwa tabu zile na hizi, ili nipate kukua,
Awalipe Mwenyezi, kheri na baraka pia,
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Kwa yenu bora malezi, mimi ninafurahia,
Mmenionyesha wazi, yale yote yanofaa,
Na pia bora mavazi, nivae kilo sawia,
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Kwa yenu yote mapenzi, mengi mlivumilia,
Hamkufanya ajizi, elimu kunipatia,
Ingawa ni ngumu kazi, hili hamkuhofia,
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Ya Allahu ya Azizi, unifungulie njia,
Nienzi wangu wazazi, nisije kuwakosea,
Waniridhie wazazi, kila nitowatendea,
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Hakuna kama wazazi, sheria inatwambia.
Umuabudu Mwenyezi, wazazi wema fanyia.
Atanadhibu Azizi, wazazi mkichukia.
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Baba na Mama mzazi, nawaombea Jalia.
Awape mema makazi, ya akhera na dunia.
Iondoke pingamizi, Peponi mweze ingia.
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Ewe Allahu Mwenyezi, Wewe umetuambia.
Tuwaombee wazazi, Dua utaipokea.
Rehemu wangu wazazi, kama walivyonilea.
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Machozi yanichirizi, kila nikifikiria.
Nilipo tambua wazi, kama niliwakosea.
Anisamehe Mwenyezi, na mnisamehe pia.
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Nasitisha beti hizi, mbele sitoendelea,
Ninamuomba mwenyezi, takabali langu dua, Awarehemu wazazi, na hata walezi pia, Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia.

Mtunzi: Arafa Muhsin.
Kuzaliwa: Mafia Kisiwani.
Makazi: Kigamboni Dar es Salaam.
Imesomwa: Radio Imaan

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close