2. Ncha ya Kalamu

Nani aliyeuza ardhi ya Wapalestina?

SEHEMU YA 21 Wiki iliyopita tuliona jinsi mataifa ya Kiarabu yalivyogawanyika kuhusu Palestina na kuibuka kwa uongozi mpya wa Wapalestina chini ya Mussa Al-Alami badala ya Mufti Amin. Tuliona pia jinsi Marekani ilivyoanza kuibuka mbabe wa dunia ikiipikuwa Uingereza Sasa endelea…

Kumalizika kwa Vita na Hatma ya Palestina

Kasi ya matukio ya mwaka 1945 kufuatiwa kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, ulioundwa mwaka mmoja baada ya Umoja wa nchi za Kiarabu (Arab League), ilionesha kwamba mataifa ya Kiarabu na Wapalestina walikuwa wana matumaini mapya. Mataifa sita ya Kiarabu yalijiunga na kuwa wanachama wa mwanzo wa Umoja wa Mataifa na kutegemea kwamba watakuwa na kauli katika uwanja wa diplomasia ya kimataifa. Mkataba wa nchi za Kiarabu wa mwezi Machi mwaka 1945 uliweka msingi wa ushirikiano kati ya nchi za Kiarabu katika medani ya kimataifa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani ilitoweka kama dola mbabe wa dunia. Mwaka 1945 ulikuwa ni mwaka wa mataifa kujipanga katika nidhamu mpya ya dunia. Uingereza ikihofia ushindani wa Urusi na dola yake ya Kisovieti (USSR), ilihitaji sana ushirikiano wa mataifa ya Kiarabu. Ingawa mataifa ya Kiarabu yalijiamini, lakini mazingira katika uwanja wa kimataifa yalikuwa yamebadilika kwa kasi sana. Enzi mpya iliyoitwa enzi ya vita baridi kati ya mataifa ya kibepari ya magharibi na yale ya mashariki ya kisoshalisti ilikuwa imeanza lakini Waarabu hawakuing’amua hali hii na wala hawakujiandaa nayo vya kutosha. Pamoja na matukio yote haya, kimsingi mataifa ya Kiarabu yalikuwa yameshapoteza fursa ya kuikomboa ardhi ya Palestina, ardhi ambayo ilikuwa imeshageuka kuwa uwanja wa mapambano wa kimataifa ambapo mshindo wa mapambano hayo ndiye mtawala wa dunia. Kuingia kwa Marekani katika medani ya kimataifa kulileta nguvu ambayo kwa upande mmoja iliikabili Uingereza lakini kwa upande mwingine ilikuwa mtetezi asiyetetereka wa Uzayuni na azma yao ya kuunda taifa lao katika ardhi ya Wapalestina. Mauaji ya kimbari (Holocaust) ya Wayahudi nchini Ujerumani yalipelekea jumuiya ya kimataifa kuwaonea huruma Wazayuni na wao wakaitumia fursa hiyo kutimiza azma yao ya kuikalia ardhi ya Palestina na kuunda taifa leo. Maelfu kwa maelfu ya Wayahudi walikuwa wakimiminika kuingia Palestina kupitia Uturuki ambayo ilikuwa chini ya Mustafa Kemal Attaturk baada ya kudondoshwa kwa dola ya Kiislamu (The Ottoman Empire). Ingawa mataifa ya Kiarabu yalikuwa yametangaza umoja wao dhidi ya Wazayuni (The Arab League), hayakuweza kuwa na stratejia na malengo ya pamoja na ni jinsi gani wataweza kuikomboa ardhi ya Palestina kutoka mkononi mwa Uingereza na kisha kuizuia isiangukie mikononi mwa Wazayuni. Kwa upande wao, Wazayuni walikuwa wameshajizatiti ndani ya Palestina wakiongeza idadi yao na pia kununua ardhi ya Wapalestina kwa bei yoyote ile pamoja na kuwanyan’ganya Wapalestina wanyonge ardhi yao huku wakijiimarisha kijeshi kwa kuongeza vikosi vya wapiganaji na silaha tayari kwa vita na Waarabu. Hatimaye kurudi kwa Jamil Hussain ndani ya ardhi ya Palestina na kurejesha uongozi wao siyo tu kuliharibu mahusiano na masikilizano yaliyokuwa yamejengwa kati ya kiongozi mwenye msimamo wa wastani uliokubalika na mataifa ya Kiarabu, Mussa Al-Alami, bali pia kuliwafanya Wapalestina wawe wamegawanyika tena kimsimamo. Badiliko hili la uongozi wa Wapalestina halikufikiwa pasina upinzani. Mussa Al-Alami alijaribu kufuatilia mafanikio aliyoyapata katika mkutano wa mataifa ya Kiarabu kule Alexandria nchini Misri kwa kuzuia kurejea kwa Mufti Amin nchini Palestina kutoka uhamishoni nchini Ujerumani. Alijaribu pia kumvutia Jamil AlHussain awe upande wake lakini yeye aliamua kubakia mtiifu kwa Mufti Amin ambaye pia alikuwa mpwa wake kuliko kumuunga mkono Mussa Al-Alami aliyekuwa shemeji yake. Maana yake ni kwamba, Wapalestina walikuwa wamegawanyika pande sita kinzani. Waarabu na Wapalestina: Wamoja au Wapinzani? Katika jambo lililoathiri sana kadhia ya Palestina ni uhusiano kati ya mataifa ya Kiarabu na uongozi wa Wapalestina. Mataifa ya Kiarabu hayakuwa tayari kuacha ushawishi wao juu ya kuzitawala harakati za Wapalestina. Kwa hakika hawakutaka kurudia makosa ya mwaka 1939 ambapo Mufti Amin aliweza kuwa na kauli yenye nguvu na kuikataa kura ya maoni au White Paper iliyopendekeza uwepo wa taifa moja la Palestina lenye Wapalestina na Wayahudi lakini Wayahudi wakiwa raia kama raia wengine. Zile tofauti zilizokuwepo kati ya nchi za Kiarabu iliendelea kuwepo. Kwa hiyo siyo tu Wapelestina wenyewe walikuwa wamegawanyika, lakini hata watetezi wao yaani mataifa ya Kiarabu walikuwa pia wamegawanyika kimtazamo juu ya Palestina. Iraq na TransJordan (Jordan) zilikuwa na malengo ya kuzimeza nchi nyingine jirani za Kiarabu. Jordan ilikuwa inaiwania Lebanon, Syria na Palestina wakati Iraq ikiilenga Syria. Misri nayo haikuficha azma yake ya kutaka kuwa taifa lenye kauli ya mwisho katika nchi za Kiarabu. “We will play the part in the Arab League that Britain does in the British Commonwealth”, alijigamba Mahmoud Abdil Fatah wa Misri akimaani- isha kwamba Misri itakuwa na nafasi kama ya Uingereza katika Jumuiya ya Madola. Madai haya yalipata nguvu kwani Makao Makuu ya Umoja wa nchi za Kiarabu yalikuwa Cairo nchini Misri na Katibu wake Mkuu, Mussa Azzam alikuwa pia raia wa Misri. Kuonesha jinsi Misri nayo ilivyotaka kupewa mamlaka juu ya Wapalestina, nci hiyo iliahidi kumsaidia Al-Alami Pauni 50,000 kwa ajili ya mfuko wa kutetea ardhi ya Wapalestina. Alipofuatilia kupewa fedha hizo, serikali ya Misri ilipunguza kiasi hicho hadi pauni 20,000 na baadaye haikutoa kabisa. Al-Alami alipouliza alijibiwa: “Kama Misri itaruhusiwa kuamua pesa hizo impe nani itatoa pauni 200,000”. Maana yake ni kwamba Misri ilikuwa inataka iuziwe mamalaka ya kuamua hatma ya ardhi ya Palestina.(Tazama The Arab States and the Palestinian Conflict, uk. 145). Syria na Iraq nazo zilikuwa na malengo yao kuhusu Palestina na hazikuwa zikimuamini Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Mussa Azzam. Vongozi wa Iraq hawakumuamini Azzam na waliona wachukue wenyewe juhudi zao kuhusu Palestina kupitia kuungaji mkono wao wa mpango wa kukomboa ardhi ya Palestina, yaani Istiqlaal. Syria nayo ilikua na mkakati wake kuhusu Palestina uliojulikana kama Kamati kwa Ajili ya Kuihami Ardhi ya Palestina (Committee for Defence of Palestine) ambapo wapiganaji kutokea Syria walikuwa wakiingia na kutoka Palestina wakipeleka huko silaha na misaada mbali mbali. Kama zilivyokuwa Jordan, Syria na Iraq, Saudi Arabia na Misri nazo zilikuwa na mitazamo yao kuhusu Palestina. Kila moja ilijiona ndiyo taifa kiongozi wa mataifa ya Kiarabu hivyo kwa wakati wao kila moja lilijaribu kufanya ushawishi kwa Marekani. Kwa mfano, Misri na Saudi Arabia zilikataa katakata mpango wa Rais Truman wa Marekani wa mwezi Oktoba uliopanga kuingiza wakimbizi Wayahudi laki moja kwenda nchini Palestina. Hizi zilikuwa njama za kuongeza idadi ya Wayahudi lakini pia kuingiza wapiganaji kwa ajili ya kujenga jeshi la Kizayuni. Mkakati wa pamoja wa Waarabu ulihitajika kuikomboa Palestina kutoka mikononi mwa Waingereza na Wazayuni na k u w a p a Wapalestina uhuru waliouhitaji. Je, hili lilifanikiwa? Tukutane tena toleo lijalo inshaAllah.

 

Show More

Related Articles

Back to top button
Close