2. Ncha ya Kalamu

Hivi ndivyo watu wanavyotawaliwa na maasi

Ni maafa, maafa maafa. Ndivyo tunavyoweza kusema katika zama hizi ambazo watu wengi wametawaliwa na maasi na tamaa za ulimwengu. Inasikitisha kuona mwanadamu anafanya maasi hadharani bila ya hofu wala woga kwa kisingizio cha kwenda na wakati.

Kufanya maasi imekuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku ya mwanadamu. Huu ni mwenendo mbaya ambao huathiri madhumuni na malengo ya kuwepo kwetu hapa duniani, yani kumcha Allah.

Allah anasema katika aya mashuhuri: “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu.” [Qur’an, 51:56]. Lakini kwa sababu ya kuwapo vita baina ya haki na batili na mivutano mikubwa baina ya kambi mbili hizi kunapelekea wakati mwingine mizani kutetereka na mambo kuharibika hasa pale nguvu ya kishetani ya batili inapoonekana kushika hatamu katika jamii.

Hali hii inadhihirika wazi pale tunapoangalia masuala mbalimbali likiwamo la watu kudumu katika maasi, ambayo msingi wake ni kufuata matamanio ya kupita na starehe za muda.

Jamii inayopigia upatu au kuunga mkono masuala ya pumbao na maasi ni jamii ya watu wajinga, na kupitia ujinga wao huamini kuwa wataendelea kuwapo ulimwenguni. Ama jamii yenye watu wanaojitambua huwa hawashughulishwi na kufanya maasi kwa sababu wanafahamu huo ni mtego anaoutumia Iblis (shetani aliyelaaniwa) katika kuwanasa wanadamu.

Aidha, kufanya maasi ni jambo linalotia upofu na kuwafanya watu waiache haki na njia (dini) sahihi. Qur’ an Tukufu imejaa mifano mingi ya watu waliokuwa wanafanya maasi na kupelekea kungamizwa. Miongoni mwa hao ni watu (kaumu) wa Nabii Lut (amani ya Allah imshukie) ambao waliangamizwa kwa kosa la liwati, yani wanaume kujamiiana wenyewe kwa wenyewe na kuacha wanawake ambao ni twahara kwao kindoa.

Mfano mwingine ni watu wa Nabii Shuaib (amani ya Allah imshukie) walioangamizwa kwa kosa la kupunja katika vipimo na mizani. Jamii hizi na nyingine nyingi ziliangamizwa baada ya kushindwa kutanabahi hadi maasi yalipokuwa ni sehemu ya maisha yao.

Hii inathibitisha kuwa uasi ni jambo baya na lenye madhara kwa jamii nzima. Mwenyezi Mungu ameweka mipaka na anataka tusiichupe kwani licha ya sharia zake kuwafikiana na mahitaji ya binadamu, sharia hizo hazitegemei shauku na matamanio ya kibinadamu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na lau kuwa haki ingelifuata matamanio yao, basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.” [Qur’ an, 23:71].

Vile vile Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Watazuka watu katika umma wangu ambao watakuwa wamejaa matamanio kama ugonjwa wa kuambukizwa na mnyama unavyozagaa mwili mzima na kuathiri mishipa na viungo vyote.” [Abu Daudi].

Kwa kuzingatia hayo, Muislamu anatakiwa ajisalimishe katika matakwa ya Allah Muumba na Mtume wake. Hilo ni jambo rahisi mno kwa waumini hasa ikizingaziwa kuwa asili ya mwanadamu ni kupendelea kheri na kuchukia maovu (Nafsi zimeumbwa kupendelea kheri).

Vyovyote iwavyo, kufanya maasi ni kwenda kinyume na fitra (maumbile ya mwanadamu) na ndio maana kunaleta madhara na maangamizo. Mitume na Manabii (amani iwe juu yao) waliletwa ulimwenguni kwa sababu moja kubwa, nayo ni kuwatoa watu katika giza la upotovu na kuwapeleka kwenye njia (dini) ya Allah, kutekeleza maamrisho yake, kuamini upweke wake na kujiepusha na makatazo yake.

Hivyo Muislamu fanya hima urudi katika fitra sahihi na jiepushe na kufanya maasi. Tambua kila starehe ina mwisho wake, na kila neema ni yenye kupita (haitodumu). Dunia hii uliyopo sasa ni mfano wa kivuli chako; ukisimama husimama, na ukikifuata hukukimbia. Ikiwa walijua hilo vipi unafurahia umri (maisha) ilihali hujui umebakisha muda gani wa kuishi.

Je, wewe ni katika wanaofanya maasi?

Wanazuoni wametaja tabia na wasifu wa watu wenye kufanya maasi, na wale wanaopendelea zaidi kufuata rai na maoni yao kuliko sharia za Uislamu na amri zake. Moja ya tabia za watu hawa ni kwamba wanadharau, kukejeli na kupinga amri za Uislamu. Baadhi yao wamefikia kiwango cha kuifanyia mzaha Qur’ an, Sunna za Mtume na wale wanaoshikamana na viwili hivyo.

Tabia nyingine ya watu wanaodumu na kufanya maasi ni kufuata matamanio badala ya kushikamana na Sunna za Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) katika matendo yao ya ibada, desturi na hali zao. Hawa ndio aliowataja Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’an pale aliposema:

“Na katika watu wapo wanaobishana juu ya Allah bila ya elimu, wala uongofu, wala kitabu chenye nuru. Anayegeuza shingo yake ili kupoteza watu waache njia ya Allah. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua. (Ataambiwa). Hayo ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yako. Na hakika Allah si dhalimu kwa waja.” [Qur’ an, 22:8–10].

Ukitafakari kwa kina mambo haya utagundua kuwa wale waliojiingiza kwenye dimbwi la maasi wamemezwa na ujinga wa kujivunia yale yasiyobaki kwa ajili yao wala wao kubaki kwa ajili ya hayo. Kwa msingi huu, muislamu ana wajibu wa kuzingatia, kukubali na kutekeleza kwa nia na ikhlas mafundisho ya dini na kuyakimbia maasi

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close