4. Ncha ya Kalamu

Hii ndiyo thamani ya Muumini mbele ya Allah

Kuna haja kwa Waumini wa Kiislamu kuzikagua nafsi zao na kutambua namna imani yao inavyoweza kuwanyanyua, kuwalinda na kuwapa hifadhi dhidi ya maadui.

Yapo mambo mengi ambayo Allah Aliyetukuka ametutaka tuyahifadhi na kuyalinda ili kulinda heshima ya dini na watu wake.

Miongoni mwa mambo hayo ni masuala ya maadili, itikadi na tabia, mambo ambayo ni muhimu kila Muislamu kushikamana nayo. Ifahamike kuwa, Allah anao uwezo wa kuwaangamiza maadui wa Uislamu ikiwa ni njia ya kuutetea umma huu ambao ameuchagua kuwa umma bora kwa sababu ya watu wake kuamrishana mambo mema na kukatazana mabaya.

Hata hivyo, thamani ya Muislamu inaweza kushuka pale atakaposhindwa kujitofautisha na watu waovu na kutegemea zaidi mambo ya kiulimwengu na kupuuza utaratibu na mafundisho ya dini ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayomfungamanisha na Mola wake Mlezi.

na anapotaka kuwanusuru watu wema haangalii ukubwa au nguvu waliyonayo maadui, mali zitakazoteketea wala idadi ya watu watakaopata madhara

Tuitazame thamani ya Muumini mbele ya Allah pindi Allah anapoamua kumtetea na kumnusuru na matatizo na majanga makubwa ya kilimwengu. Yako mambo mengi ambayo tunaweza kujifunza kupitia kisa cha Nabii Nuhu (amani ya Allah imshukie). Miongoni mwa mambo hayo ni thamani ya Muumini mbele ya Allah.

Thamani ya Muumini
Thamani ya muumini haiwezi kulinganishwa na kitu chochote kile hapa ulimwenguni. Allah ‘Azza Wajallah’ alithamini juhudi ya Mtume wake, Nuhu (amani ya Allah imshukie) na kundi dogo la watu waliomuamini na kumfuata, hivyo akawanusuru na adhabu na akaliangamiza kundi kubwa la watu waovu bila kujali utajiri, hadhi na vyeo vyao. Allah aliwapandisha hadhi na kuwanyanyua daraja wafuasi wa Nabii Nuhu kutokana na imani yao sahihi katika kumpwekesha Allah na kujisalimisha kwake kimatendo na kitabia.

Kufaulu huko kwa kikundi kidogo cha wafuasi wa Nabii Nuhu, ambao baadhi ya riwaya zinasema kuwa walikuwa 15 ni mavuno ya kazi ya ulinganiaji iliyofanywa na Nabii Nuhu (amani ya Allah imshukie) kwa muda wa miaka 950. Nabii Nuhu aliwalingania watu wake usiku na mchana, kwa njia ya siri na dhahiri hatimaye akapata wafuasi kiduchu ambao Allah aliwanusuru na kuwalinda na maangamivu.

Kwa upande mwingine, Allah aliwaangamiza watu waovu ili kabadilisha nidhamu ya ulimwengu na kuwajulisha watu kuwa yeye anao uwezo wa kuwaadhibu makafiri na kuwahami Waumini, na anapotaka kuwanusuru watu wema haangalii ukubwa au nguvu waliyonayo maadui, mali zitakazoteketea wala idadi ya watu watakaopata madhara.

Sehemu kubwa ya watu duniani hivi sasa wamerejea katika zama za ujahili (ujinga), dhulma, uonevu, maasi na machafu ya aina mbalimbali, na baadhi yao wamekuwa wakiwapiga vita na kuwakejeli watu wanaokemea maovu. Hawa hawatofautiani sana na watu wa Nabii Nuhu, ambao mara kwa mara walikuwa wakiziba masikio yao ili wasisikie mahubiri ya Nabii wao, Nuhu (amani imshukie).

Allah ananukuu maneno ya Nabii Nuhu (amani ya Allah imshukie) ambaye amesema: “Na hakika mimi kila nilipowaita ili upate kuwasamehe, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno!” [Qur’an, 71:7].

Katika zama za sasa, watu hawazibi masikio wala kujifunika kwa nguo bali wanabuni njia nyingine za kuwafanya watu wapende kusikiliza na kufuata upotovu badala ya haki.

Hakika kuwapo kwa watu wema katika dunia hii ni jambo kubwa katika mizani ya Allah, ni jambo linalohalalisha kulinusuru kundi la watu wema na kulilinda ili liweze kurithi ardhi hii na kulingania mambo mema. Waumini hawapaswi kujidunisha wala kujidharau bali wanatakiwa kuishi na hisia hizi na kutambua kuwa wao wana thamani kubwa mbele ya Allah.

Waumini wanao uwezo wa kufanya jambo lolote ikiwa watasimama katika misingi thabiti ya kiimani, kutenda mema na kujipamba na tabia njema. Wakati Nabii Nuhu (amani ya Allah imshukie) alipokuwa akitengeneza Safina viongozi na wakuu wa jamii za washirikina walimbeza, kumkejeli na kumpiga, lakini hatimaye Allah alimnusuru.

Nabii Nuhu alimuelekea Mola wake kwa maombi hadi ilipokuja adhabu ya maangamizi. Allah anasema: “Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika. Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo liliokadiriwa.” [Qur’an, 54:11–12].

Hivi ndivyo jamii ya Kiislamu inapaswa kuishi katika kila zama na kila mahali. Waislamu waelewe kuwa katika nyoyo zao wamebeba imani sahihi ambayo ni muhimu kuliko kitu
chochote ulimwenguni na ndiyo maana Allah anawanusuru na kuwalinda na vitimbi vya watu waovu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close