2. Ncha ya Kalamu

Hicho ni kipande cha moto; una hiyari ya kukitwaa au kukiacha

Kutoka kwa Ummu Salama (Allah amridhie) amesema, siku moja Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alisikia kelele za ugomvi karibu na mlango wa chumba chake, akatoka na kusema (kuwaambia watu wanaogombana):

Hakika mimi ni binadamu na si vinginevyo huwa nahukumu kulingana na kile nilichokisikia, na huenda baadhi yenu wakawa na uwezo zaidi wa kutoa hoja kuliko wengine (wakapindisha ukweli). Kwa hiyo yule ambaye nitahukumu kwa kumpa haki ya Muislamu, hakika hicho ni kipande cha moto – aidha akichukue au akiache.” [Bukhari na Muslim].

Na katika riwaya nyingine, Imam Abuu Daudi amesema: “Watu wawili wenyeji wa Madina (Ansaar) walikuja nyumbani kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ili kutafuta suluhu ya mgogoro wa mirathi lakini hawakuwa na ushahidi. Mtume akawaambia kuwa yeye ni binadamu na anahukumu kulingana na kile alichokisikia, na huenda baadhi ya watu wakawa na uwezo wa kutoa hoja kuliko wengine (wakapewa mali isiyowahusu). Kwa hiyo, yule ambaye nitahukumu kwa kumpa haki ya Muislamu, atambue kuwa anachukua kipande cha moto.”

Mafundisho ya tukio
Katika tukio hili tunatahadharishwa kudhulumu, kufanyiana uadui na kuchukua mali za watu pasina haki ya kufanya hivyo. Kinachotakiwa kwa Muislamu ni kuitafuta haki na akusudie kuipata kwa njia ya haki.

Pia, katika tukio hili tunajifunza kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) hakuwa anajua mambo yaliyofichikana (ghaibu) wakati wa uhai wake kama alivyobainisha yeye mwenyewe.

Mtume amesema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Lau ningeyajua yaliyofichikana bila shaka ningejizidishia mema mengi, wala ovu lisingenigusa. Mimi si chochote ila ni muonyaji na mbashiri kwa watu wanaoamini.” [Qur’an, 7:188].

Aya hii inathibitisha wazi kwamba Mtume hakuwa anajua mambo yaliyofichikana (ghaibu) isipokuwa yale mambo aliyofahamishwa na kupewa wahyi (ufunuo) na Mola wake. Mtume aliwahukumu watu kupitia utaratibu wa kisharia kwa kuzingatia hoja na ushahidi wa wazi. Mtu atakayetoa hoja zinazokinaisha au ushahidi wa wazi ndiye atakayepewa ushindi katika kesi hiyo hata kama amepindisha ukweli. Jambo hili ndilo lililomfanya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), kwanza kuwalingania wale watu wawili waliokuwa wakigombana kabla ya kutoa hukumu baada ya kusikiliza hoja zao.

Kushinda kesi hakuhalalishi dhulma
Mtu yeyote atakayewasilisha mahakamani vielelezo vya uongo au kutoa ushahidi wa uongo kwa lengo la kumdhulumu mwenzake atambue kuwa kufanya hivyo ni dhambi kubwa mbele ya Allah. Mtume aliwahukumu watu baada ya kupitia vielelezo na ushahidi wa pande zote (upande wa mlalamikaji na ule wa mlalamikiwa) bila kuacha shaka yoyote.

Ajabu ni kwamba katika zama zetu hizi kuna watu wengi wanaodiriki kutoa ushahidi wa uongo mahakamani ili kupata mali kwa njia ya dhuluma. Imepokewa Hadithi kutoka kwa Ummu salama (Allah amridhie) akisema: “Nilimsikia Mtume (rehema na amani zimshukie) akisema: Hakika kuna watu wanajichukulia mali za Allah pasina haki, malipo yao yatakuwa ni moto.” [Bukhari].

Kutoa ushahidi wa uongo ili kushinda kesi hakuhalalishi mali ya haramu bali kufanya hivyo ni kujiandalia makazi mabaya katika moto wa Jahannam Siku ya Kiyama. Ikiwa wewe ni mmoja kati ya wale wanaodhulumu haki za watu, kaa ukitambua kwamba dhuluma unazozifanya zitabaki kuwa deni Siku ya Kiyama.

Ni kwa kutambua hayo yote, Mtume (rehema na amani zimshukie) akatutahadharisha kwa kusema: “Aliyekuwa na kitu cha dhulma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham. Ikiwa ana amali njema, basi (Siku ya Kiyama) zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe.” [Bukhari].

Tahadhari kwa mawakili na wanasheria
Tukio hili lina mazingatio makubwa kwa mawakili na wanasheria kwani asilimia kubwa ya wasomi hawa wa sheria hawajali hali za wateja wao katika uendeshaji wa kesi mahakamni. Ni ukweli kuwa wapo baadhi ya mawakili ambao hutumia taaluma yao kwa manufaa binafsi ikiwa ni pamoja na kuwatetea watu waliodhulumu mali za watu ili na wao wajipatie chochote.

Baadhi yao hutumia mbinu mbalimbali na vifungu vya sheria ili kuhakikisha kuwa wateja wao wanashinda kesi huku wakijua kuwa vielelezo walivyoviwasilisha mahakamani ni vya kughushi. Mawakili waelewe kuwa, kufanya hivyo ni kusaidia dhulma na kusababisha ufisadi katika ardhi. Labda tujiulize, ni watu wangapi ambao wamepoteza mali zao kwa sababu
mbalimbali zikiwamo kutojiamini, kuogopa, kushindwa kujieleza au kukosa mawakili wa kuwatetea mahakamani? Na je, ni watu wangapi ambao kwa sababu ya kukosa watetezi wamejikuta wakisota magerezani? Allah Aliyetukuka anaonya:

Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyokuonesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe mtetezi wa watu wenye kufanya hiyana. Na muombe Allah msamaha, Hakika Allah ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu. Wala usiwatetee wanaozifanyia hiyana nafsi zao. Hakika Allah hampendi mwenye kufanya hiyana, mwenye dhambi” [Qur’an, 4:105–107].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close