2. Ncha ya Kalamu

Haki ya kuabudu shuleni izingatiwe

Kumekuwa matukio kadhaa ya wanafunzi wa Kiislamu katika baadhi ya shule za msingi na sekondari wakilalamikia kunyimwa ruhusa ya kuhudhuria ibada ya sala siku ya Ijumaa.

Baadhi ya walimu katika shule hizo wanasema wamefikia hatua hiyo kutokana na baadhi ya wanafunzi kuchelewa kurejea shuleni baada ya kumalizika sala; pia wengine kufanya vitendo viovu wawapo njiani.

Tunachofahamu ni kuwa, zipo haki za msingi za binadamu ambazo hazitegemei ridhaa ya mtu yeyote. Na haki si fadhila ambayo mtu anaweza kupewa na kupokonywa wakati wowote.

Uhai na kuishi ni haki ya msingi ya binadamu yeyote, na katiba za nchi zote duniani hata zile zisizofuata mfumo wowote wa dini zimeitambua haki hii japo kwa maandishi tu.

Linaloambatana na haki hii ni haki ya kuabudu. Mantiki ya haki hii ni kuwa ibada ni jambo la kiroho na takatifu. Si hivyo tu, pia ibada ni wajibu ambao mtu anapaswa kuutekeleza katika maisha yake ya kila siku, na hakuna yeyote aliyeidhinishiwa kuupora wajibu huo.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua. Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa.” [Qur’an, 62:9-10]

Kwa kuzingatia hilo ndio maana tunahoji, ni kwanini haki ya wanafunzi wa Kiislamu kuhudhuria ibada siku ya Ijumaa inakiukwa? Ni haki yetu Waislamu kuelezwa kama ipo sheria ya nchi iliyohalalisha kukiukwa haki hiyo.

Sote tunafahamu kuwa kila mtu ana haki ya kuamini dini apendayo. Vivyo hivyo, Waislamu kuitukuza siku ya Ijumaa ni moja ya mambo ya msingi katika imani yao. Hivyo, ni makosa na ni kukiuka katiba kuwazuia wanafunzi wa Kiislamu kuhudhuria msikitini Siku ya Ijumaa.

Labda tujiulize swali hili, japo ni siku ya mapumziko, je, yawezekana kuwazuia wanafunzi wa bweni wanaosoma shule za kikatoliki kwenda kanisani siku ya Jumapili kwa hoja kwamba wengine wakipewa ruhusa hiyo wanaishia kilabuni kunywa pombe? Bila shaka jawabu ni hapana. Kwa msingi huo, pia hatutarajii kwa mwalimu yeyote wa shule awazuie wanafunzi kwenda msikitini siku ya Ijumaa kwa hoja ya kuchelewa kurejea shuleni au kufanya vitendo viovu wawapo njiani.

Wanachoweza kukifanya walimu ni kuweka utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa wanafunzi wao na ikibainika kuwapo wanaohujumu fursa hiyo waadhibiwe na sio kuwanyima haki ya kwenda msikitini.

Suala la kuabudu ni haki ya msingi ya kikatiba hivyo ni lazima liheshimiwe. Na tunadhani ni muhimu masheikh na viongozi wa dini wachukue fursa hii kuwaelimisha waislamu waliopo sehemu za kazi, shuleni na vyuoni, juu ya haki ya kuabudu.

Pia, ni muhimu serikali iwe makini juu ya masuala haya, kwani moja ya mambo yanayochochea kuwapo uhusiano mbaya kati ya raia na serikali ni raia kuhisi wanaonewa, kupuuzwa na kudhulumiwa haki zao.

Na ili kuzuia hali hiyo isitokee ni vema yanapoibuka malalamiko yatazamwe kwa uadilifu na kama kweli wapo walimu wanaokiuka katiba ya nchi wachukuliwe hatua za kisheria.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close