4. Ncha ya Kalamu

Elimu ni amana, tuitumie kiuadilifu

Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema: “Baadhi ya watu katika jamii hutumia elimu, ujuzi na maarifa yao kuangamiza, kubomoa na kudumaza ustawi wa jamii ili kulinda maslahi yao binafsi.”

Rais Mstaafu Mwinyi anaamini kuwa elimu ikitumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kujiletea maendeleo chanya na endelevu, taifa litafikia malengo iliyojiwekea katika muda mfupi.

Mwinyi, ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Zanzibar kuanzia mwaka 1984 hadi 1985, alipata umaarufu mkubwa kutokana na sera yake ya kufufua na kuimarisha uchumi wa nchi. Yeye alirithi nchi yenye uchumi uliozorota, na kutokana na ugumu uliokuwapo wakati huo, aliamua kufanya mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na nchi wahisani ili kufufua uchumi wa Tanzania.

Ni elimu, busara na uzalendo vilivyomuwezesha mpambanaji huyu kuwa na ujasiri wa kutosha kuwatumikia Watanzania wanyonge na masikini. Lakini, si Mwinyi pekee aliyetumia elimu na uzalendo kupambana na hali ngumu ya maisha ya wananchi wake, bali hata viongozi wengine wa Afrika kama vile Muammar Gaddafi, Gamal Abdel Nasser, Nelson Mandela na wengineo wengi. Hawa wote waliweza kutumia fikra pevu iliyotokana na elimu kuzikwamua nchi zao na lindi la umasikini. Kwa hakika, itoshe kusema kuwa, uzalendo kwa Mzee Mwinyi haukuanza leo wala jana. Ajabu ni kwamba kadri miaka inavyosonga, mambo yanabadilika kwani elimu ambayo ilidhaniwa kutumiwa na wasomi kuikwamua jamii na changamoto za kimaisha, hivi sasa imekuwa kaa la moto.

“Kisha kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema (mlizopewa mlizitumiaje).” (Qur’ an, 102:8).

Wasomi wengi wa sasa wanaongoza kwa dharau na wanapenda kusifiwa na kuabudiwa badala ya kuwa wanyenyekevu. Najiuliza wasomi hawa wenye viburi, majivuno na dharau watawezaje kuwasaidia/kuwaelekeza watu wenye uelewa mdogo na kutatua matatizo yao?

Ni wasomi wetu hawa waliogeuka ‘mazuzu’ wakitumia elimu yao vibaya kwa kupanga kuwadhuru watu wengine ili kulinda maslahi yao – aidha ya kisiasa au ya kiuchumi. Ni kawaida siku hizi kusikia msomi mwenye shahada ya chuo kikuu amekamatwa kwa kosa la kutoa/kupokea rushwa, kutakatisha fedha, ufisadi au uhujumu uchumi. Kama hali ni hiyo kwa wasomi; je, wananchi ambao hawakupata elimu wakimbilie wapi?

Uzuzu umewafanya wasomi wetu wawe wauaji wakubwa. Hebu fikiria mhandisi wa majengo anapowasaliti wananchi kwa kusimamia ujenzi wa maghorofa yasiyo na viwango na hatimaye majengo hayo yanaporomoka na kuangamiza watu.

Fikiria daktari anapoamua kumuomba rushwa mwananchi masikini ambaye hata kupata chakula chake ni tabu. Je, huyu daktari si anataka masikini asipate matibabu na hatimaye apoteze maisha?
Tumchukuliaje, Bwana shamba/mifugo anayekataa kuwahudumia wakulima/ wafugaji eti mpaka apate kitu kidogo?
Na je, kuna tija gani kwa mwalimu/mhadhiri kumfelisha mtihani mwanafunzi wa kike kwa sababu tu amemnyima penzi. Hii ni dalili kuwa idadi kubwa ya wataalamu wetu wamekosa maadili na hofu ya Mungu.

Elimu ni amana
Elimu ni amana na neema ambayo Mwenyezi Mungu amewatunuku wanadamu, hivyo yeyote aliyejaaliwa elimu na akaitumia katika kufanya wema, basi kwa hakika ameitekeleza amana ipasavyo. Elimu ni msingi wa maendeleo ya watu na ustawi wao. Mataifa kama Marekani, Uingereza, Urusi, Japan, Ujerumani, China yanafanya juhudi kubwa katika kusomesha raia wake wakiamini kuwa elimu ndio nyenzo pekee ya kukabiliana na changamoto za ulimwengu
wa sasa.

Yapo maswali mengi ya kujiuliza, miongoni mwa hayo ni: Je, tuwachukulie hatua gani wale wanaosoma lakini hawatumii elimu yao kuitumikia jamii na taifa lao? Binafsi sina majibu ya swali hili, lakini naamini tunaweza kuibadili hali iliyopo na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye wasomi wenye maadili, waadilifu na wenye kujitambua.

Wahenga walituusia kuwa elimu ni bora kuliko mali. Hii ina maana kuwa, kadiri mtu anavyoitumia elimu ndivyo anavyojiongezea maarifa na ujuzi, tofauti na mali ambayo kila inapotumika ndivyo inayvyokwisha. Kwa mnasaba huu, yapasa tutumie fikra na ubunifu utokanao na elimu katika kuleta chachu na mwamko mpya wa kutatua changamoto za watu.

Haifai na wala haipendezi kwa mtu anayejiita ‘msomi’ kujihusisha na vitendo viovu vya ulaji rushwa, ufisadi nabuhujumu uchumi. Wasomi waelewe kuwa elimu waliyoipata ni amana na neema ambayo Mwenyezi Mungu ataiuliza Siku ya Kiyama, kama anavyosisitiza ndani ya Qur’an: “Kisha kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema (mlizopewa mlizitumiaje).” (Qur’ an, 102:8).

Pia, tunasoma katika hadithi kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu mwenye busara (akili) ni yule aliyeihifadhi nafsi yake na akafanya matendo (amali) mema kwa ajili ya maisha baada ya kifo. Na mtu ajizi (mlemavu wa akili) ni yule aliyeyaendekeza matamanio nafsi yake na akatamani amani (isiyo na amali njema) kwa Allah.” (Tirmidhiy).

Fundisho la ndani tunalolipata katika hadithi hii ni kwamba, upo uhusiano wa karibu baina ya mtu aliyetumia elimu yake vibaya hapa ulimwenguni na adhabu ya moto wa Jehannam Siku ya Kiyama. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie kuwa miongoni mwa waja wake wanaosikia maneno mazuri na kuyafanyia kazi. Amin

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close