2. Ncha ya Kalamu

Bid’a zifanywazo katika Mwezi wa Rajab

Alhamdulillah, tumejaaliwa kuufikia mwezi wa Rajab, kama tuuitavyo kwa Kiswahili, ‘Mfungo wa kumi’, ambao ni mwezi wa saba katika Kalenda ya Kiislamu maarufu kama Kalenda ya Hijriyya.

Hapana shaka kwamba, mwezi wa Rajab ni mwezi wenye hadhi kubwa mbele ya Allah kwa sababu ni miongoni mwa miezi mitakatifu. Allah ameitaja miezi hiyo katika Qur’an na akawakataza Waislamu kutojidhulumu nafsi zao kwa kutenda maasi au kuzembea kufanya ibada ndani yake.

Allah anasema: “Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah ni 12 tangu siku alipoumba mbingu na ardhi. Minne kati ya hiyo ni miezi mitakatifu, hiyo ndiyo dini ya sawa sawa, basi msizidhulumu nafsi zenu ndani yake [miezi hiyo].” [Qur’an 9:36].

Kwa hiyo, hapana shaka kwamba mwezi wa Rajab ni katika miezi minne mitakatifu kwa mujibu wa Qur’an na Sunna. Lakini kuwa kwake miongoni mwa miezi minne mitakatifu si kibali kwa Waislamu kuelekee mwezi huu kwa ada fulani fulani kwani hakuna ibada zilizowekwa na Allah kupitia Mtume wake mahsusi kwa mwezi huu tu.

Ni kwamba, haijathibiti kutoka kwa Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) kitendo chochote kile cha kiibada kwa hiyo yafanywayo na watu ndani ya mwezi wa Rajab ni ada tu na siyo ibada. Matendo ya kiibada ni ‘Tawqiifiyyah,’ yaani ni haramu mtu kufanya jambo akaliita ibada isipokuwa kuwe na dalili kutoka katika Qur’an na Sunna kwa Hadithi sahihi za Mtume.Wale wafanyao matendo ya uzushi katika miezi mitakatifu wanaweza wakawa na nia njema lakini nia njema pekee haifanyi kitendo kiwe ibada. Ili kitendo kikubalike kuwa ni ibada, ni lazima kiwe kimefundishwa na Mtume wa Allah na kifanywe kwa nia njema.

Ndani ya mwezi wa Rajab hufanyika matendo yakihesabiwa na watu kuwa ni ibada wakati hayapo katika hukumu za ibada katika Uislamu. Wanafanya hivyo aidha kwa kutokujua au kwa kujua, lakini wameweka mbele maslahi ya kidunia kama vile kujipatia mali au ukubwa na vyeo. Hawa wamesahau kuwa, maslahi haya ya kidunia hayatawasaidia Siku ya Kiyama.


Ndugu msomaji, tumekuwekea kauli za wanawachuoni kuonesha kuwa matendo mengi yafanyikayo mwezi wa Rajab ikiwa ni pamoja na kusherehekea usiku wa Israi na Miiraj ni uzushi

Sheikh Muhammad Issa

Bid’a katika mwezi wa Rajab
Huenda Rajab ndio mwezi ambao hudhihirika zaidi bid’a; na kwa kuwa tuko katika mwezi wa Rajab, nimeona ni vema kuandika kuhusu bid’a na mambo ya upotofu yanayofanyika katika mwezi huu mtakatifu. Kinachowafanya watu wazue bid’a hizi ni kule kudhania kwao mwezi huu una utakatifu kuliko miezi mingine. Anasema Ibn Hajar Al-Asqalaniy (Allah amrehemu): “Hakuna ushahidi wowote unaoonesha ubora wa mwezi wa Rajab si kwa kufunga swaumu sehemu au mwezi mzima wala kisimamo cha usiku maalum ndani yake.” [Taz: Tabyiinul ‘Ajab Bimaa Warada fiy Fadhli Rajab, uk. 6].

Ibn Hajar (Allah amrehemu) ni katika wanazuoni wakubwa katika Madhehebu ya Imam Shafi. Maneno kama haya haya yako pia katika kitabu kingine kiitwacho, As-Sunan Walmubtada’aati cha Imam Al-Qushayriiy,’ uk
125]. Amesema tena Ibn Hajar (Allah amrehemu): “Ama Hadithi zilizopo kuhusu fadhila za mwezi wa Rajab au fadhila za swaumu ndani yake ziko za aina mbili -dhaifu au zilizozushwa…” [Taz: As-Sunan Walmubtada’aati cha Imam Al-Qushayriiy, uk. 8].

Mfano wa hizo ni Hadithi dhaifu isemayo: “Hakika peponi kuna mto unaitwa Rajab, maji yake ni meupe kuliko maziwa na matamu kuliko asali Yeyote mwenye kufunga swaumu siku moja tu katika mwezi wa Rajab, Allah atamywesha maji ya mto huo.” [Taz: Ad-Daylaamiy, juz 1/ uk. 281].

Hadithi nyingine dhaifu ni ile isemayo “Ilikuwa ikiingia Rajab, Mtume wa Allah akisema, ‘Ewe Mola wangu tubariki katika mwezi wa Rajab na Shaban na utujaalie tuufikie mwezi wa Ramadhan.’” [Ahmad]. Tanbihi: Hadithi dhaifu hazifai kutumika kwa hukumu ya ibada au hukumu yoyote ile ya kisharia kwa makubaliano ya wanawazuoni wa elimu ya hadithi.

Je Israi na Miiraj zilitokea katika Rajab?
Hakuna shaka kwamba Israi na Miiraj ni matukio mawili yaliyotokea kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na ni miongoni mwa miujiza aliyopewa na Allah. Lakini kila mwaka katika mwezi wa Rajab watu husherehekea usiku wa Israi na Miiraj ifikapo tarehe 27 Rajab wakati hakuna ushahidi wa kuaminika kwamba matukio ya Israi na Miiraj yalitokea tarehe hiyo. Amesema Ibn Hajar (Allah amrehemu): “Na baadhi ya wasimulizi wametaja kwamba Israi ilitokea katika mwezi wa Rajab na huo ni uongo.” [Taz: Tabyiinul ‘Ajab, uk.6].


Ilikuwa ikiingia Rajab, Mtume wa Allah akisema, ‘Ewe Mola wangu tubariki katika mwezi wa Rajab na Shaban na utujaalie tuufikie mwezi wa Ramadhan.’” [Ahmad].

Naye Sheikhul Islaami ibn Taymiya (Allah amrehemu) amesema: “Haikusimama dalili maalumu kuhusu Israi na Miiraj ilitokea mwezi gani au kumi la ngapi la mwezi au siku gani, bali yaliyonukuliwa kuhusu hilo ni habari zilizokatika katika, hakuna usahihi moja kwa moja” [Taz: Latwaaiful Ma’aarif cha Ibn Rajab Al-Hambaliy, uk. 233].Hata kama ingethibiti kwamba Israi na Miiraj vilitokea usiku wa tarehe fulani, isingefaa kwa yeyote kuuadhimisha usiku huo maalum kwa matendo fulani.

Kwa ujumla, haikuthibiti kwa Mtume wala yeyote katika Maswahaba wake wala Taabiiina kuufanya usiku huo kuwa usiku wa ibada au sherehe ambazo ni katika Bid’a za kuchukiza kabisa [Taz: Ibnul Haaj katika Al-Mad-
khali, uk. 211-212].

Ushahidi kwamba Israi na Miiraj havikuwa 27 Rajab
Kusema kwa yakini kwamba usiku wa tarehe hiyo ndiyo Israi na Miiraj na watu wakakesha wakisoma kisa cha Israi Miiraj ni kwenda kinyume na Ijmaa ya wanawazuoni wa madhehebu zote za Ahlu Sunnah Wal Jama’ah.

Maulamaa wametofautiana sana kuhusu tarehe ambayo Israi na Miiraj vilitokea na miongoni mwa kauli hizo ni hizi zifuatazo: Kwanza, Israi na Miiraj vilitokea mwaka mmoja kabla ya Hijra ya Mtume kutoka Makka kwenda Madina. Amesimulia Imam Nawawiy (Allah amrehemu): “Israi na Miiraj vilitokea tarehe 27 mwezi wa Rabiiul Aakhir -Mfungo wa Saba [Taz:
Sherhu Muslim, juz 2/ uk. 209]. Pili, amesema Ibn Duhayyah Al-Kilaabiy (Allah amrehemu) akimnukuu Imam Nawawiy akisimulia kwamba Israi na Miiraj vilitokea tarehe 27 mwezi wa Rabiiul Awwal –Mfungo wa Sita [Taz: Sherhu Muslim].

Kwa hiyo, zimenukuliwa kauli mbili tofauti kutoka kwa Imam Nawawiy. Kisha Ibn Hajar akasema: “Hakika kama kauli ya Israi na Miiraj vilitokea mwaka mmoja kabla ya Hijra ya Mtume ingeswihi, ingekuwa alichonukuu Ibn Duhayyah ndiyo karibu na ukweli. Hii ni kwa sababu Hijra ya Mtume ilikuwa mwezi wa Mfungo wa Sita hivyo mwaka mmoja nyuma inaangukia katika mwezi wa Mfungo wa Sita, kama alivyonukuu Ibn Duhayyah kwamba Israi na Miiraj vilitokea katika mwezi huo [Taz: Tabyiinul ‘Ajab, uk. 9]. Kisha Ibn Hajar (Allah amrehemu) akasema: “Mimi sijaikuta kauli iliyosimama katika dalili ya nguvu (kuhusu Israi na Miiraj kuwa katika mwezi wa Rajab).” Tatu, kuna kauli kwamba Israi na Miiraj vilitokea mwezi mmoja na nusu kabla ya Hijra ya Mtume lakini si katika mwezi wa Rajab. Nne, kwamba Israi na Miiraj vilitokea mwezi 27 Rajab.

Anasema Ibn Hajar (Allah amrehemu): “Kauli hii ipo pamoja na kwamba haina dalili yenye hoja na hakuna Hadithi sahihi wala dhaifu wala ya kutunga na hakuna kauli ya yeyote katika wema waliotangulia. Pamoja na ukweli huo, watu wengi wamekuwa wakiitakidi hivyo.

“Si hivyo tu, bali wanaongeza juu yake itikadi batili kwa kufanya matendo katika usiku huo ambayo Iblis aliyelaaniwa amewapambia.Miongoni mwa matendo hayo ni kusherehekea jambo ambalo hakuteremsha Allah dalili, kisha kukusanyika na kula na kujaza matumbo kuwa aina mbali mbali za vyakula na vinywaji. Kisha wanasimama wakiwa wameshikana mikono wakimdhukuru Allah wakinesanesa kulia na kushoto, mbele na nyuma, wakitunga mashairi mazuri mazuri na sauti za kuvutia hadi vilivyo katika matumbo yao viyeyuke! Pamoja na hayo, wao wanaamini kwamba wanatenda jambo jema!

Jambo linaloshangaza siyo wasiojua kitu wafanyao hayo bali wale wenye elimu wajiitao wanazuoni. Hawa wanajuzisha na kutoa fatwa kwa wale wasiojua, kwamba, matendo hayo (kusherehekea Israi na Miraj) yanajuzu.” [Tabyiinul ‘Ajab, uk 13].

Ndugu msomaji, tumekuwekea kauli za wanawachuoni kuonesha kuwa matendo mengi yafanyikayo mwezi wa Rajab ikiwa ni pamoja na kusherehekea usiku wa Israi na Miiraj ni uzushi. Hakuna wajibu juu letu isipokuwa kufikisha ili mwenye kutaka afuate uongofu kwa ajili ya nafsi yake na asiyetaka aukatae kwa madhara ya nafsi yake.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close