2. Ncha ya Kalamu

Ahsanteni nyote mliohudhuria Kongamano la Misk ya Roho

Desemba mosi ya mwaka huu ilikuwa ni siku ya furaha kwa Waislamu wa Afrika Mashariki pale walipokutana kwa minajili ya kupashana ujumbe wa dini yao tukufu ya Uislamu.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam ambapo Masheikh saba tofauti kutoka ndani na nje ya Tanzani walitoa mada mbalimbali kuhusu Kitabu kitukufu cha Qur’ an.

Ni faraja sana kuona tukio la kidini likihudhuriwa na umati mkubwa kama ule, zaidi ya watu 5,000, ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee huku wengine wakifuatilia kupitia vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii. Huu ni ushahidi wa athari ya Uislamu, dini pekee ya kweli mbele ya Mwenyezi Mungu. Pia, huu ni ushahidi wa mapenzi ya Waislamu kwa Mola wao na Mtume wao, Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie). Waislamu waliohudhuria walipata ujumbe maridhawa kutoka kwa wahadhiri wa ndani na nje ya Tanzania ambao ni pamoja na Sheikh Djumapili Mbabajende kutoka Rwanda, Sheikh Yusuf Abdi (Kenya), Sheikh Zuberi Bizimana (Burundi) na Sheikh Muhammad Abduweli kutoka Uganda. Wengine ni Sheikh Ibrahim Twaha na Dkt. Sheikh Salim Qahtwan, wote kutoka Tanzania na Sheikh Abubakar Abdi (Abu Hamza) kutoka Kenya.

Wahadhiri hao waligusia mambo mbalimbali yaliyomo ndani ya Qur’an Tukufu. Mambo hayo yameelezwa kwa kina katika habari zilizochapwa katika toleo hili.

Kimsingi, mada zilizowasilishwa katika kongamano la Misk ya Roho mwaka huu ni muhimu mno kwani zinaihuisha imani na kutanabaisha juu ya umuhimu wa kushikamana na mafundisho ya Qur’an. Hivyo, tunasema Waislamu wamevuna elimu kubwa wanayotakiwa kuifanyia kazi ipasavyo kwa ajili ya faida yao ya hapa duniani na kesho akhera.

Tuna kila sababu ya kuwashukuru na kuwapongeza wahadhiri wote kwani walifanya kazi kubwa ya kukonga nyoyo za wahudhuriaji. Pia, tunawapongeza watu wote waliohudhuria Kongamano hilo na wale waliofuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kuhudhuria kwao ndiyo ilikuwa chachu ya kufanikiwa kwa kongamano hilo, hivyo tunazidi kuwaomba waendelee kushiriki katika makongamano yatakayofuata.

Itakuwa ni uchoyo wa fadhila endapo tutahitimisha tahariri hii bila ya kuwapongeza na kuwashukuru wadhamini wote wa Kongamano la Misk ya Roho mwaka huu.

Wadhamini hao ni wale wa Platnum ambao ni Asas Dairies Ltd ya Iringa na Afya pure drinking water. Kwa upande wa dhahabu (Gold) ni Dar Al Ber Society, Afiya Juice, Dar fresh Milk, O-GAS na Fedha (Silver) ni Usangu logistics (T) Limited na shirika la ndege la Emirates, Carmel floor milk na kampuni ya mafuta ya ATN.

Na shaba (Bronze sponsors) ni MOROBEST, Simba Oil, Afro Oil, OnAfrica Construction, KCB Bank na taasisi ya Education and Research Academy (IERA) ya nchini Uingereza.

Tunasema kazi waliyoifanya wadhamini hao ni kubwa kwani wamewezesha kongamano kung’ara. Mwisho, tunaupongeza uongozi wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) kwa kuandaa kongamano hilo lenye tija

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close