2. Ncha ya Kalamu

Achana na Biashara Haramu Zitakupeleka Motoni

Ni kazi ngumu mno kumshawishi Muislamu wa kawaida kuacha kufanya kazi au biashara ambayo inakwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu. Hali hii inachangiwa na jamii kutawaliwa na mfumo wa maisha ya kibepari unaotajwa kuingilia mambo muhimu ya msingi katika maisha ya mwanadamu.

Pamoja na ugumu waliojivika Waislamu katika harakati za kuyaendea maisha yao katika kuchunga mipaka ya maagizo ya Allah Ta’ala na kanuni zake, bado Allah Ta’ala amewaharamishia Waislamu baadhi ya kazi ambazo kimsingi huwapelekea kupata madhambi.

Si hivyo tu, pia Uislamu umewakataza waumini wake kushiriki katika kueneza mambo ya haramu sanjari na kujifunza taaluma zinazoonekana kuleta madhara katika itikadi, maadili na heshima ya dini yao.

Kwa tafsiri fupi, naweza kusema, kazi halali ni ile iliyoelekezwa katika kutengeneza au kufanya kitu, biashara, utaalamu, au ufahamu ambao kwa ujumla wake, Uislamu umeifanya kama sehemu ya amali inayomsaidia mja kuvuna thawabu kwa ajili ya maisha ya Akhera.

Allah Ta’ala anasema: “Na tafuta katika yale aliyokupa Mwenyezi Mungu, makazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la Dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia wema. Wala usifanye ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.” [Qur’an, 28:77].

Moja katika hoja za watu wanaoishi kwa kutegemea chumo la haramu na kudhulumu katika kuendesha maisha yao ni kwamba Mwenyezi Mungu ndivyo alivyowajaalia. Hata hivyo, Menyezi Mungu amekanusha madai hayo.

Mwenyezi Mungu anasema: “Mfano wa waliobebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.” [Qur’an, 62:5].

Licha ya Uislamu kubainisha mambo yote haramu na halali, baadhi yetu tumekuwa tukibuni taswira chanya katika kuhalalisha chumo lililotokana na kazi/ biashara haramu.

Mfano wa chumo litokanalo na haramu ni mtu kufanya kazi katika taasisi za riba na kamari, viwanda vya pombe, kupunja katika vipimo, kumhadaa mnunuzi kwa viapo vya uongo, kudhulumu, kutapeli au kughushi, kuuza vinyago, masanamu, nyama ya nguruwe, kufanya kazi ya ukahaba, kupiga ramli, kuimba/ kucheza au kupiga ala za muziki, na kadhalika.

Licha ya Uislamu kuharamisha biashara hizi, bado Waislamu wengi wanashikilia misimamo ya kuendelea na kadhia hizi kwa hoja zisizo na maana ikiwamo kubuniwa fursa ya kile kinachoitwa ‘Kufunguliwa Dunia’.

Uhuru huu usiojali mipaka ya dini umekuwa kichocheo kikubwa kwa baadhi yetu kutimiza malengo huku tukidhani kuwa ndio ustaarabu, usasa na kwenda na wakati.

Allah Mtukufu anatuambia: “Na aminini niliyoyateremsha ambayo yanasadikisha mliyonayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze ishara zangu kwa thamani ndogo. Na niogopeni mimi tu, wala msichanganye kweli na uongo na mkaificha kweli hali ya kuwa mnajua.” [Qur’an, 2:41–42].

Kwa hakika, tumeshuhudia athari nyingi mbaya katika nchi za magharibi ambazo kuna idadi kubwa ya Waislamu waliohamia huko kuendesha maisha yao.

Waislamu wanaoishi katika nchi hizo ni wazi kuwa wanakosa uhuru wa kutekeleza masharti ya dini yao vile inavyotakiwa. Hii ni sawa na mtu kujidhulumu nafsi.

Ni vema Waislamu wakaelekea kule kilipo Qibla kila wakati wanapotaka kuendesha harakati zao za kimaisha, kwani hakuna shaka kwamba kuikumbatia dhuluma ni sawa na kulikimbia jivu huku wakisahau kama wanaelekea kutumbukia kwenye moto.

Kutumia hila ili kuhalalisha yaliyoharamishwa

Haifai na ni haramu kwa Muislamu kufanya hila na udanganyifu ili kuhalalisha mambo ya haramu. Miongoni mwa hila chafu zinazotumiwa na maadui wa Uislamu ni kubuni taswira chanya katika kuhalalisha huduma na bidhaa haramu.

Miongoni mwa mifano hai ni ile ya wazinifu kuitwa wapenzi, kumbi za kufanyia maasi kupewa jina la kumbi za starehe, walevi wa pombe kuitwa wanywaji, kamari kuitwa bahati nasibu na riba kubadilishwa jina na kuitwa faida.

Haya yote yalitabiriwa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliposema: “Zitakuja zama katika umma wangu watu watahalalisha zinaa na kuvaa hariri na kutumia khamri (vileo) na ala za muziki.” [Bukhari].

Wale wote wanaokula chumo la haramu watambue kuwa wanaandikiwa madhambi, na Siku ya Kiyama watapata adhabu kali.

Ikiwa mtu amechuma mali kwa njia ya haramu kisha akaitumia katika kujenga msikiti au kufanya jambo lolote la kheri, amali yake hiyo haitokubaliwa kwa mujibu wa kauli ya Mtume isemayo:

“Allah ni Mzuri  hakubali ila kilicho kizuri.” [Muslim].  

Na katika riwaya iliyosimuliwa na Abdullah bin Masu’ud (Allah amaridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema, yeyote atakayeacha mali ya haramu, baada ya kufa mali hiyo itakuwa akiba yake ya kumpeleka motoni, [Bukhari].

Hii ni kwa sababu, Allah Aliyetukuka hafuti baya kwa baya bali hufuta baya kwa zuri. Kwa kuzingatia hadith hizo mbili, ipo haja ya kutambua kuwa siku moja tutasimama mbele ya Allah Ta’ala na atatuhukumu kwa uadilifu juu ya yale tuliyoyatenda.

Wanadamu hususan Waislamu tunatakiwa tujitahidi kutafuta riziki kwa mujibu wa muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie). Huo ndio msimamo wa Muislamu anayekubali kwamba riziki iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Allah anasema kuhusu riziki: “Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa njia asiyoitarajia. Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake.” [Qur’an, 65:2–3].

“Na hakuna mnyama yeyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha.” [Qur’an, 11:6].

Kwa sababu hiyo, tunapaswa kutafuta riziki kwa mujibu wa muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie).

Muislamu anatakiwa kufanya kazi ya halali ili kujipatia riziki kwa kuchunga mipaka aliyoiweka Mwenyezi Mungu. Kulingana na aya za hapo juu, Muislamu anatakiwa atafute kipato kwa njia za halali kwa sababu kilicho haramu kwa mtu binafsi, pia ni haramu kwa familia na jamii nzima. Uislamu umeweka utaratibu maalumu wa kutafuta kipato, ambapo kila mtu anao uhuru wa kuzalisha mali ya kutosha kukidhi mahitaji yake binafsi na familia. Hii ni kwa sababu, Uislamu una mfumo wake wa kiuchumi uliokamilika, ambapo kila Muislamu anawajibika kuchuma kulingana na mfumo huo

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close