4. Jamii

Mfumo wa madrasa haukidhi changamoto za sasa

Uwepo wa madrasa katika jamii ya Waislamu ni jambo muhimu sana kwa sababu ni kupitia taasisi hizi, watoto hupata fursa ya kuijua dini yao na pia viongozi wa baadaye wa kidini huanza kuandaliwa. Kwa muda wote, tangu Uislamu uingie Afrika ya Mashariki, madrasa zetu zimetoa wanafunzi wengi ambao walikuja kuwa masheikh wakubwa katika zama zao.

Licha ya mafanikio hayo, bado wahitimu wengi wa madrasa zetu wanahitimu wakiwa hawajui hata mambo ya msingi kuhusu Uislamu wao kwa kiwango cha kuwawezesha kuishi maisha ya uchamungu. Hii ni kwa sababu, madrasa nyingi zimekosa mfumo maalum wa ufundishaji, bali kila mwalimu anaendesha chuo chake aonavyotaka yeye.

Madrasa zetu, hasa zile za ngazi ya chini kabisa, hazina mitaala ya masomo, vitabu na hata majaribio na mitihani. Kadhalika, kuna upungufu mkubwa katika upimaji wa maendeleo ya mwanafunzi. Siyo jambo la ajabu kusikia mtoto wa fulani amehitimu Msahafu lakini ukimpa kitabu kingine asome atakwambia sijafundishwa.

Maana yake ni kwamba mfumo wa ufundishaji haulengi kumfanya mwanafunzi asomaye madrasa kuelewa masomo anayofundishwa bali hukaririshwa tu na wakati mwingine kwa kuchapwa viboko. Hali hii ndivyo ilivyo katika madrasa zetu nyingi ambapo madrasa yenye wanafunzi 120 unaweza ukakuta mwalimu ni mmoja akimfundisha kila mwanafunzi sura aliyofika kiasi kwamba kuna wengine humaliza siku pasina kufundishwa kwani hatimaye mwalimu huchoka.

Changamoto zinazokabili madrasa

Changamoto za madrasa zetu ni nyingi sana lakini kwa uzoefu ulioelezwa na masheikh, walimu wa madrasa, wazazi/walezi na wanafunzi changamoto kubwa ni pamoja na Mosi, mfumo wa kusomesha kwa kukaririsha badala ya kuelimisha.

Mwanafunzi hukaririshwa tu kama kasuku herufi za Kirabu na kisha kuanza kusoma kuanzia Suratul Faatiha (alhamdu). Matokeo ya mfumo huu, kwanza mtoto huchukua muda mrefu kuweza kumudu kusoma kwa kukariri na pili kwa kuwa anakuwa amekariri, asipojenga tabia ya kurudiarudia kusoma baada ya muda husahau yote aliyoyakariri. Kwa sababu hiyo, sio ajabu kumkuta mtu aliyekuwa amehitimu kusoma Qur’an juzuu ‘Amma au hata msahafu akiwa ameshasahau kusoma. Wahitimu kama hawa wa madrasa ndiyo wengi katika jamii yetu.

Pili, ukosefu wa mitaala na mihutasari ya masomo (curriculum) na silabasi (Syllabus) iliyoandaliwa kitaaluma kwa mujibu wa mazingira, hali za wanafunzi na zama tulizonazo ni tatizo jingine sugu kwa madrasa zetu. Matokeo ya hali hii, masomo yanayofundishwa katika madrasa zetu ni uamuzi wa mwalimu wa madrasa husika.

Hakuna hatua za ukuaji kielimu katika madarasa zetu kulingana na umri. Haijulikani haswa hata wanafunzi wa madrasa hutakiwa kuanza madrasa wakiwa na umri gani na huhitimu hatua gani ya masomo wanapomaliza madrasa na je, hupewa vyeti vya uhitimu? Jibu ni kwamba hakuna masharti ya umri wa kuanza madrasa.

Mtoto akiweza kutembea na kusema hupelekwa madrasa jambo ambalo huzifanya madrasa kama vituo vya kulelea watoto wadogo (day care centre). Anayeambiwa amemaliza madrasa haijulikani amemaliza hatua gani na hakuna vyeti au shahada za kumaliza madrasa tofauti na madrasa za zama za kale ambapo wanafunzi walipewa ijaaza na kuvikwa majoho ya kiilmu! Kwa utaratibu huu, huwezi kumhamisha mtoto kutoka madrasa moja kwenda nyingine na akaendelea na masomo aliyokuwa akiyasoma madrasa alikotoka kama ilivyo kwa shule za msingi au sekondari.

Tatu, kukosekana kwa vitabu maalum vya kutumika katika madrasa zetu ni changamoto nyingine ambayo inatokana na kukosekana kwa mtaala (curriculum) mmoja na silabasi moja. Madrasa hazina sio tu vitabu vya kiada bali hata vya ziada. Hata miongozo kwa walimu pia walimu.

Ni kweli kuna baadhi ya vitabu vya awali vya fik-hi kama vile Irshadul Muslimiina, Hidaayatul Atfaal, Safiinat Swalaat, Safiinat Najaa na Rub’ul Ibaada au Matinul Ghaayah. Vitabu hivi vinafundishwa kwa wanafunzi walioinukia kidogo baada ya kuhitimu mas-hafu lakini mamilioni ya wanafunzi wanaopitia madrasa zetu na wasiendelee kusoma elimu ya madrasa hawapati bahati ya kusoma hata vitabu hivi. Na hata ufundishaji wa vitabu hivi ni jambo la ada tu na siyo mfumo rasmi uliorasimishwa kutokana na ukweli kwamba hakuna walimu wa kutosha wenye viwango vya kutosha maana wanahitajika kujua lugha ya Kiarabu.

Nne, pia kuna changamoto ya kutokuwa na mihula na ratiba za masomo hivyo zinanyang’anyana wanafunzi na shule za msingi na sekondari/vyuo. Wakati wanafunzi wakiwa katika mihula ya shule za msingi na sekondari, madrasa zetu hubakia na muda wa masomo kwa wanafunzi jioni tu au wakati mwingine usiku baada ya Magharibi.

Baadhi ya wanafunzi wa zamani wanakumbuka walivyosoma madrasa nyakati za baina ya Magharibi na Isha, wakati mwingine hadi saa nne za usiku tena kwa chemli au hata vibatari; na kuanzia asubuhi hadi saa kumi na nusu Alasiri walikuwa shuleni. Bahati mbaya kwa watoto wa zama hizi kuna mpango wa masomo ya ziada (tuition) kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari yanayofundishwa baada ya kurudi kutoka shule au huko huko shuleni, kiasi kwamba madrasa zimebakia na watoto wa umri wa chekechea ambao hawajaanza kwenda shule za msingi.

Tano, ni changamoto ya ukosefu au upungufu wa miundo mbinu. Kwa sababu jamii za Waislamu zama zimeipa kipaumbele masomo ya kisekula, miundo mbinu katika madrasa zetu aidha haipo kabisa au ina upungufu mkubwa. Ni madrasa chache zenye majengo ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi, nyingi zikiendeshwa katika misikiti katika nyakati zisizo za Swala za jamaa. Hakuna madarasa, ofisi wala maktaba kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kujisomea.

Picha za kinachoitwa majengo ya madraza hasa za vijijini ni za kusikitisha sana maana ni vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi au makuti ya minazi huku wanafunzi wakikaa chini katika mikeka au hata ardhini kabisa. Sambamba na hilo, hakuna mavazi rasmi ya madrasa.

Huko vijijini, kipindi cha mvua au mavuno madrasa hufungwa ili wanafunzi wakawasaidie wazazi kazi mashambani.

Sita, walimu hawana mafunzo ya kutosha, ambapo mtu yeyote aliyesoma kiwango chochote kile cha elimu ya dini anaweza kuanzisha madrasa yake au kupewa kazi ualimu. Hata hivyo, hivi karibuni baadhi ya taasisi, kama vile Hay-atul Ulamaa, Basuta, Kalamu Education Foundation (KEF), zimejitahidi kutoa mafunzo kwa walimu wa madrasa na maimamu wa misikiti kuwapa mbinu za ufundishaji na uongozi.

Wakati tukizipongeza taasisi hizi, tunapenda kuzitanabahisha kwamba kama changamoto za mitaala, silabasi na vitabu hazitatatuliwa, mafunzo hayo ya ualimu hayatozaa matunda tarajiwa. Umefika wakati taasisi zianzishe vyuo ili kuwaandaa walimu wa madrasa watakaozibadili madrasa ziendane na mahitajio ya zama hizi.

Saba, ni changamoto ya idadi ya walimu hususan katika ngazi za chini ambapo utakuta mwalimu mmoja anafundisha watoto wa umri na viwango tofauti hadi inakuwa zogo kubwa, kila mtoto akisoma kwa sauti sura aliyofikia.

Kama tunataka madrasa zetu ziwe na tija ni lazima ziwe na walimu kulingana na idadi ya masomo yatakayopangwa kufundishwa kwa mujibu wa mtaala. Hapo ndipo umuhimu wa kujenga madarasa, ofisi za walimu, nyumba za walimu na maktaba utakapoonekana, sambamba na kuwa na vitabu vya kiada na ziada vinavyoendana na hatua za ukuaji wa mwanafunzi.

Nane, changamoto nyingine ni kukosekana kwa mazoezi, majaribio na mitihani. Hii inatokana na kukosekana kwa silabasi, miongozo na vitabu vya kiada na ziada, hivyo mwalimu anakosa miongozo ya namna ya kuwapa wanafunzi kazi za kufanya nyumbani (home work), majaribio na mitihani. Hii inaleta ugumu katika kupima uelewa wa wanafunzi.

Siku hizi walimu wa madrasa wamebuni utaratibu wa maonesho au matamasha ya masomo ambapo huwaita wazazi na wanafunzi kufanya maonesho ya walichokisoma ambacho kimsingi ni mambo waliyokaririshwa kwa lengo la kukonga nyoyo za wazazi tu hata kama hayana manufaa kielimu kwa wanafunzi husika.

Tisa, changamoto nyingine ni wazazi na walezi kutokulipa ada. Madrasa hazina fungu maalumu la bajeti hivyo hutegemea michango ya wazazi/walezi ya ada kwa ajili ya watoto wao. Hata hivyo, wazazi wengi hawawalipii watoto wao ada ya madrasa ambayo haizidi elfu kumi kwa mwezi katika madrasa nyingi.

Wazazi wako tayari kuwalipia pesa nyingi katika shule za kisekula, lakini kwa madrasa ni bora mtoto akae nyumbani. Zama zilizotangulia, mwalimu hakuachiwa akusanye ada ya wanafunzi wa madrasa bali madrasa ziliendeshwa kwa Waqf uliotolewa na wenye uwezo na wapenda kheri na mapato yake kuhudumia madrasa.

Umefika wakati turejeshe mfumo huu. Athari ya jumla ya hali hii, ni madrasa zetu kuwa butu. Haziwezi kutoa elimu itakayowawezesha watoto kwenda na changamoto za zama hizi kama masuala ya watu kuabudia dunia, maasi mbali mbali na uharibifu wa kimaadili.

Historia ya mfumo wa madrasa

Madrasa ya kwanza katika Uislamu ni ile iliyoanzishwa na Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) katika nyumba ya Zaid bin Arqam karibu na kilima cha Swafah pale Makka mwalimu akiwa ni Mtume mwenyewe na wanafunzi wakiwa ni Maswahaba wake (Allah awaridhie).

Baada ya Mtume na Maswahaba kuhamia Madina, Mtume alianzisha vikao vya kimadrasa kwenye msikiti wa Madina. Mtume ‘Ubaadah bin Swaamit (Allah amridhie) kuwa mwalimu katika madrasa hii na wakati mwingine yeye mwenyewe Mtume akifundisha.

Masomo yaliyofundishwa ni pamoja na Qur’an, Hadithi, Faraaidh (mirathi), elimu ya nasaba, kusoma na kuandika, huduma ya kwanza, mazoezi ya kupanda farasi, kupiga mishale nk. Mfumo huu uliendelea na ukapanuka zaidi kutoka zama za Mtume hadi kufikia zama za utawala wa Banii Umayyah pakawa na madrasa nyingi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Mwaka 859, chuo kikuu cha kwanza cha Kiislamu kikaanzishwa katika mji wa Fas nchini Morocco. Chuo kikuu hiki kinait- wa Jaamiat Al-Qarawiyyiin kwa kuwa kilianzishwa katika msikiti uitwao Masjid Al-Qarawiyyiin. Chuo hiki kilianzishwa na binti wa mfanyabiashara tajiri Muhammad Al-Fihri aitwaye Fatmah Muhammad Al-Fihri.Baadaye ndiyo kikaanzishwa chuo kikuu cha Al-Azhar mjini Cairo nchini misri mnamo mwaka 959.

Kipindi cha mwisho wa utawala wa Banii Abbas, waziri wake Mturuki aliyeitwa Nizaam Al-Mulk alianzisha madrasa rasmi zilizosimamiwa na dola (mfano wa shule za msingi na sekondari) zikiitwa Madrasat An-Nidhwaamiyyah katika dola nzima ya Banuu Abbas. Katika historia ya Uislamu, madrasa zilitoa wahitimu walioinua hadhi na heshima ya Uislamu katika elimu ya dini na maendeleo ya  dunia kupitia uvumbuzi mbali mbali wa kisayansi na kiteknolojia. Akina Ibn Nafiis, Ibn Al-Haytham, Jaabir bin Hayyaani na wengine walitoka katika mfumo madhubuti wa madrasa.

Leo moja ya matunda ya madrasa zetu ni waimba taarabu na wasanii wa kizazi kipya kulikoni? Tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa kuhusu madrasa zetu kama tunataka ziweze kukabiliana na changamoto zinazoukabili umma.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close