4. Jamii

Matumizi ya simu na mitandao ya kijamii na changamoto ya malezi

Toka azali simu ni miongoni mwa chombo muhimu cha mawasiliano. Watu wamekuwa wakipashana habari kupitia simu. Ukitembea maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kuona namna chombo hiki kilivyoenea utakubaliana na mimi kuwa simu ni l chombo muhimu sana kwa maisha ya kileo.

Watu wanawasiliana bwana!! Simu zimevunja mipaka ya kimasafa na  kuwaleta watu pamoja. Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia kuenea kwa simu za kisasa ziitwazo simu janja (smart phone) ambazo sio tu zimenogesha sekta ya mawasiliano, bali pia zimeongeza wigo mkubwa wa mawasiliano na kuibua fursa na changamoto nyingi katika jamii.

Kupitia simu hizi na vifaa vingine vya kielektroniki, tumeshuhudia kushamiri kwa mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApp.

Nakiri kuwa mitandao hii inazo fursa nyingi (panapo uhai kuna siku tutaizungumzia). Hata hivyo, kukithiri kwa matumizi ya simu hasa smart phone na mitandao ya kijamii kumeibua pia  changamoto nyingi katika malezi ya watoto wetu.

Watu wengi tumekuwa tukitumia muda wetu mwingi katika mitandao ya kijamii na hatuna muda wa kutosha kufanya mambo ya kifamilia. Hapa tunazungumzia kukithiri kwa makundi sogozi hasa katika WhatsApp na mitandao mingine.

Mama au baba akirudi nyumbani hana muda kabisa hata wa kuongea na watoto bali huo na ni muda muafaka wa kuingia katika mitandao ili kuchangia mada katika makundi. Wazazi na walezi, wekeni simu chini na simamieni malezi.Mzazi huna muda hata wa kukagua madaftari ya mtoto? Je, akiharibika lawama tumpe mwalimu au wewe?

Pia, mitandao ya kijamii imetumika sana kusambaza picha chafu na taarifa nyingine zisizo na maadili. Ukiingia mitandao kama Instagram na Facebook  utashangaa kuona vijana wadogo wanavyofanya mambo ya ajabu na kuyatuma katika mitandao bila woga.Nadhani, wao wanaona kuwa njia hii ni sahihi kwa kujipatia wafuasi (followers)  au kujiongezea umaarufu.

Swali la kujiuliza, wapo wapi wazazi, ndugu na jamaa wa hawa watoto?Mitandao ya kijamii imetumika sana kuchafua watu na kusambaza taarifa za  uongo. Watoto wetu wanaona na kusikia taarifa chafu kupitia mitandao hii kuhusu baba zao, mama zao au ndugu wengine wa karibu. Kwa namna yoyote iwavyo, taarifa hizi hazikustahili kuwafikia watoto.

Aidha, taarifa hizi hazikupaswa kabisa kuwa za wazi kiasi hiki. Pia, jambo hili  linakatazwa sana katika dini yetu tukufu ya Kiislamu. Dini inahimiza sana kulinda heshima za watu wengine. Iweje leo kila kitu kinaanikwa uwanjani?

Vilevile, wapo watu wengi wanaotumia mitandao hii kuwadhihaki na kuwadhalilisha watoto. Wapo wanaofanya kwa makusudi na wapo wengi wanaofanya hili kwa kutojua. Tumeona na kusikia watu wengi wakiposti picha au video za watoto na kuweka maneno ya kuchekesha. Watu wengi huwarekodi watoto wanaposhindwa kufanya/kuelezea jambo fulani kwa ufasaha na kulirusha mitandaoni. Haya ni matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Picha za namna hii hupata umaarufu mkubwa na hurushwa huku na huko. Kwangu mimi, hii dalili mbaya tunapozungumzia malezi ya watoto. Jamii inahalalisha udhalilishaji wa mtoto na kumfanya kituko katika mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii imetumika sana kuchafua watu na kusambaza taarifa za uongo. Watoto wetu wanaona na kusikia taarifa chafu kupitia mitandao hii kuhusu baba zao, mama zao au ndugu wengine wa karibu

Aidha, mitandao ya kijamii imeharibu faragha za kifamilia. Wapo watu kutokana na ‘ushamba’ wamekuwa
wakiyaanika mambo yao yote ya kifamilia katika mitandao. Akiamka asubuhi ataposti picha ‘tunapata chai
ya nguvu hapa na familia’…mchana ataandika ‘tupo hotel…tunakula nyama choma’, usiku hivyohivyo.

Swali la muhimu hapa ni je, kuna haja gani ya kuanika mambo ya familia yako  mitandaoni? Hatari iliyopo ni kuwa, picha hizihizi hutumika wakati mwingine na watu wabaya kuvumisha  taarifa za uongo zinazohusiana na familia hizi.

Sikatai kuwa yapo mambo yanayoweza kurushwa mitandaoni kwa malengo mbalimbali, hata hivyo ni muhimu kuhifadhi faragha za kifamilia kwa ustawi wetu na watoto wetu. Tunatoa pongezi kwa serikali na wadau wote  wanaosimamia nidhamu katika matumizi ya simu na mitandao ya kijamii. Wazazi wenzangu, tutumieni simu na mitandao ya kijamii kwa uangalifu, vinginevyo tusubiri maafa na majanga katika jamii yetu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close