2. Ncha ya Kalamu4. Jamii

Mapatano ya Sudan: matumaini na changamoto

Tarehe 21 Agosti mwaka 2019 itaingia katika historia ya Sudan kama siku ambayo taifa hilo liliingia katika mapatano ya kudumu ya amani kati ya pande mbili zilizokuwa zikihasimiana.

Kufuatia maandamano ya amani ya wananchi ya mfululizo kwa miezi takriban minne wakipinga utawala wa rais aliyeondolewa madarakani Omar Al-Bashir, zilizuka pande mbili zinazohasimiana. Pande hizo ni Baraza la Uongozi la Kijeshi lililoshika hatamu baada ya kupinduliwa kwa Omar Al-Bashir na upande wa pili ni harakati za wananchi za kupinga baraza hilo.

Kuundwa kwa Baraza la Utawala ambalo litadumu kwa muda wa miezi 39 likiongozwa na Jenerali Abdel Fatah Al Burhan ambaye ataongoza nchi kwa muda wa miezi 21 na kufuatiwa na kiongozi wa kiraia, ni hatua muhimu zaidi katika siasa za Sudan. Abdalla Hamdok, mchumi mwenye uzoefu wa masuala ya kiuchumi kimataifa, aliapishwa kama Waziri Mkuu wa Baraza hilo la Utawala la Sudan.

Matumaini ya wananchi

Wananchi wa kawaida wa Sudan walijawa na matumaini makubwa kwa kutiwa saini mapatano ya amani tarehe 17 Agosti na kuundwa kwa Baraza la Utawala la taifa tarehe 21 Agosti.

Matumaini haya yanatokana na ukweli kwamba, haya ni mapatano yaliyohitimisha miaka takriban 29 ya utawala Rais Omar Al-Bashir uliokuwa ukilalamikiwa kwa kuitia Sudan katika hali ngumu ya uchumi, misukosuko ya kisiasa sambamba na kukosekana kwa amani na utulivu.

Katika kipindi hicho, ramani ya Sudan iliyokuwa nchi ya pili kwa ukubwa wa eneo barani Afrika ikiifuatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilibadilika baada ya kujitenga kwa eneo la Kusini lenye utajiri mkubwa wa mafuta na kuundwa kwa taifa la Sudan ya Kusini mwaka 2011.

Kwa hiyo kutiwa saini kwa mapatano ya amani na hatimaye kuundwa kwa Baraza la Utawala la Taifa linalojumuisha wanajeshi na raia wa nchi hiyo ni hatua chanya iliyofurahiwa na wananchi wengi na hata jumuiya za kimataifa. Matumaini ya wengi ni kuiona Sudan ikirejea katika jukwaa la kimataifa kwa kuwa uanachama wake katika Umoja wa Afrika (AU) ulisimamishwa.

Aidha, mashirika mengi ya kimataifa, likiwemo Umoja wa Mataifa (UN), yalilipa taifa hilo kisogo baada ya mauaji ya raia waandamanaji yanayoaminika kufanywa na kikosi kijulikanancho kama Rapid Response Force (RRF), ambacho kinaundwa na waliokuwa wanamgambo wa Darfur maarufu kama Janjaweed. Kikosi hiki kimetuhumiwa kufanya mauaji mengi, na kinahofiwa mno na wanannchi wa Sudan.

Kwa maendeleo haya makubwa ya kisiasa yaliyopatikana nchini Sudan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, aliipongeza Sudan kwa mweleko mpya iliyouchukua baada ya kuapishwa kwa Baraza la Utawala.

CHANGAMOTI ZINAZOLIKABILI BARAZA

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa; bado Sudan, moja ya mataifa kongwe Afrika, inakabiliwa na changamoto lukuki.

Uchumi wa Sudan

Waswahili wanasema “Mwiba unapoingilia ndipo unakotokea.” Chanzo cha maandamano yaliyomtoa madarakani Rais Al-Bashir wa Sudan ni hali ngumu ya uchumi ikiwemo kupanda kwa bei ya mikate ambacho ndiyo chakula kikuu cha Wasudan.

Kwa hiyo, kuurejesha uchumi wa Sudan katika hali nzuri ndiyo changamoto kubwa ya kwanza kwa Baraza la Utawala la Sudan kwa sababu watu wenye njaa hawawezi kujali amani wala usalama.

Kuteuliwa Abdalla Hamdok kama Waziri Mkuu wa Baraza la Utawala ni dalili tosha kuwa wajumbe wa Baraza hilo wanaielewa fika changamoto hii na wameazimia kuishughulikia.

Dkt Hamdok amepata kufanya kazi katika taasisi ya Umoja wa Mataifa (UN) inayoshughulikia uchumi barani Afrika na ni mchumi mwenye uzoefu mkubwa kimataifa. Dkt Hamdok anategemewa kuongoza jitihada za kuukwamua uchumi wa Sudan kutoka ulikokwama na kujenga imani ya Wasudan kwa serikali hiyo ya mpito.

Ikumbukwe kwamba uchumi wa Sudan ilikuwa ukitegemea mafuta ambayo asilimia 80 yalikuwa katika eneo la Kusini mwa nchi hiyo. Sudan ya Kusini ilipojitenga nchi hiyo ilipata pigo kubwa kiuchumi.

Kwa sasa, uchumi wa Sudan unategemea zaidi ushuru wa kusafirisha mafuta ya Sudan ya Kusini kupitia bandari yake ya Port Sudan na shughuli za kilimo kwa kiasi kidogo utalii.

Usalama na amani

Suala la amani na usalama ni changamoto nyingine kubwa. Kimsingi bado jimbo la Darfur kuna machafuko na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) wako huko Darfur wakiwemo wanajeshi wa Tanzania.

Mpakani mwa nchi hiyo na Sudan ya Kusini katika jimbo la Kordofan nako kuna machafuko, ambako wanamgambo waasi wanapigana dhidi ya jeshi, ingawa kwa sehemu kubwa wamedhibitiwa.Maelewano yaliyoko kati ya Sudan mbili – Sudan an Sudan ya Kusini yamechangia sana kupungua kwa mapigano katika jimbo hilo tajiri kwa mafuta.

Kwa wananchi wa kawaida wa Sudan, watakwambia hofu yao kubwa ni wale wanamgambo wa kikosi kijulikanacho kama RRF kilicho chini ya Jenerali Dagalo, ambaye yuko katika Baraza la Utawala. Wananchi wamefikia hata kupinga uwepo wa Jenerali Dagalo katika Baraza hilo kutokana na historia ya kikosi hicho ambacho kimehusishwa na utekaji nyara watu na hata mauaji ya wanasiasa na wapinzani wa jeshi.

Kwa hiyo, Baraza la Utawala lina kazi kubwa kuhakikisha amani na usalama vinatamalaki nchini Sudan. Iwapo hili halitafanikiwa sambamba na lile ka kurekebisha uchumi, basi kuna uwezekano mkubwa wa Baraza hilo kushindwa.

Hofu ya historia kujirudia

Hii siyo mara ya kwanza nchini Sudan wananchi kuandamana na kusababisha jeshi kumuondoa madarakani mwanajeshi mwenzao. Miaka 29 iliyopita, wananchi wa Sudan wakiongozwa na mwanasiasa aliyekuwa na mvuto mkubwa kwa Wasudan Dkt Hassan Al-Turabi, waliandamana na kusabaibisha Rais Jaafa Nimeiri kuondolewa madarakani.

Nimeiri alipoondoka madarakani alirithiwa na Omar Al-Bashir, ambaye ndiye huyu aliyetimuliwa tena kwa staili ile ile aliyoitumia kumwondoa madarakani mtangulizi wake.

Omar Al-Bashir mwazo aliungwa mkono na raia, lakini baada ya vumbi la kumuondoa madarakani Nimeiri kutulia, aliwageuka raia waliomuunga mkono na kuamua kung’ang’ania madaraka na kukataa kurejesha utawala wa kiraia.

Wananchi wengi wa Sudan wanafuatilia kwa makini yanayotokea hivi sasa nchini Sudan kwani yalikwishawahi kutokea kama haya na wanajeshi wakafanya hiyana.

Watu wanajiuliza, je safari hii wanajeshi wataheshimu mapatano yaliyofikiwa ya kufanyika uchaguzi na kuunda serikali ya kiraia au watafuata nyayo za wenzao waliowatangulia? Bado ni mapema kupata jibu la swali hili. Itabidi kusubiri miezi 21 ya zamu ya wanajeshi kuongoza Baraza la Utawala imalizike kisha tuone nini kitatokea katika kipindi cha zamu ya raia kutawala.

Hatimaye picha kamili itapatikana iwapo uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2023 utafanyika na kama utakuwa kweli uchaguzi huru na wa haki kwa wote.

ICC na Omar Al-Bashir

Changamoto nyingine ni kuweko hati ya kukamatwa Omar Al-Bashir iliyotolewa na Mahakama ya Jinai ya KImataifa (ICC) kule The hegue, Uholanzi. Al-Bashir anatuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari kule Darfur na anashtakiwa kwa kufanya ukatili dhidi ya binadamu.

Akiwa madarakani, Omar alifaulu kukwepa kukamatwa kwa sababu nchi nyingi ziliiheshimu nafasi yake kama rais wa nchi ya Sudan, lakini kwa kuondolewa madarakani ICC sasa inaitaka Baraza la Utawala kumkabidhi Al-Bashir ili mashitaka dhidi yake yapate kusikilizwa. Swali la msingi ni je, Baraza la Utawala lenye wajumbe 11, watano wanajeshi na sita raia litakubali kumkabidhi Al-Bashir ICC?

Changamoto hizi na nyingine za ndani ya Sudan zinalikabili Baraza la Utawala lililopewa miezi 39 tu kuiweka Sudan katika hali nzuri kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kidiplomasia.

Iwapo Baraza hili litafanikiwa litakuwa limejiandikia historia nzuri na litalikuwa Baraza la mfano wa kuigwa katika utatuzi wa migogoro ya ndani barani Afrika hasa inayohusisha wanajeshi na raia; lakini Iwapo litashindwa, litakuwa limezima ndoto za mamilioni ya raia wa Sudan kujionea nchi yao ikishamiri kiuchumi, kisiasa, kiusalama na uhusiano wa kimataifa.

Na kwa hali ilivyo tete, wananchi wameshaonya kuwa, kama mambo hayatabadilika, basi wembe ni ule ule, mapambano yao kwa njia ya maandamano yataendelea.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close