malezi

Zawadi huimarisha mapenzi kwa watoto

Utoaji wa zawadi ni kitu kinachowafurahisha sana watoto. Mara nyingi, zawadi hulenga kuimarisha matendo chanya ya mtoto. Baadhi ya mambo ambayo huweza kumfanya mzazi kutoa zawadi ni pamoja na matokeo mazuri ya shuleni au madrasa.

Kuna aina nyingi sana za zawadi.
Zipo zawadi kubwa. Hizi ni zile zenye thamani kubwa kama vile magari, pikipiki, nyumba, viwanja n.k. Kwa hakika hizi ni zawadi nzuri, lakini siyo muafaka sana kwa watoto. Pia, kuna zawadi ndogo. Hizi ni zile zenye thamani ndogo kama vile nguo, vyakula [biskuti, pipi na chipsi], viatabu, rangi za kuchorea, kalamu, madaftari na viatu. Zawadi hizi, hupendwa sana na watoto na zinafaa sana katika kushajiisha matendo chanya ya watoto.

Pia, zawadi zinaweza kuwa katika mfumo wa matembezi, mafupi au marefu. Muhimu ni kuwa, yanapaswa kulenga kutoa furaha na starehe kwa watoto. Matembezi yanaweza kuwa katika mbuga za wanyama, maeneo ya kihistoria, safari za nje ya nchi n.k.


Mzazi, fahamu kuwa, zawadi inayotoka moyoni hata kama umeichuma porini au umeinunua kwa shilingi mia ina maana kubwa sana kwa mwanao

Mbali ya zawadi kutumika kama chachu ya kuimarisha matendo chanya, pia huweza hutolewa kama sehemu ya kushajiisha nidhamu kwa watoto. Hii ni kusema kuwa, mzazi unaweza kumpa mtoto zawadi kama sehemu ya kufurahia matendo mazuri ya mtoto. Kwa sehemu kubwa, zawadi zikitumika vizuri hujenga daraja baina ya mzazi na mtoto.

Pia, husaidia kutoa msukomo chanya kwa watoto wengine kwani watoto mara nyingi hupenda ushindani. Watoto wakiona mwenzao kapata zawadi, ni wazi kuwa nao watajituma ili mara nyingine nao wapate zawadi. Tanbihi muhimu kwa wazazi ni kuwa, zawadi hutolewa kwa lengo maalumu.

Pia, ni muhimu kwa wazazi kutumia zawadi kwa umakini mkubwa. Itakuwa ni makosa makubwa kuwajengea watoto dhana na mategemeo kuwa, kila atakachokifanya vizuri basi anastahiki kupata zawadi. Lahasha!!! Hii siyo sawa. Aidha, zipo kanuni muhimu ambazo mzazi unapaswa kuzingatia ili kuifanya zawadi yako iwe na manufaa kwa mtoto. Hapa tutataja baadhi ya kanuni hizo.

Sababu maalumu
Zawadi itolewe kwa sababu maalumu. Ni muhimu kufahamu kuwa siyo kila jambo zuri analofanya mtoto linapaswa kufuatiwa na zawadi. Jenga utamaduni wa kutoa zawadi katika matendo muhimu. Hali hii humjenga mtoto kujituma kila wakati bila kutegemea msukumo wa zawadi.

Angalia umri wa mtoto
Wape watoto wako zawadi kulingana na umri wao ili zawadi iwe na thamani kubwa kwa mtoto. Kwa mfano, nyumba au gari ni vitu vyenye thamani kubwa, lakini kama utampatia zawadi hiyo mtoto wa miaka miwili, ni wazi kuwa hataifurahia, sawa na atakavyofurahia biskuti au mapulizo [balloon].

Zawadi anayoipenda
Mpatie mtoto zawadi anayoipenda. Watoto wana vitu wanavyovipenda kuliko vingine. Kwa minajili ya kumfurahisha, jitahidi kumpatia mwanao zawadi ya kitu anachokipenda. Kwa mfano, wapo watoto wanapenda zawadi za kitalii kama vile kutembelea mbuga za wanyama au maeneo ya kale. Wengine wanapenda sana nguo au viatu vipya, mabegi ya shule, viatabu n.k. Hivyo, kulingana na uwezo wako, jitahidi kumpatia mwanao zawadi ambayo anaipenda zaidi.

Zingatia uwezo wako
Zawadi izingatie uwezo wa mzazi. Zawadi nzuri ni ile ambayo mzazi unaweza kuimudu. Ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya wazazi wanakopa ili kununua zawadi za watoto! Hili ni jambo la hatari na linaondoa hata ladha ya zawadi yenyewe. Mzazi, fahamu kuwa, zawadi inayotoka moyoni hata kama umeichuma porini au umeinunua kwa shilingi mia ina maana kubwa sana kwa mwanao

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close