6. Malezi

Wakinamama, lengo la kuumbwa kwetu iwe dira yetu ya malezi

watoto ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini pia ni mtihani, kama Mwenyezi Mungu alivyosema: “Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu ni Fitna (mtihani), na kwamba kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa,” [Quran, 8: 28].

Na katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndiyo walio khasiri.” [Qur’an 63:9].

Wakati tukifurahia neema ya kuruzukiwa mtoto, tukumbuke wajibu wetu kama wachungaji wa watoto, yaani wazazi, kama Mtume alivyosema: “ Jueni kuwa, kila mmoja kati yenu ni mchunga na ataulizwa juu ya wale anaowachochunga.” [Muslim].

Miongoni mwa mifano ya wachungaji ambayo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliitaja katika Hadithi hii, ni ule mwanamke: “Mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mumewe na wanawe na ataulizwa kuhusu hao.”

Mwanamke ana jukumu kubwa mno katika malezi, ukiacha lile jukumu muhimu la mwanzo ambalo tushalijadili la kuwa mlango wa mtoto wa kuingilia duniani – yaani kubeba ujauzito, kuulea na kuzaa. Historia imejaa mifano ya watu watukufu waliolelewa na mama tu baada ya baba zao kufariki.

Mmoja wa mifano bora tunayoweza kuitoa wa akina mama waliotoa mchango mkubwa katika kuwajenga watoto wao kuwa mashujaa wakubwa watakaokumbukwa katika historia ni shangazi wa Mtume, Safiya bint Abdul Muttalib, ambaye ni mama wa shujaa mkubwa wa Uislamu, Zubair bin Al- Awwam. Safiya ambaye ni ndugu wa Hamza bin Abdul Muttalib, ndiye shangazi pekee wa Mtume aliyesilimu na kuhamia Madina.

Safiya bint Abdul Muttalib

Safiya alikuwa ni mwanamke jasiri. Baada ya baba wa watoto wake, AlAwwam bin Khuwaylid (kaka wa mke mkubwa wa Mtume, Bi. Khadija) kufariki, Safiya alitumia muda na nguvu zake nyingi kulea wanawe wawili walioachwa yatima, Sa’ib and Zubair.

Inatajwa kuwa, mwanawe mdogo Zubair, aliporejea home akilalamika kupigwa na watoto wenzake, alimsema na kumpiga ili kumjenga awe kumjengea ujasiri wa kupambana. Mmoja wa ndugu wa mumewe siku moja alimkuta anampiga Zubair akamuomba asifanye hivyo, lakini yeye akamwambia anataka amjenge mwanawe awe mwanamume asiyeshindika na asiyekubali kutii kiumbe yoyote.

Si ajabu basi Zubair alikuja kuwa Swahaba mkubwa na shujaa aliyeutetea Uislamu hadi akawa miongoni mwa wale 10 waliobashiriwa pepo.

Wanaingia katika mfano wa wanawake mashujaa pia mama wa maimamu wakubwa wa Hadithi na Fiqhi, akiwemo Imam Mohammed Al-Bukhari, Abu Abdillah Muhammad Idris al-Shafi na Imam Ahmad bin Hanbal.

Ukiachilia hao, hata wale ambao walilelewa na baba na mama, bado wakina mama walikuwa na jukumu kubwa katika kuwajenga kitabia, akiwemo mfano Imam Malik Ibn Anas ambaye alinukuliwa akisema: “Mama yangu alikuwa akinivalisha vizuri mavazi yanayofanana na ya wanazuoni nikiwa mvulana mdogo na kisha akanambia ‘Nenda msikitini ukasome kwa Go to the Masjid Imam ar-Rabia. Soma tabia zake kwanza kabla hujachukua elimu.’”

Kwa hiyo, wakinamama tuna majukumu makubwa, tukiwa kama walimu wa kwanza wa mtoto katika maisha yake. Mtoto hujifunza mambo yote ya awali kutoka kwetu, kula, kuongea, kutambaa, kutembea, kukimbia, kuheshimu na kusuhubiana na watu, kuvaa na kadhalika.

Lengo la kuumbwa kwetu kama dira ya malezi.

Ili kuelewa vema umuhimu wa majukumu yetu ya kimalezi, ni muhimu sana wazazi, hasa sisi akinamama tusisahau lengo la msingi la kuumbwa kwetu, nalo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ambaye pekee anayestahili kuabudiwa. Mwenyezi anasema: “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” [Quran, 51:56].

Ninamkumbusha mama lengo hili la kuumbwa kwetu kwa sababu lengo hilo ndiyo yafaa litengeneze dira ya malezi, yaani kumjenga mtoto kiafya, kielimu, kimaadili na kadhalika ili awe mja mwema anayemuabudu Mwenyezi Mungu.

Katika huko kumuabudu Allah, jambo kubwa ni kumfundisha mtoto Tawhid, asiabudiwe mwingine yoyote zaidi ya Allah Ta’ala; na kuepuke aina zote za shirki kwani hii ni dhambi kubwa kuliko zote. Pia, ajue nguzo sita za imani na tano za Uislamu na ajifunze kuzitekeleza hatua kwa hatua, kadri anavyokua.

Pia, malezi yalenga katika kumfundisha kuwatendea wema wazazi wake na awatii, isipokuwa pale watakapomuamrisha kutenda uovu na vilevile kuunga undugu. Malezi pia yalenge kujenga hofu ya Mwenyezi Mungu kwa mtoto. Aelewe kuwa, kila tendo, jema au la uovu, dogo au kubwa, linarekodiwa na Malaika na atalipwa kwalo.

Malezi pia yalenge katika kumjengea mtoto imani kuwa, hata kama hamuoni Mwenyezi Mungu haina maana kuwa yeye haonwi, bali Mwenyezi Mungu anamuona popote alipo. Malezi yalenge katika kumfundisha mtoto awe na mtazamo sahihi wa Uislamu kama mfumo wa maisha aliotuchagulia Mwenyezi Mungu.

Malezi pia yalenge kumjenga mtoto katika tabia njema, tukimuigiza Mtume wetu (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye Mwenyezi Mungu kamtaja kwenye Qur’an kwa kumwambia: “Na hakika wewe una tabia tukufu.” [Qur’an, 68:4].

Mwenyewe Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakuna kitu kizito katika mizani ya matendo kuliko tabia njema.” [Bukhari]; na akasema tena: “Watumwa wa Allah wanaopendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni wale wenye tabia njema. [Bukhari].

Tabia njema, amabayo mtoto anatakiwa afundishwe ni pamoja na kuwa na subira na kujiepusha na maradhi ya moyo kiburi, kujiona, kujisifu, husuda, ria na kadhalika. Wiki ijayo, in-shaa- Allah, tutaangalia misingi ya mbinu za kimalezi katika ulimwengu wa sasa.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close