6. Malezi

Unataka wanao wasome vitabu? Onesha mfano

Tukizungumzia kusoma Qur’an, tuna maana siyo tu kuisoma tu kwa kuiimba katika Kiarabu chake, lakini pia kujifunza maana na kuizingatia mafundisho yake ili yaakisiwe katika matendo.

Bahati nzuri, katika miaka ya karibuni, kumekuwa na vitabu vingi vya tafsiri ya Qur’an. Licha ya uwepo wa vitabu hivyo, kasi ya Waumini ya kujisomea ni ndogo. Kasi ni ndogo hata mwezi huu mtukufu ambao kuisoma Qur’an kuna ujira mkubwa.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa kutosomwa Qur’an ni sehemu ya tatizo kubwa la watu kukosa utamaduni wa kujisomea siyo tu vitabu vya dini bali hata vitabu vya kawaida.

Utamaduni wa kujisomea unazidi kupotea Duniani, lakini hapa Tanzania hali ni mbaya zaidi. Watanzania si wasomaji kiasi kwamba inasemwa ukitaka kupitisha mambo ya hovyo au kumuibia Mtanzania, weka jambo lako katika maandishi. Tunaona uvivu kusoma hata mikataba tunayoingia!

Utamaduni wa kujisomea ni mdogo mno kiasi kwamba unaweza kukuta mjadala juu ya muswada wa sheria fulani; lakini hao wanaojadili hata hawajaisoma hiyo rasimu.

Katika muktadha wa dini, utakuta watu wanajadili aya ya Qur’an au hadith fulani ya Mtume lakini kwa misingi ya kusikiasikia tu. Wala hawajawahi kuitafuta aya au hadith husika na kuisoma na kusoma sherhe za wanazuoni! Ni ajabu kwamba watu wengi wetu hatupendi kusoma lakini tunapenda kujadili mambo, hususan mitandaoni!

Sababu ya kupungua kwa utamaduni wa kujisomea ni nyingi, ikiwemo maendeleo ya teknolojia ambayo yanafanya watu wawe wavivu. Ni kwamba, vifaa vya kieltroniki kama simu za mkomoni na kompyuta mpakato zilizoungwa katika mitandaoni ya kijamii zimefanya upatikanaji wa taarifa katika hali ya muhtasari kuwa rahisi, hivyo watu tumejikuta tukitegemea mno vidokezo hivyo vya taarifa kuliko taarifa katika ukamilifu wake

Sababu nyingine ya kupungua kwa utamaduni wa kujisomea kwa hapa Tanzania ni kukosekana kwa mbinu sahihi za kujenga mapenzi ya kujisomea kwa watoto mashuleni. Shule ngapi hapa Tanzania zina maktaba zenye vitabu zaidi ya vile vya kawaida vya masomo yao?

Nina maana vitabu visivyo katika mtaala vya mambo mbalimbali yanayovutia watoto kama hadith, mashairi, michezo, visa vya mashujaa, mapishi na vinginevyo vinavyoweza kumfanya mtoto apende kusoma? Sina jibu lakini nina hakika si shule nyingi.

Utamaduni wa kujisomea hujengwa kutoka utotoni. Huenda shule anayosoma mwanao haina maktaba nzuri yenye vitabu sahihi kwa ajili ya kujenga mapenzi ya kusoma kwa watoto, lakini wewe kama mzazi unaweza kuwatengenezea watoto maktaba nyumbani ili kuwashajiisha wapende kusoma.

Kuna mambo matatu muhimu ya kuzingatia katika uanzishaji wa maktaba ya nyumbani kwa ajili ya watoto.

Uwepo wa maktaba

Kwanza, uwepo wa maktaba yenyewe yaani sehemu ambapo vitabu vinahifadhiwa na ikiwezekana mahali hapohapo watoto waweze kukaa na kujisomea. Uteuzi wa mahali hapa unategemea ukubwa wa nafasi ya nyumbani kwako.

Kama una nyumba nzima au upande, chagua chumba chenye utulivu na kinachopitisha hewa vizuri kiwe maktaba. Lakini hata ukikosa nyumba yenye nafasi, siyo sababu ya kutokuwa na maktaba. Ndani ya hicho chumba kimoja unachoishi na wanao, tafuta mahali pazuri popote pa kutunzia vitabu.

Vitabu sahihi

Jambo la pili la kuzingatia katika kuwajengea watoti utamaduni wa kujisomea ni kutafuta vitabu muafaka vinavyokidhi mahitaji ya watoto wako, kadri ya umri wao, na vitakavyopelekea kufikiwa kwa malengo ya usomaji.

Vitabu muafaka ni vile ambavyo vinaendana na uelewa wa mtoto wa umri husika, vinavyomjenga kiakili na kumpa mafundisho mbalimbali, ikiwemo ya kimaadili. Vinaweza kuwa vitabu vya dini, hadith, visa vya watu maarufu na kadhalika, lakini vilivyoandikwa kwa ajili ya mtoto.

Kipya kinyemi, Waswahili wanasema. Isiwe vitabu ndiyo hivyohivyo kila siku. Kila upatapo fursa, nenda katafute vitabu vipya kwa ajili ya watoto ili uweze kudumisha ari yao ya kupenda kujisomea.

Mbinu za kuwafanya wasome

Jambo la tatu na la muhimu mno ni namna ya kuwafanya watoto wapende kusoma, yaani mbinu na mikakati. Katika hili, yafaa kwanza mzazi awe mshiriki mzuri wa usomaji vitabu. Kama mzazi husomi, usitegemee wanao wasome. Kusoma kwa mzazi kupo kwa namna mbili, kwanza kusoma vitabu vya kiwango chake (mzazi) na pili kusoma vitabu vya watoto kuwapa moyo.

Namna nyingine ya kuwashawishi watoto wapende kusoma ni kujadili maudhui ya vitabu. Kiwango cha chini ya kujadili ni mtoto kutoa mrejesho wa maudhui, yaani kuhaditha kitu alichosoma, hususan hadith za kitoto.

Si vibaya pia mzazi kutenga muda maalumu wa kujisomea, kama hilo linawezekana; vinginevyo mnaweza kusoma na wanao kila muda unapopatikana.

Kazi kwenu wazazi, waandishi Kwa kumalizia tunahimiza wazazi wajitahidi sana kuwajengea watoto utamaduni wa kujisomea ambao utamsaidia atakapojiunga na elimu ya juu na pia kusoma kutamsaidia katika maisha kwa ujumla.

Kusoma vitabu kunafungua akili ya mtoto na kumsaidia kuijua Dunia. Kadhalika, kusoma vitabu kutapunguza muda anaotumia katika simu na vifaa vingine vya elektroniki.

Natoa wito kwa mamlaka waandishi, hususan wa Kiislamu, kuandika vitabu vingi zaidi kwa ajili ya watoto maana wakati tukishwishi watoto wasome lazima pia tuwachagulie vitabu sahihi kutokana na umri wao. Haiwezekani wewe ni Muislamu wa madhhebu za Sunni unaleta vitabu vya watoto vya Kikristo au vya Kishia nyumbani kwa ajili ya wanao. Utawaharibu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close