6. Malezi

Umuhimu wa kuzitunza haki za wanandoa

Kwa hakika dini ya Kiislamu imemtukuza mwanamke kwa namna ya pekee. Uislamu ulitambua haki za mwanamke na kuamrisha apewe heshima ya hali ya juu kwa sababu yeye ni moja ya vyanzo viwili vya ubinadamu kwa jumla.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.” [Qur’an, 49:13].

Licha ya dini ya Kiislamu kumpa mwanamke heshima na hifadhi ya hali ya juu, wapo wanaojaribu kuichafua kwa kudai imemnyima mwanamke uhuru wake na kumfanyia dhulma kwa kumpendeleza mwanamume.

Hata hivyo, ukweli ambao uko wazi kwa yeyote mwenye akili na uelewa ni kwamba Uislamu ulimpa mwanamke uhuru wake na kumfanya mwandamu mwenye huruma na heshima. Kabla ya Uislamu mwanamke alikuwa hana uhuru wa aina yoyote.

Kwa kuangalia hali ya mwanamke kabla ya Uislamu na baada yake, tunaona tofauti kubwa sana katika hali zote. Mwanamke wa enzi za kabla ya ujio wa Uislamu alikuwa ni kama ‘kitu’ tu miongoni mwa vitu anavyomilki mwanamume. Mwanamme alimfanya mwanamke anachotaka, muda wowote anapotaka na kwa namna anavyotaka.

Mwanamke wa kabla ya Uislamu alikuwa anauzwa, anatumwa, anabakwa, anasalitiwa, anadhalilishwa hadi kiasi cha kuzikwa akiwa hai. Hali ya mwanamke imebadilika sana mara baada ya kuja kwa Uislamu. Mwanamke ametukuzwa na akapewa haki sawa na mwanamme katika utekelezaji wa majukumu ya kimaisha.

Kwa mtazamo wa Uislamu, mwanamke ndiye msaidizi wa mwanamme; na mwanamke bora zaidi ni yule anayemsaidia mumewe katika majukumu ya maisha.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ametaja sifa za mwanamke bora katika kauli yake: “Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanaojilinda hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika utiifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye juu na Mkuu” [Quran, 4:34].

Hizo ni sifa za mwanamke bora ambaye ni mke. Kwa wakina mama, Uislamu pia umewatukuza sana. Watoto wameamrishwa wawatii mama zao na kuomba radhi yao. Watoto wametakiwa kutomkasirisha mama.

Pia Uislamu umesema kuwa, ridhaa ya wazazi na hasa mama, ni njia mojawapo za kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na baraka dunaini na malipo mema Akhera, yaani Pepo.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema: “Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapofika utu uzima wake, na akafikilia miaka 40, husema, ‘Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayoyapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu’” [Qur’an, 46:15].

Inabainika kutokana na dua katika aya hiyo kuwa wametajwa wazazi wawili ikafuatiwa na kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu wa kuitengeneza dhuriya. Na kule kutajwa kwa mama peke yake ni kutia mkazo juu ya nafasi yake kubwa na adhimu kutokana na taabu alizozipata kuanzia kipindi cha ujauzito, kujifungua, kunyonyesha, kulea hadi mtun anakuwa mtu mzima.

Uislamu umemtukuza mama kwa kuzingatia fadhila na mchango katika kulea wanawe katika misingi ya malezi mema iliyopitishwa na Uislamu. Malezi hayo mema ya mama na maelekezo yake yanachangia kukiandaa kizazi cha Waislamu wanaolazimika kufuata njia iliyonyooka wakishikilia tabia njema.

Katika kujibu mjadala ambao unaibuka kila wakati kuhusu msimamo wa Uislamu juu ya mirathi, ndoa za mitala, mamlaka aliyopewa mwanamme ya kumsimamia mwanamke, tunasema kwamba kila sheria ina sababu na hekima yake. Hivyo basi, ni muhimu kutafakari sababu na hekima hiyo kabla hatujahukumu kuwa sheria hii inamsaidia mwanamke au inamdhulumu.

Kwa mfano, katika hukumu za mirathi, kuna wanaodai kwamba mwanamume anapata kiasi kikubwa zaidi kuliko mwanamke wakati wawili hawa wanatakiwa kuwa na hadhi sawa katika urithi walioupata kutokana na kifo cha baba au yeyote mwingine.

Tunawajibu kuwa, ukiangalia kwa makini mfumo wa mirathi katika Uislamu, unaona uhalali wake katika sura mbalimbali. Kwanza, katika hali kadhaa nyingine mwanamke anapewa hadhi sawa sawa na mwanamume na wakati mwingine mwanamke anachukua kiasi kikubwa zaidi.

Kuhusu ndoa ya mitala, sheria ya Kiislamu hairuhusu kila Muislamu kuoa wake wanne hovyo hovyo, bali sheria imeweka vidhibiti, vigezo na masharti maalumu kwa mwanamme kutimiza kabla ya kutekeleza hilo.

Sheria ya Kiislamu ilipitisha hukumu hiyo kwa kuzingatia mazingira ya jamii. Kwa mfano, inajulikana kuwa, kimaumbile wanawake wako wengi zaidi kuliko wanaume. Hali hii imepelekea wanawake wengi kuishi bila kuolewa. Wakati huo huo, hutokea wakati mwingine matukio yanayolazimsha mwanamume aoe mke wa pili kama vile kutopata mtoto kutoka kwa mke wake wa kwanza.

Jambo la kuzingatiwa kuhusu suala la ndoa za mitala ni kuwa sheria ya Kiislamu haikuacha jambo lifanywe ovyo bali imeainisha masharti na vigezo ili kudhibiti kuoa kiholelaholela. Itoshe kukumbusha kauli yan Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:

“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” [Qur’an 4: 3].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close