6. Malezi

Ukali siyo njia pekee ya malezi

Katika jamii yetu watoto wamekuwa wakilelewa kwa namna mbalimbali. Moja ya njia maarufu ambayo watoto wengi hupitia ni ya kutishwa ili wawaogope wazazi.

Wazazi wengi ni watu wakali sana na hawaoni haja ya kuongea kiupole na watoto kurekebisha tabia zao, bali huona njia nzuri ni kuwafanya watoto wawaogope. Ukiwauliza wazazi wengi kwanini wanaamua kutumia njia hii, hoja yao kubwa huwa ni hofu ya kuharibika kwa watoto. Kwa wazazi hawa, njia hii ni mujarabu kwa kuwa huwafanya watoto muda wote kuwa watiifu kwa wazazi wao.


Malezi ya ukali huwafanya watoto kuogopa kuripoti matukio ya hatari

Kwa mtazamo wa juu juu ukali unafanyika kwa nia njema ya kuimarisha nidhamu ya watoto. Hata hivyo, kwa mtazamo wa ndani njia hii ina mushkeli mkubwa. Mzazi unatakiwa kuwa mkali pale inapobidi, yaani mtoto anapofanya kosa kubwa. Vinginevyo kwa makosa ya kawaida, mzazi anaweza kutumia njia ya mazungumzo (kuonya) kurekebisha tabia zisizofaa.

Ni muhimu kufahamu kuwa, ukali uliopitiliza hausaidii sana katika malezi ya watoto. kuwa mkali pale inapobidi; na tumia njia za mazungumzo pale inapobidi. Wazazi ambao wanapenda sana kutoa ukali na kutoa adhabu ngumu, wanaweza kujikuta wanazalisha watu wasiofaa katika jamii. Ulezi huu una madhara kwa mtoto, jamii na hata taifa. Baadhi ya madhara ya ukali ni haya yafuatayo:

Nidhamu ya woga
Ukali huzalisha watoto wenye nidhamu ya uoga. Hali hii husababishwa na mibinyo ya wazazi ambapo watoto hulazimika kuigiza tabia ili tu kuwaridhisha wazazi. Matokeo ya hali hiyo ni kutengeneza jamii yenye watu feki ambao hufanya mambo ili kuwafurahisha watu waliowazunguka hata kama wao wenyewe hawayapendi.

Ukali huondoa kujiamini
Malezi ya ukali huwanyima watoto kujiamini. Wazazi wakali ni kama watu watata-hawajulikani wanachopenda na wasichopenda. Hivyo, watoto mara zote wanaishi roho juujuu bila kujua hatima yao. Maisha haya huwanyima watoto hali ya kujiamini.

Hofu na kushindwa kujieleza
Ukali huwajengea watoto hofu na kushindwa kujieleza. Katika jamii yetu, tunashida kubwa ya watu wetu kukosa stadi muhimu za kujieleza. Njia nzuri ya kuijenga tabia hii ni wazazi kujenga utamaduni wa kuwasikiliza watoto wao hata pale wanapoonekana kuwa wamekosea. Ikiwa utalea watoto kwa ukali, inakuwa jambo gumu sana kuwapata watoto wenye kujiamini na wanaoweza kujieleza.

Ukali hupunguza mapenzi
Malezi ya ukali hupunguza mapenzi ya watoto kwa wazazi. Kama mzazi hujui basi fahamu kuwa, ukali uliopitiliza huweza kumfanya mto wako akuchukie. Katika familia zetu nyingi utaona watoto wengi sana wapo karibu mno na mama zao, jambo ambalo linawaudhi wazazi wa kiume wakidai kuwa hali hiyo inaharibu watoto. Ukweli ni kuwa, mama wengi wana uwezo mkubwa wa kuongea na kujadiliana na watoto wao hata pale wanapoonekana wamekosea. Ile hali ya kuwasikiliza watoto na kuwakosoa pale inapobidi hujenga maelewano na mapenzi makubwa baina ya watoto na mama zao.

Malezi ya ukali huwafanya watoto kuogopa kuripoti matukio ya hatari. Kama kuna hatari kubwa kwa watoto wetu katika zama hizi, basi ni kule kushindwa kwao kuripoti matukio ya hatari. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, watoto wamejengewa hofu na wazazi wao kiasi cha kushindwa kuwakimbilia katika matatizo. Hali hii inathibitishwa na namna matukio mengi ya udhalilisha watoto yamekuwa yakichukua muda mrefu kubainika.

Watoto wengi wamekuwa wakitaja sababu kuu kuwa ni woga wa kuwaeleza kwa wazazi. Watoto wengi wapo njia panda, hawajui waseme au wakae kimya. Tuepukeni kuwajengea watoto hofu ili wawe huru kuripoti matukio haya haraka iwezekanavyo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close