6. Malezi

Uhujumu uchumi ni kielelezo cha mdororo wa maadili

Ni doa kubwa la kimaadili miongoni mwa Watanzania. Hivi ndivyo tunavyoweza kusema baada ya watuhumiwa 467 wa makosa ya uhujumu uchumi kukiri makosa yao na kuahidi kurejesha fedha Shilingi 107 bilioni wanazotuhumiwa kuzihujumu.

Hatua hiyo inafuatiwa na msamaha alioutoa Rais John Magufuli kwa watuhumiwa hao, mnamo siku ya Jumatatu, Septemba 30 mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa Septemba 22 mwaka huu, wa kuwasamehe wale wote watakaokiri makosa yao na kulipa kiasi cha fedha walizozihujumu.

Aidha, Rais ametoa wito kwa watuhumiwa wengine wa makosa ya uhujumu uchumi, ambao wana nia ya kurejesha fedha walizozijuhumu kufanya hivyo ndani ya siku saba (kuanzia Septemba 30 hadi Oktoba 6 mwaka huu).

Hii si mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kuwachukulia hatua watu wanaobainika kutekeleza vitendo vya uhujumu uchumi, kwani katika awamu zilizopita viongozi wa ngazi mbalimbali walipambana kwa namna moja ama nyingine na vitendo vya uhujumu uchumi huku wakiwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii.

Jitihada zote hizo zinaonesha ni kwa kiwango gani mapambano dhidi ya vitendo vya uhujumu uchumi yalivyo magumu. Hii ni vita kubwa ambayo inawataka wapiganaji kuwa shupavu na kukubali kujitoa ili kuliokoa Taifa kuepukana na janga hilo.

Serikali imeonesha juhudi zake kukabiliana na vitendo vya uhujumu uchumi, lakini vile vile ni muhimu kwa viongozi wa dini kukemea vitendo hivyo viovu. Kwa ufupi, vita ya kupambana na uhujumu uchumi inahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa viongozi wa dini na serikali, watendaji, wananchi na wenye mamlaka ya kupambana na uhujumu uchumi.

Hata ndoto ya Tanzania kufikia lengo la kuwa nchi ya viwanda haliwezi kufikiwa iwapo viwanda hivyo vitaendeshwa na watu wenye silika ya kulihujumu taifa.

Uhujumu uchumi, kama wizi mwingine wowote ni dhambi na unaweza kukuingiza katika moto wa Jehannamu. Si hivyo tu, uhujumu uchumi unaweza kukuingiza katika sifa ya unafiki kwani unabeba sifa zote za watu wa kundi hilo baya, umetenda uongo, umekosa uaminifu na umefanya hiana.

Kwa hali tuliyofikia sasa, inaonekana tuko tayari kufanya chochote kupata kinachoitwa ‘mafanikio’ ya kidunia. Hivyo, ipo haja kwa viongozi wa dini wa kweli kuwa mstari wa mbele kuwaonya waumini wao waache vitendo vya uhujumu uchumi kwani licha ya kudhoofisha wananchi na taifa, pia kuhujumu uchumi ni kitendo kisichokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ni muhimu viongozi wa dini kutoa maonyo kwa sababu, aghalabu watu wengi huhofia masuala ya dini hasa pale yanapohusu maisha ya baada ya kifo kwani wengi huwa wanatamani waende peponi na siyo motoni.

Katika mazingira hayo, kauli za viongozi wa dini zina nguvu kubwa na zinaweza kuleta ushawishi mkubwa katika vita dhidi ya uhujumu uchumi ambayo taifa inapigana nayo. Viongozi wa dini iwapo watakubali kutekeleza wajibu wao na kuufanyia kazi, watakuwa wametoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya vitendo vya uhujumu uchumi.

Ni balaa na ni dhambi kubwa kuruhusu au kuendekeza tabia ya uhujumu uchumi. Viongozi wa dini ya Kiisalmu wana kila sababu ya kuikemea na kuipinga tabia hii, kwa kuzingatia mafundisho ya Mtume wetu: “Mtu aliyeuona uovu, na auondoe kwa mkono wake, akishindwa, basi auziwie kwa ulimi wake, na kama akishindwa, basi na achukie moyoni mwake, na kuchukia kwa moyo ni imani dhaifu.” (Muslim).

Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close