6. Malezi

Ufanisi wa kimalezi huanza na chaguo sahihi la mwenza

Malezi ya watoto ni jambo kubwa na muhimu ambalo wazazi wanatakiwa kulishughulikia na kulipa umakini mkubwa ili kujenga familia nzuri, yenye mafanikio siyo tu ya kidunia bali pia kesho Akhera. Malezi mema, pia, huzalisha watoto watakaochangia mafanikio si tu yao binafasi bali pia ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Mtoto anatakiwa alelewe kiafya, kiakili, kitabia, kihisia na kiroho. Ingawa malezi halisi yanaanza mtoto anapozaliwa, misingi yake inaanza kwenye chaguo la mwenza wa ndoa. Chaguo sahihi la mwenza wa ndoa huchangia katika ufanisi wa kimalezi.

Mtu asiingie katika ndoa bila kufanya uchunguzi wa kina kwa yule ambaye anakusudia kumfanya mwenza wake, kisha kutaka ushauri [istikhara] kwa Allah juu ya uchaguzi huo na kuwataka ushauri watu wa kweli na wenye nia nzuri wanaoweza kumpa nasaha zenye manufaa katika ngazi hiyo ya maisha anayokusudia kuingia.

Mke ndiye anayetarajiwa kuwa mama wa watoto. Watoto hao watakulia katika malezi yake na wataathirika na tabia zake. Baba pia atakuwa na sehemu kubwa ya ulezi kwa watoto, nao wataathirika na tabia zake.

Mwanazuoni mkubwa wa lugha ya Kiarabu na pia mshairi, Abu al-Aswad al-Du’ali aliwaambia watoto wake:

“Nimekufanyieni wema mkiwa wadogo, wakubwa na kabla hamjazaliwa.” Wakamwambia: “Ulitufanyia vipi wema kabla hatujazaliwa?” Akawaambia: “Niliwachagulieni mama zenu ambao hamtatukanwa kwa sababu yao.” Ni muhimu kuweka msingi imara na si kuhangaika kuziba ufa.

Ukiacha chaguo sahihi la mwenza ipo pia misingi mingine ya kuzingatia inayochangia katika ufanisi wa malezi mwema. Ukiangalia misingi hiyo, bado unaona kuwa ukiwa na mwenza mwenye uelewa sawa nawe, mambo huwa rahisi zaidi.

Kumuomba Allah kizazi chema

Ni muhimu tujue kuwa, Allah ndiye Mjuzi wa kila jambo na hutegemewa kwa kila kitu. Ni Yeye ndiye hutoa msaada kwa waja wake kutokana na udhaifu wao. Hivyo, ni muhimu kumtaka msaada katika malezi ya watoto. Ukimtegemea Allah na kumtaka msaada, utafanikiwa.

Kuwaombea watoto ni moja kati ya mambo muhimu kwa mzazi na ya kudumu nayo kwani dua ya mzazi ina nafasi kubwa sana ya kukubaliwa. Hivyo basi, ni vizuri kutumia fursa hiyo kuwaombea watoto mazuri na si kuwaombea mabaya.

Ikiwa watoto ni wema, mzazi awaombee ziada ya wema kwa Allah, na ikiwa wana dalili ya kutokuwa wema, basi mzazi adumu katika kuwaombea uongofu kwa Allah kwani wakipotoka mzazi naye anakuwa na sehemu ya makosa juu ya kupondoka kwao na atakwenda kuulizwa.

Hivyo, katika hali zote, ni muhimu wazazi wawili kudumu katika kuwaombea watoto kwa Allah. Hili ni jambo walilolifanya Manabiii wa Allah na pia ni moja kati ya sifa za waja wema wa Allah. Mathalan, Nabii Zakaria (amani imshukie) amesema.

“Palepale Zakaria akamwomba Mola wake Mlezi, akasema, ‘Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi.’” [Qur’an, 3: 38].

Allah Aliyetukuka anaelezea moja ya miongoni mwa sifa za waja wema: “Na wale wanaosema, ‘Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMungu.’” [Qur’an, 25:74].

Kufurahia uzao na kumtaka Allah msaada

Kuridhia na kutokasirika kwa sababu ya aina yoyote ya mtoto aliyezaliwa ni katika misingi ya kujenga jamii bora. Asione dhiki mzazi wala kuhisi kuwa ni mzigo juu yake (akipata mtoto wa kiume au wa kike) kwani mwenye kuruzuku ni Allah Aliyetukuka.

Isitokee mmoja kukasirika kwa hoja kuwa mkewe anazaa sana au anazaa watoto wa kiume tu au anayezaa watoto wa kike tu, bali hiyo ni tunu kubwa kutoka kwa Allah naye ndiye anayepanga wa kumruzuku aina ya mtoto anayetaka yeye na si yule unayemtaka wewe.

Allah Aliyetukuka anasema: “Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu, anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.” [Qur’an, 42: 49-50]

Wape watoto majina mazuri, waombeae dua

Ni jambo muhimu sana kuchagulia watoto majina mazuri na yenye maana nzuri. Haifai kuwaita watoto majina yaliyokatazwa kisharia au yanayochukiza au yenye kuonesha ubaya.

Majina yanadumu na watoto muda wa uhai wao wote. Majina pia yanaathiri tabia za watoto. Huenda mtoto akaitwa jina baya ikawa ni sababu ya kuchukiwa katika jamii. Amesema Ibnul-Qayyim: “Ni mara chache sana ukaliona jina baya juu ya kitu kisichokuwa kibaya.”

Kupandikiza Imani, maadili na itikadi sahihi mapema

Watoto wafundishwe tangu wakiwa wadogo kumtambua Muumba wao na kumpenda pamoja na kumpenda Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), kama alivyofanya Mtume kumfundisha Ibn Abbas itikadi sahihi tangu akiwa mdogo. Pia, mtoto alelewe katika misingi ya kumcha Allah, ukweli, upendo uaminifu, uvumilivu, upole, na tabia nyingine nzuri tangu utotoni.

Vilevile, mzazi amfundishe mtoto Qur’an, Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na vilevile amfundishe adhkaar (uradi) wa kutumia katika maeneo mbalimbali kama alivyofundisha Mtume. Mtoto aliyehifadhi Qur’an na Sunna huathirika na mafundisho yaliyomo ndani yake na kuwa msaada mkubwa katika malezi.

Ni muhimu mzazi atenge muda wa kukaa na familia yake kuifundisha au kuinasihi katika yale yanayomridhisha Allah. Mzazi awazoeshe watoto tabia nzuri kama vile kuwakirimu wageni, kutoa na kuitikia salamu, kusaidia wenye shida, kuwa na upendo kwa watu, kuwazoesha mazungumzo mazuri kwa kutumia maneno yanayofaa na yanayopendeza, pamoja na kujiepusha na maneno machafu na mazungumzo mabaya yasiyofaa mbele ya watoto kama vile kutukana na kugombana.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimfundisha Amr bin Abii Salam tabia za kula tangu akiwa mdogo, kama Amr mwenyewe alivyosimulia:

“Nilikuwa kijana mdogo katika malezi ya Mtume, mkono wangu ukawa unazunguka kila sehemu kwenye sahani. Mtume akaniambia, ‘We kijana kwanza litaje jina la Mola wako (yaani aseme ‘Bismillahi’ anapoanza kula) na ule kwa mkono wako wa kulia na kula sehemu inayokuelekea.’” [Bukhari na Muslim].

Kuwatenga na tabia mbaya

Ni muhimu kuwatenga watoto na tabia mbaya kama vile uongo, dhulma, kuwadharau wazazi, kukata undugu, tamaa, uoga, kusengenya, uchoyo na tabia zote mbaya. Mzazi achukie tabia hizi, adhihirishe mbele ya watoto kuwa ni tabia mbaya na anazichukia. Pia awafundishe kuwa Allah anachukia tabia hizi na mwenye kuwa nazo ataadhibiwa mbele ya Allah Aliyetukuka .

Kuwa kigezo chema

Mzazi anatakiwa awe ni mfano wa kuigwa kwa watoto wake. Kile anachokifanya mbele yao ni sehemu ya malezi. Atambue kuwa maneno yake na matendo yake ni sehemu ya somo analolitoa kwa familia yake kila siku, asiwaamrishe watoto jambo ambalo anafanya kinyume.

Kutekeleza ahadi uliyoitoa kwa mtoto ni jambo muhimu sana kwani kutotekeleza kunamvunja moyo na pia ni kumzoesha kuahidi ahadi zisizotekelezeka.

Pia, kufanya ibada mbele ya watoto ni namna ya kuwafundisha kwa vitendo. Pia ni muhimu kuwahimiza kwenda msikitini. Mzazi pia afuatilie makuzi ya mtoto na mabadiliko yake kwa karibu pamoja na kuangalia marafiki wake wanaomzunguka, kwani mazingira yanachangia sehemu kubwa ya malezi ya mtoto.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close