6. Malezi

Tuwe mabalozi wa Uislamu kupitia tabia njema

Ili Uislamu wa mtu ukamilike, unahitaji siyo tu kuwa na itikadi (aqidah) sahihi moyoni juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu Mmoja asiye na mshirika anayestahili kuabudiwa yeye peke yake na pia kutekeleza ibada za wajibu na sunna kama sala, funga na kadhalika; bali unahitaji pia kuwa na tabia njema.

Katika kuzungumzia umuhimu wa tabia njema, Abu Darda amesimulia kuwa, Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Hakuna kitu kizito katika mzani wa amali (Siku ya Kiyama) kuliko tabia njema.” [Bukhari]. Hivyo tabia njema ni uokovu wetu Siku ya Kiyama.

Hadith zinazozungumzia tabia njema ni nyingi. Abu Huraira (Allah amridhie) amesema: “Nilimsikia Abu al Qasim (Mtume), akisema, ‘Wabora miongoni mwenu katika Uislamu ni wale tabia njema…” [Bukhari]. Katika Hadith nyingine, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Vipenzi zaidi katika viumbe wa Mwenyezi Mungu ni wale wenye tabia njema.” [AtTabarâni na imesahihishwa na Albani katika ‘Silsilatul-AHaadeethisSaheehah’].

Katika Hadith iliyosimuliwa na Abu Huraira (Allah amridhie) amesema aliulizwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema:

“Kumcha Allah na tabia njema.” Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema: “Kinywa (mdomo) na utupu.” [Tirmidhiy].

Ukiizingatia Hadith hii utaona kuwa hata hicho kinywa na utupu, viungo ambavyo vitawaaingiza wengi motoni pia vinawakilisha tabia mbaya mbalimbali kama vile uzinifu, usengenyi, uchonganishi, uongo, matusi, maudhi kwa watu na kadhalika.

Mtume katika Kigezo Chema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye ametajwa kuwa ni Kiigezo Chema kwetu.

“Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye ni Kiigizo Chema kwetu, alikuwa na tabia njema kiasi hadi Mola wake Mtukufu amemsifu katika Qur’an: “Na hakika wewe una tabia tukufu.” [Qur’an, 68:4]. Tunapaswa kuiga tabia zake tukufu.

Moja ya vipengele vya tabia njema ya Mtume, ni huruma na ulaini wake kwa Maswahaba, Allah Aliyetukuka anasema:

“Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndiyo umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia.” [Qur’an 3:159]. Naye Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alielezea lengo kuu la Utume wake kwa ufupi kwa kusema: “Hakika nimetumwa kwa kukamilisha tabia njema.” [Baihaqi]

Hata Maswahaba wenyewe wanashuhudia kuhusu tabia njema na tukufu za Mtume akiwemo Anas (Allah amridhie) ambaye amesema:

“Nilimtumikia Mtume kwa miaka 10. Katika kipindi hicho, hajawahi hata siku kuniambia ‘Oof’ pale nilipofanya makosa. Hakuwahi kuniuliza, niliposhindwa kufanya kitu, ‘Kwa nini hukufanya kitu kadhaa?’ na hakuwahi kuniambia nilipokosea, ‘Kwa nini umefanya kadhaa.’” [Bukhari].

Na tabia njema zinampandisha mtu katika uchamungu, kama Hadith inavyoelezwa katika Hadith ilisimuliwa na Abu Huraira inavyosema kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie):

“Mtu akiwa na tabia njema, anaweza kufikia daraja sawa na wale wanaosali usiku.” [Bukhari]. Katika Hadith nyingine nyingine zilizosimuliwa na Maswahaba mbalimbali (Allah awaridhie), zimemnukuu Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akinasibisha mafanikio ya duniani na Akhera na tabia njema, na akikemea wale wenye tabia mbaya. Mfano katika Hadith moja maarufu, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwahi kusema: “Yeye ambaye haoneshi huruma kwa wadogo na heshima kwa wakubwa si miongoni mwetu.” [Bukhari].

Kwa ujumla, Uislamu ni dini ya tabia njema na maadili. Miongoni mwa misingi ya dini ni kuwa na tabia nzuri katika mambo yote na hali zote. Kuwa na tabia njema, pia, ni msingi wa kheri za dunia na Akhera, licha ya kuwa pia ni sababu ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Umuhimu wa kufundisha watoto tabia njema

Ukiangalia uzito wa tabia njema katika Uislamu, utajua pia kwa nini unahitaji kukazania kuwafundisha wanao tabia njema. Imesemwa hakuna kitu kizito katika mzani wa matendo Siku ya Kiyama kama tabia njema. Nani hahitaji tabia njema zimsaidie katika siku hiyo nzito? Nasi tuna jukumu la kuwaandaa wenetu kwa ajili ya siku hiyo.

Lakini mwanao akijipambana tabia njema itamsaidia katika maisha yake. Ni kawaida ya wanadamu kuchukia watu wenye tabia mbaya – wadokozi, wasengenyaji, wachonganishi, wavuta bangi, wazinifu, waongo, watu makatili na kadhalika. Mwanao aikukua na tabia hizi unamjengea mazingira magumu sana ukubwani!

Tabia njema, siyo tu humkinga mtoto na madhila ya kuchukiwa na walimwengu, bali pia humfanya apendwe na watu na hata aweze kupata kusaidiwa asipotegemewa. Wapo watu wengi walioajiriwa kwa sababu tu ya tabia zao nzuri za uaminifu. Wapo waliopandishwa vyeo kwa tabia zao njema. Kwa ujumla tabia njema inalipa.

Kwa upande mwingine, kuwafundisha watoto tabia njema kutakusaidia wewe mwenyewe mzazi. Hii ni kwa sababu wema wa mtoto aliyebarikiwa na Mwenyezi Mungu utaanza kwa wazazi wake. Mwanadamu aliyeelewa somo la tabia njema, bila shaka, atawalea, atawaonea huruma na kuwasaidia wazazi wake kipindi cha uzeeni. Kama hiyo haitoshi, binafsi naamini, hakuna da’awa nzuri kuliko kuwa balozi wa Uislamu kwa wasio Waislamu kupitia tabia njema za Kiislamu. Na kuna ushahidi mwingi tu wa visa vya watu kuanzia zama za Mtume na Maswahaba hadi sasa ambao waliukubali Uislamu kwa sababu ya tabia njema za Waislamu. Muandae mwanao awe balozi wa Uislamu kwa kumvesha tabia za Kiislamu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close