6. Malezi

Tuwasaidie watoto wa kike kutimiza ndoto zao

Katika kipindi cha miezi mitatu tangu serikali kusitisha masomo katika taasisi na ngazi zote za elimu hapa nchini ili kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, tumeshuhudia vyombo mbalimbali vya habari vikiripoti matukio ya baadhi ya wazazi kuwaoza watoto wao wanaosoma shule za msingi na sekondari ikiwa ni mkakati wa kuzalisha kipato.

Mbali na hao, pia kuna waliothubutu kuozesha watoto wao kwa kisingizio cha kukosa fedha za kuwasomesha, au pia kwa madai ya kuhuisha mila na desturi za jamii zao. Jambo hili linatusikitisha mno ndiyo maana tumelazimika kulisemea kutokana na ukweli kuwa vitendo vya kuwaoza watoto wa kike angali wanafunzi hupelekea kukatisha ndoto zao wakiwa bado wadogo.

Ripoti nyingi ikiwamo ya takwimu za elimu inayotolewa kila mwaka na Serikali pamoja na ile ya waangalizi wa haki za binadamu (Human Rights Watch) ya mwaka 2016, zinaonesha kuwa kati ya maelfu ya wanafunzi wanaoacha shule, wasichana ndiyo waathirika wakubwa ukilinganisha na wanafunzi wa kiume.

Kwa mfano, takwimu za Serikali mwaka 2016, zinaonesha jumla ya wanafunzi 3,439 walikatisha masomo yao baada ya kupata ujazito na wengine kuolewa. Kadhalika ripoti ya waangalizi wa haki za binadamu ya mwaka 2016, inaonesha kuwa takriban wasichana 8,000 huacha shule kila mwaka kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujazito na kuolewa.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, idadi hiyo ni kwa wanafunzi wanaofikiwa na tafiti ama kujulikana, lakini wapo wasichana wengi ambao baada tu ya kupata ujauzito hufichwa na taarifa zao kutowekwa wazi shuleni kutokana na wazazi kukwepa kunaswa na mkono wa sheria.

Kwa kuzingatia hali hiyo, sisi kama jamii tunapaswa tuwajibike kwa kuhakikisha tunawalinda watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao. Aidha, wazazi wanapaswa kutimiza wajibu wa kusimamia tabia njema za watoto wao wanazofunzwa na walimu pindi wawapo shuleni.

Pamoja na ushauri huo, tunawaasa wazazi na walezi ambao bado wana mawazo mgando kuwa mtoto wa kike hastahili kupata elimu, waachane na fikra hizo kwani watoto wa kike nao ni watoto, wanapaswa kulindwa na kupatiwa elimu kama ilivyo kwa watoto wa kiume.

Ndoa ni muhimu kwa mtoto wa kike, lakini elimu pia ni muhimu hasa katika umri mdogo.

Serikali imejielekeza kutoa elimu ya msingi na sekondari bure kwa wanafunzi wote hivyo wazazi na walezi hawana sababu ya kukatisha masomo ya watoto wao kwa kisingizio cha kushindwa kulipa ada.

Mwisho, tunamuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu, afya na moyo wa uvumilivu wanafunzi wote wakiwamo wa kidato cha sita ambao wanatarajiwa kufanya mtihani wa taifa mwishoni mwa mwezi Juni, 2020.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close