6. Malezi

Tuwajengee watoto moyo wa kujitolea kwa ajili ya jamii

kitaka kujua umuhimu wa wafanyakazi wa kujitolea iangalie taasisi ya Jumuiya ya Kuhuisha Tabia za Kiislamu (JAI). Nenda hospitali yoyote kubwa hapa nchini utasikia sifa nyingi inazomwagiwa jumuiya hiyo ya Kiislamu ambayo imejikita zaidi katika kusaidia wagonjwa.

Tofauti na jumuiya nyingine, wanajumuiya wa JAI hawasadii wagonjwa kwa kuwapa tu vifaa, fedha au chakula, bali wanawauguza kabisa na hivyo kuwapunguzia kazi wauguzi.

Huduma hii imesaidia zaidi wagonjwa wasio na ndugu au wale waliosuswa na ndugu. Kujitolea kwa wajumuiya ya JAI siyo kwa siku moja kwa mwaka, mwezi au wilaya, bali kila siku.

Wanachama wa JAI huamka asubuhi na kwenda hospitali kuhudumia wagonjwa kabla ya kuanza shughuli zao za kutafuta riziki.

Msingi wa jumuiya hii ni kuonesha tabia halisi za Kiislamu. Jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa, kama alivyokuwa Mtume wanayefuata nyayo zake, nao hawabagui. Wanasaidia Waislamu na Wakristo na watu wa dini nyingine.

JAI pia imeng’ara mno katika ukusanyaji damu kiasi hadi serikali yenyewe na wakala wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama wanawatambua!

Sio JAI pekee wanaofanya kazi za kujitolea, zipo taasisi nyingine nyingi za Kiislamu. Kimsingi, Uislamu umejengwa katika msingi wa kujitolea kuliko kazi za kulipwa.

Kuna jumuiya tuliwahi kuandika habari zake iitwayo Sunshine Muslim Volunteers iliyoanzishwa na madaktari wa Chuo cha Afya Muhimbili mwaka 2007 huku ikilenga kutatua changamoto za kitabibu katika jamii lakini hususan kwa Waislamu ambao wao hutakiwa mtu atibiwe na daktari wa jinsia yake. Hawa nao wamefanya miradi mingi ya kujitolea.

Kuna taasisi iitwayo Asw-haabul Kahf ambao wao hujenga misikiti maeneo ambayo hamna nyumba hizo za kumuabudu Mwenyezi Mungu au kuiboresha pale wanapoikuta katika hali mbaya. Hawa wamejenga misikiti 50 hususan katika mikoa ya kanda ya kati katika takriban miaka sita ya uhai wa taasisi yao!

Hiyo ni mifano michache tu ya taasisi za Kiislamu zinazofanya kazi kwa msingi wa kujitolea, lakini ipo mingi.

Tukisema kujitolea, tunakusudia kitendo cha watu kufanya shughuli za kijamii hususan zenye kunufaisha watu masikini na wenye hali duni bila ya kutaka malipo. Katika muktadha wa Uislamu, tunajitolea tukitumai kulipwa Pepo na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.

Kujitolea hakuko kwa Waislamu peke yake bali dunia nzima katika jamii mbalimbali na kimataifa. Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa Waislamu wapo mstari wa mbele zaidi katika kujitolea kwa sababu kufanya hivyo ni sehemu ya ibada (sadaka).

Kimataifa, wafanyakazi wa kujitolea wamefanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano, hususan katika Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika yake huku Waislamu wakiwa ni sehemu muhimu ya hao wanaojitolea huko na kuleta tofauti katika maisha ya jamii mbalimbali.

UN yaadhimisha wanaojitolea

Kwa kutambua umuhimu wa watu hawa, Disemba 5 iliteuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi wa Kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Siku hii ilipitishwa kwa azimio namba A/ Res/40/212 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 17 mwezi Desemba mwaka 1985.

Tangu wakati huo, serikali, mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wamekuwa wakiungana na wafanyakazi wa kujitolea duniani kote kusherehekea siku hii.

Mwaka huu, UN ilitumia siku hiyo adhimu kutambua na kuthamni mchango wa wafanyakazi wa kujitolea katika kukabiliana na majanga mbalimbali, ikiwemo ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona au COVID-19.

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ulimulika wafanyakazi hao katika siku hii kwa kutambua kuwa, “duniani kote, wafanyakazi hao wanasaidia makundi yaliyo hatarini zaidi, wanarekebisha taarifa potofu, wanaelimisha watoto, wanatoa huduma muhimu kwa wazee na kusaidia wahudumu wa afya walio mstari wa mbele.”

Guterres alisema kadri dunia inavyojaribu kujikwamua kutoka kwenye majanga mbalimbali, wafanyakazi wa kujitolea wataendelea kuwa na dhima muhimu kuelekea katika kujenga ustawi wa jamii, kujenga uchumi usioharibu mazingira, jumuishi na wenye haki.

Aidha, alikumbusha kuwa bila shaka kujitolea ni uti wa mgongo wa jamii na kwamba mara nyingi wafanyakazi wa kujitolea wanajenga hisia ya umoja, wanaimarisha utangamano wa kijamii, na wanahitajika kulinda jamii hususan kwa kuwafikia wale watu walio kwenye uhitaji zaidi.

Katibu Mkuu huyo alizitaka serikali zichagize moyo na ari ya kujitolea kwa wananchi na kuunga mkono na kuzitambua juhudi hizo katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katibu Mkuu Guterres alitamatisha ujumbe wake akisema, wafanyakazi wa kujitolea wanahitaji shukrani za dhati.

Mfano wa TIF

Kama nilivyosema awali, taasisi za kujitolea zipo nyingi, lakini ujumbe muhimu katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku hii ni kuwaenzi jamii hii ya wafanyakazi wa kujitolea.

Katika hili, tunaweza kuiga mfano wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) ambayo inawatumia wanaojitolea katika shughuli zake nyingi lakini pia inawapa nafasi na heshima kubwa.

Kupewa nafasi kunamuisha kuwashirikisha katika mambo mbalimbali hadi wajisikie kuwa wao ni sehemu halisi ya kampeni au mradi husika. Taasisi ya TIF imefanya hivyo kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwaheshimisha wanaojitolea. Naelewa kuwa, TIF ina kitengo kabisa cha wanaojitolea na kiko madhubuti mno.

Kukumbusha tu, taasisi ya TIF inayoongozwa na Arif Nahdi, kama mwenyekiti akisaidiwa kwa karibu na timu ya watendaji akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Sheikh Ibrahim Twaha, inafanya shughuli nyingi za kijamii na kidini ikiwemo ujenzi wa misikiti, uchimbaji wa visima, uendeshaji wa vituo vya watoto yatima.

TIF pia inaendesha shule nne zikiwemo za msingi na sekondari na zahanati moja iliyopo Mikumi. TIF pia inamiliki TV Imaan, Radio Imaan na Gazeti Imaan, bila ya kusahau idara ya Da’awah inayoeneza ujumbe wa Uislamu kupitia njia mbalimbali ikiwemo uandaaji wa makongamano.

Eneo jingine ambalo taasisi ya TIF imeng’ara mno ni katika kutoa misaada ya kibinaadamu kwa wahanga wa majanga mbalimbali ikiwemo mafuriko, moto, matetemeko ya ardhi na kadhalika. Taasisi ya TIF imekwenda karibu kila mahali kulipotokea majanga ili kuwafaraji watu.

Ili kukamilisha shughuli hizi mbalimbali zilizo katika wasifu wa taasisi ya TIF, watendaji waajiriwa pekee hawatoshi. Kazi ni nyingi, watu ni wachache. Ni kwa sababu hiyo kumekuwa na watu wanaojitolea kusaidia kufanikisha shughuli hizi. Hawa na wengineo wanaojitolea katika taasisi nyingine ni mashujaa, hivyo tuwaenzi.

Hii ikiwa ni makala ya malezi na familia, nimalize kwa kutoa rai kwa wazazi tuwafundishe watoto wetu dhana ya kujitolea na tuwahimize kufanya hivyo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close