6. Malezi

Tuwafunze watoto kutoa sadaka

Dunia ni daraja ambalo viumbe hupita kuelekea Akhera. Qur’an Tukufu na Sunna vinathibitisha hilo lakini pia kitendo cha mtu kuzaliwa na kufa ni ushahidi wa mwingine wa kimazingira.

Walikuwepo hapa duniani watu (umma) katika zama moja kisha wakaondoka na nafasi yao kuchukuliwa na umma mpya. Kwa hiyo, kimsingi, dunia siyo mahala pa kudumu bali ni daraja la kuelekea Akhera .

Licha ya kuyafahamu haya, wengi miongoni mwetu tumekuwa tukitumia muda mwingi kuzama moja kwa moja katika kuitafuta dunia na kuisahau kabisa Akhera yao ambako ndiko kuna maisha ya milele.

 Kutokana na kughafilika huko, Allah Ta’ala anakumbusha kwa kusema: “Wanayoyajua wao ni mambo yaliyofunuka wazi ya dunia na pambo lake, na wao kuhusu mambo ya Akhera na yale yanayowafaa huko wameghafilika, hawayafikirii. [Qur’an, 30: 6-7].

Aghlabu, kundi la watu walioghafilika na kuitafuta dunia hutamani Mwenyezi Mungu Aliyetukuka awape mali nyingi na umri mrefu, lakini wanapopewa neema mbili hizi hushindwa kuzitumia katika mambo yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

Katika kughafilika huko, wapo baadhi ya Waislamu wanaotumia sehemu kubwa ya mali yao katika kufadhili na kudhamini mambo ya maasi na pumbao, huku wengine wakiyafanya hayo kwa lengo la kutaka kusifiwa au kutafuta umaarufu.

Allah Ta’ala anaonya kwa kusema: “Enyi mlioamini, msibatilishe sadaka zenu kwa masimulizi na udhia kama wale ambao hutoa mali zao kwa ajili ya kutaka kuonekana na watu. . . ” [Qur’an, 2:264].

Kutoa zaka ambayo ni nguzo ya dini na sadaka ambayo ni Sunna ni muhimu mno. Malipo makubwa katika kutoa zaka na sadaka yanaelezwa katika Qur’an:

“Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate malipo ya ukarimu. ” [Qur’an, 57:11].

Kwa mujibu wa aya hii, Muislamu analazimika kuchuma mali ya halali na kuitoa katika mambo ya kheri huku akitaraji kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Kutoa ni ibada ya wajibu

Kama ilivyothibiti katika Qur’an na Sunna, suala la kutoa zaka limefanywa kuwa wajibu kama zilivyo ibada za sala, funga, Hijja na kadhalika. Ndani ya Qur’an, mara nyingi kama si zote, Zaka iimekuwa ikifungamanishwa na ibada ya sala, mathalan:

“Na simamisheni sala na toeni zaka. ” [Qur’an,24:56].

Kwa upande mwingine, kutoa sadaka za aina mbalimbali ni miongoni mwa sunna zilizosisitizwa mno siyo tu katika Qur’an bali pia katika hadith na imenasibishwa na uchamungu.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an, 33: 35 ametaja orodha ndefu ya watu aliowaandalia msamaha na ujira mkubwa wakiwemo:

“..watoao sadaka wanaume na wanawake…”

Moja ya njia inayoweza kutumiwa ili kuwafanya Waislamu waitekeleze ibada hii ipasavyo ni kuubeba Uislamu kama mfumo kamili wa maisha na kama walivyofanya waja wema waliotangulia. Njia ya pili ni kufundisha familia zetu, hususan watoto, ibada hii ya kutoa.

Kutoa katika muktadha wa kifamilia

Ili kujenga utamaduni wa kutoa ni muhimu sana kuifundisha ibada hii kwa watoto ili waizoee na wakue na tabia hiyo. Kuna namna nyingi za kufundisha watoto kutoa, ikiwemo kuwataka watoe katika kiasi cha fedha, chakula na kadhalika na kuwapa wanaohitaji.

Si namna nzuri kuwafundisha watoto kutoa kwa kuwapa pesa yako na kuwaambia katoe. Hapa umewafanya daraja tu la kutoa lakini sio wao watoaji. Kilicho bora ni kuwataka kile ambacho ushawapa, kishakiwa chao na huenda washapanga namna ya kukitumia ndio watoe sehemu na wagawie wengine. Njia nyingine ni kuwaelekeza watoto umuhimu wa kutoa.

Hivi karibuni nilikaa na wanangu wawili nikawaambia maneno ambayo yaliwagusa na kuwapa hamasa ya kutoa. Wakati tumekaa, walipita watoto wa mitaani wakiombaomba. Niliwaambia wanangu, si kwa uhodari wao wamezaliwa katika familia yenye walau chakula, malazi na mahitaji muhimu na wala si kwa ujinga wao watoto wamezaliwa katika umaskini.

Niliwataka wanangu wawe wenye kushukuru kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu amewabariki kwa kutoa kichache wanachopata kuwasaidia maskini. Pia, niliwaambia wakitoa, Mwenyezi Mungu atawazidishia riziki zao. Mwenyezi Mungu mwenyewe kaahidi hivyo lakini pia ni ziada unayopewa ni kwa sababu Mwenyezi Mungu amejua kuwa akikupa na wengine watapata! Basi wakafurahi!

Katika kufundisha watoto ibada ya kutoa, tuwaambie pia umuhimu wa kutoa vitu vizuri. Mwenyezi Mungu anasema:

“Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msingevipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.” [Qur’an, 2:267].

Tena tuwaambie watoto kuwa wasidharau kutoa japo iwe ni kitu kidogo mno kadiri ya tendo moja. Mtume katika haditi iliyosimuliwa na ‘Adiyyi bin Haatim amesema:

“Jikingeni na moto hata kwa kipande cha tende.” [Bukhari na Muslim].

Tuwaonye watoto kuwa, mtu anayetumia vibaya yaani katika njia za haramu mali aliyoruzukiwa na Allah Aliyetukuka anajiandalia maangamizi. Mifano ya walioangamia iko mingi katika umma zilizopita na hata zama hizi! Kinachohitajika ni kutumia neema ya mali katika mambo ya kiibada na kusaidia watu tukifuata mifano ya Maswahaba (Allah awaridhie) na wema wengine waliotangulia.

Kwa munasaba huo, ikiwa tunataraji kupata mafanikio ya hapa duniani na kesho Akhera hatuna budi kujitolea mali zetu katika kuunusuru Uislamu na Waislamu, huku tukijiepusha na malengo mengine ya kimaslahi wakati wa kuyafanya hayo.

Katika kuwafundisha watoto kutoa tusisahau kuwahimiza kujiepusha na ria na kujionesha ili wapate malipo makubwa. Tuwafundishe watoto kutoa kwa ajili yaMwenyezi Mungu pekee:

“Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi ya maovu yenu.” [Quran, 2:271].

Onyo kali zaidi dhidi ya kutoa kwa ajili ya kujionesha linapatikana katika Qur’an (2:264):

“Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyochuma.

Na Hakika kutoa ni ibada inayopandisha daraja ya mtu na kumfanya mja mwema. Allah anathibitisha kwa kusema:

“Hamtafikia kabisa wema hadi mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachokitoa basi hakika hakika Allah anakijua. ” [Qur’an, 3:92].

Tunamuomba Allah Ta’ala atujaalie kuweza kuiona haki na kuifuata na pia atuoneshe batili tuweze kuiepuka ili kubaki katika radhi zake. Allah ni mjuzi zaidi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close