6. Malezi

Tusiruhusu runinga na mitandao viwafunze maadili watoto wetu

Maadili kwa vijana wengi hapa nchini imekuwa ni kitu adimu sana. Miaka ya nyuma mtoto alikuwa na maadili ya hali ya juu kwa kuwa mtu yeyote alikuwa na nafasi ya kumsimamia na kumuongoza. Mwanafunzi alikuwa anamuheshimu mwalimu kama anavyowaheshimu wazee wake. Alipokemewa na mwalimu alisikiliza na kutii.Mwalimu alipomwadabisha mwanafunzi shuleni, mwanafunzi huyo alikiri na kukubali kosa.

Bahati mbaya sana jambo hili halipo hivi sasa. Leo hii mwanafunzi akiadabishwa na mwalimu wake ataondoka na kilio hadi nyumbani na kutoa malalamiko kuwa amepigwa. Mzazi au mlezi bila ya kuuliza ataenda mbio mpaka kwa mwalimu na kuanza kumkaripia.

Jambo hili kwa namna moja au nyingine huweza kumpa mwanafunzi nafasi ya kujijengea utovu wa maadili. Hii ni kwa sababu mtoto hujifunza kutokana na vitu anavyoviona.

Kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia imepelekea watoto wengi kufanya mambo kwa vile walivyoyaona yakifanyika ughaibuni. Kwa sababu ya kuiga mambo kibubusa, watoto na vijana wengi wamejikuta wakitenda vitendo
viovu vya uvutaji sigara, bangi na matumzi ya dawa za kulevya. Hivyo vyote vinachangia uharibifu wa
maadili.

Tofauti na ilivyo sasa, miaka ya nyuma vijana walichukuliwa kama watoto wa jamii.

Mathalan, mtu alipomkuta mwanafunzi mitaani nyakati za masomo alikuwa na uwezo wa kumuadhibu na kumpeleka madrasa, shuleni ama nyumbani kwao. Lakini hivi sasa mtu akijaribu kufanya hivyo hushitakiwa ama ugomvi waweza kuzuka baina yake na mzazi wa mtoto aliyeadhibiwa.

Haya ndio yaliyoifikisha jamii yetu katika dimbwi la ufisadi wa kimaadili. Katika zama zetu hizi tunashuhudia baadhi ya wazazi wakishindwa kabisa kusimamia maadili ya watoto wao na huku wakiwaacha huru wakitazama picha zisizofaa kupitia runinga na mitandao ya kijamii.

Si hao tu, pia wapo baadhi ya wazazi hasa wenye vipato ambao hupenda kuwaridhisha watoto wao kwa kuwapa simu, pesa nyingi na kadhalika. Hii huwaharibu kisaikolojia na kimaadili.Katika hili wazazi na walezi wanapaswa kuwajibika kwani wao ndio wasimamizi wa karibu wa watoto. Hii ni kwa sababu, ujenzi wa jamii bora huanzia ndani ya familia ambako mzazihumjenga na kumuandaa mtoto kitabia.

Ijulikane kuwa, maadili ndio urithi pekee na wa kweli ambao mzazi anaweza kumpatia mtoto wake. Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Zawadi bora ambayo mzazi anaweza kumpa mtoto wake ni tabia njema,” (Bayhaqi). Tuna haja ya kurejea maisha ya Mtume (rehema na amani zimshukie) na Maswahaba zake na kujiuliza walifanya nini mpaka wakaweza kuilea jamii katika maadili
ya kumhofu Allah.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close