6. Malezi

Tuibebe ajenda ya kupambana na kamari, ushoga 2019

Mwaka 2018 Miladiya sawa na 1440 Hijiriya umemalizika na kuingia mwaka 2019, ingawa kwa kalenda tukufu ya Kiislamu bado tupo mwaka 1440 Hijiriya.

Mwaka 2019 unaingia huku maovu kama kamari na ushoga yakizidi kushika kasi katika jamii yetu. Kwa sababu kamari na ushoga vina madhara makubwa katika jamii, sisi kama chombo cha habari cha Kiislamu tunalo jukumu la kumkemea kila anayejihusisha na vitendo hivyo viovu na kushauri hatua za kuchukuliwa ili kuvitokomeza.

Jambo kubwa kwa sasa ni jamii kufanya jitihada za kupambana na kadhia hizi kwa mapana yake, kwani Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:
Mwenye kuona uovu kati yenu basi na auondoshe kwa mkono wake, kama akishindwa basi atumie ulimi (mdomo) wake (yaani akemee) na akishindwa basi achukie moyoni mwake na huko kuchukia ni udhaifu wa imani.” (Bukhari na Muslim).


Tunatambua uwepo wa changamoto ya wazazi na walezi kuwasaidia watoto na vijana wao kuvuka bahari iliyochafuka kwa wimbi la kamari na ushoga. Jambo la kusikitisha ni kuwa, baadhi ya wazazi nao ambao walitegemewa kukemea, nao ni washiriki wa dhambi hizi. Sasa je, ikiwa mzazi anajihusisha na maovu haya vipi ataweza kumuonya mtoto wake? Kwa nafasi yetu kama taifa ni muhimu kuzingatia yafuatayo:

Mosi, tuweke adhabu kali kwa mashoga na wakati huohuo viongozi wa dini wafanye juhudi za ulinganiaji ili kuwanusuru watu waliojiingiza katika vitendo vya ushoga. Pili, Ingefaa kwa serikali na taasisi binafsi hususani za kidini kuanzisha vituo vya kuwashauri na kuwasaidia wale wanaojihusisha na ushoga. Ni muhimu kuwasaidia waathirika kabla ya kuwahukumu kwa sababu wengine waliingia katika tabia hiyo kutokana na dhiki au vitendo vya unyanyasaji walivyofanyiwa wakati wa udogo.

Tatu, wazazi wajitahidi kuwalinda watoto wao kwa kuwapa uangalizi maalumu na kuchukua hatua za tahadhari, ikiwemo kuwatenganisha kimalazi wavulana na watoto wao wadogo wa kiume. Kosa dogo la kimalezi linaweza kuleta madhara makubwa mno katika maisha ya watoto wetu.

Kadhalika, wazazi wanapaswa kujua minyumbuliko ya utamaduni wa ufuska na kuwatahadharisha watoto wao wa kiume na wa kike dhidi ya juu ya athari hasi za utandawazi. Hii itawafanya watoto waishi katika hali ya uadilifu na kujitambua. Tukiyafanya haya kwa maneno na vitendo, ‘Inshaa Allah’ Mwenyezi Mungu atatuafikisha katika dhamira yetu ya kupiga vita maovu haya.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close