6. Malezi

Tufanye usawa baina watoto wa kiume na wa kike

UADILIFU ni hali ya kukipa kila kitu haki yake inayo stahiki. Kwa maana nyengine, uadilifu ni usawa. Uadilifu kwa watoto wetu ni kufanya usawa baina yao katika mambo mbalimbali.

Hukumu ya uadilifu inatajwa kuwa ni wajibu na ni faradhi kwa kila mtu, awe Muislamu au asiwe Muislamu,, kwani imeandikwa katika Qur’an:

“Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.” [Qur’an, 16:90].

Anasema Mwenyezi Mungu tena katika aya nyingine: “…Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndiyo kuwa karibu mno na uchamungu….” [Qur’an, 5:8]. Kwa ujumla, suala la uadiifu limetajwa mahali mwingi katika Qur’an.

Watoto ni baraka kutoka kwa Allah, na ni kiburudisho cha macho yetu. Pamoja na hayo, watoto wametajwa pia kama jaribio kwetu, kama Mwenyezi Mungu anavyosema:

“Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.” [Qur’an, 64:15].

Moja ya mambo yanayofanya watoto kuwa mtihani ni suala la uadilifu katika kuwalea. Mzazi hana budi kutekeleza uadilifu baina ya watoto wake katika nyanja zote: katika maneno yake, matendo yake pamoja na katika kuhukumu baina yao.

Tukumbuke kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Kila mmoja wenu ni mchungaji na ataulizwa kwa alichokichunga… Mwanaume ni mchunga wa familia yake na anawajika kwao na mwanamke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe na watoto, na ataulizwa kuhusu hao.” [Bukhari].

Kadhalika, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema katika hadith iliyopokewa na Tirmidhi:

“Mbora miongoni mwenu ni yule aliye mbora kwa familia yake; na mimi ni mbora kati yenu kwa kwa familia yangu.”

Basi ni muhimu katika kumuiga Mtume, tuwe wabora kwa familia zetu katika nyanja hii pia ya kufanya uadilifu baina yao.

Katika hadith kadhaa, Mtume amehimiza kufanya uadilifu kwa watoto. Katika hadith iliyosimuliwa na Al-Nu’man bin Bashir, Mjumbe wa Allah amesema:

“Muogopeni Allah na fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu.” [Bukhari na Muslim].

Uadilifu una faida nyingi. Katika hadith ya Mtume Muhammad iliyohadithiwa na Abu Huraira (Allah amridhie) ambaye amemnukuu Mtume akitaja watu saba ambao watakuwa katika kivuli cha Allah katika siku ambayo hakutakuwa kuwa na kivuli isipokuwa cha Allah, mmojawapo akiwa ni imamu muadilifu. [Bukhari, Muslim].

Hutokea katika familia nyingi kwa wazazi kumpendelea mtoto mmoja zaidi ya mwingine au kuwapendelea watoto wa jinsia moja kuliko nyingine (zaid ya kiume kuliko wa jinsia ya kike) au watoto wa mke huyu kuliko wa wake wengine (katika ndoa za wake wengi). Jambo hili ni kinyume kabisa na maadili ya Kiislamu.

Hata kama moyoni unampenda huyu kuliko yule, jambo ambalo ni la kihisia na hakuna namna ya kulidhibiti, lakini haifai kuonesha mapenzi hayo wazi wazi hadi watoto wengine wakahisi wanatengwa, hawapendwi, wanabaguliwa na kadhalika.

Mathalan, mzazi asijenge tabia ya kumkaripia mtoto mmoja muda wote; lakini hapo hapo akawa anaongea kwa upole kwa mtoto mwengine. Pia, mzazi afanye uadilifu katika kuhudumia watoto ambapo yatakiwa atoe huduma sawa baina yao ikiwemo, kwa mfano, katika kuwapa elimu. Pia, kuwe na uadilifu katika kuwapa zawadi.

Watoto wanapoona wazazi au walezi wao wanawalea kwa uadilifu na usawa, jambo hilo huwajengea huruma na upendo baina yao na kujihisi kuwa kweli wao ni familia moja. Vinginevyo, mzazi akifanya upendeleo ni kama anapanda mbegu ya chuki baina ya watoto.

Juzi tu, mtaani ninapokaa nimeona vita ya ndugu baada ya mzazi kufariki kwa sababu alikuwa akimpendelea mmojawao. Wale waliokuwa wakihisi hawapendwi wanasema, tuone sasa, mama yetu, mtetezi wako hayupo utafanya nini?

Ikiwa ni lazima kumpendelea mtoto fulani basi iwe kwa sababu za kimantiki. Kwa mfano, ni kawaida watoto wadogo wadogo kupewa kipaumbele katika mambo fulani fulani, kama vile nguo za sikukuu. Vilevile, watoto wa kike wanaweza kupewa kipaumbele katika maeneo fulani kwa sababu wao wana mahitaji maalumu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close