6. Malezi

Tuepuke mambo yenye kutatanisha

Hawatofautiani Waislamu wawili kuhusu uharamu wa kamari, wizi, uzinzi, kula riba, kushiriki michezo ya kamari, kunywa au kuuza pombe, kuua na kula mali za yatima. Sababu ni kwamba, uharamu wa mambo hayo uko wazi na unajulikana kwa kila Muislamu.

Kadhalika, Waislamu hawatofautiani juu ya kufaradhishwa kwa ibada za sala, zaka, funga, hijja na nyinginezo. Hii ni kwa sababu, Mwenyezi Mungu ameziwajibisha ibada hizi kwa Waumini kama alivyowafadhilisha kwa kuwapa vyakula na vinywaji vizuri na vya halali.


Mathalan, katika zama zetu hizi watu wengi huchukua mikopo yenye masharti yanayoendana na mikopo ya riba. Hivyo, ni vema Muislamu akajikurubisha katika mambo ambayo uhalali wake uko wazi na kujiepusha na yale yenye kutatanisha.

Tatizo hujitokeza katika vitu au mambo yenye kutatanisha ambayo hayafahamiki kama ni halali au haramu. Ni vizuri kuepuka mambo yenye kutatanisha ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuitakasa dini. Wakati mwingine watu hufanya matendo ambayo hayajulikani ikiwa yana uhalali au uharamu ndani yake. Hali hii inawapa mashaka Waislamu na kuwakosesha amani na utulivu wa moyo.

Mtu anaweza kufanya biashara ya halali lakini ndani yake kuna miamala mingi inayofanyika ambayo kama utaichunguza kwa makini utagundua kuwa ina dosari na mashaka mengi. Mathalan, katika zama zetu hizi watu wengi huchukua mikopo yenye masharti yanayoendana na mikopo ya riba. Hivyo, ni vema Muislamu akajikurubisha katika mambo ambayo uhalali wake uko wazi na kujiepusha na yale yenye kutatanisha.

Kutoka kwa Nuuman bin Bashir (Allah amridhie) amesema kuwa alimsikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema: “Hakika halali iko wazi na haramu iko wazi, na kati ya mawili hayo kuna mambo yenye kutatanisha, watu wengi hawayajui. Basi atakayejiepusha na mambo yenye kutatanisha kwa hakika amejitakasia dini yake na heshima yake; na atakayejiingiza kwenye mambo yenye kutatanisha, atakauwa ameingia katika haramu. Ni kama mfano wa mchungaji anayechunga (mifugo) kando kando ya eneo lenye uwigo anakaribia kuingia ndani yake. Tambua kuwa katika kiwiliwili kuna kipande cha nyama, kikitengamaa mwili mzima utatengemaa na kikiharibika basi mwili mzima utaharibika, tambua kuwa kipande hicho ni moyo.” [Bukhari na Muslim].

Katika Uislamu, haramu iko wazi na inajulikana, na halali iko wazi na imejipambanua. Yapo mambo mengi yenye kutatanisha na yasiyoeleweka vizuri kama ni ya halali au haramu; na hakika ni wanazuoni pekee ndiyo wanaofahamu hukumu ya mambo hayo. Hivyo, ni wajibu wa kila Muislamu kujishughulisha na mambo ya halali na kujiepusha na mambo yanayotatanisha ili kuinusuru dini na watu wake.


Duniani kuna mambo/vitu vya halali, vya haramu na vyenye kutatanisha (havipo katika uhalali wala uharamu).

Hadithi tuliyoitaja hapo juu inazungumzia kadhia mbili za msingi; kwanza ni usahihishaji wa matendo na usalama wa moyo, pili, ni usahihi wa matendo ambao ndiyo unaopelekea kutengemaa kwa hali ya dhahiri ya mtu na usalama wa moyo.

Usahihi wa matendo ya dhahiri ya mtu na usalama wa moyo una taathira kubwa katika kuyanyoosha maisha ya watu na kuyafanya yawe katika mfumo unaomridhisha Allah. Kwa kutambua hivyo, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliyagawa mambo katika makundi matatu, akasema: “Kwa hakika halali ipo wazi na haramu ipo wazi na katikati yake kuna mambo yenye kutatanisha.” Kwa maana hiyo, duniani kuna mambo/vitu vya halali, vya haramu na vyenye kutatanisha (havipo katika uhalali wala uharamu).

Miongoni mwa mambo ya halali na yasiyo na shaka katika Uislamu ni kula vyakula vizuri, vinywaji na matunda na kufanya miamala mbalimbali. Kwa upande mwingine yapo mambo ambayo hayana shaka wala utata juu ya uharamu wake. Mfano wa mambo hayo ni uzinzi, wizi, kula riba, kushiriki michezo ya kamari, kunywa au kuuza pombe, kuua na kula mali za yatima.

Siku zote mtu mwenye kuielekea njia ya vile vilivyohalalishwa anafahamu ukweli na anajua kuwa nafsi yake ndiyo iliyochagua kufuata haki, hivyo si rahisi kutatizwa na mambo yenye mwelekeo wa uharamu au shaka.

Hata hivyo, tatizo kubwa lipo katika mambo yenye kutatanisha. Na kwa hakika mambo haya yamekuwa yakisababisha shida na matatizo makubwa katika maisha ya watu kutokana na kushabihiana kwake na mambo ya halali na haramu.

Changamoto inayojitokeza ni kwamba watu wengi hawafahamu hukumu ya mambo yenye kutatanisha na hawajui wachukue hatua gani. Katika zama zetu za sasa kuna mambo ya kutatanisha hususan katika miamala ya kibiashara, mikopo, ndoa na katika sherehe mbalimbali.

Watu wanachanganya haki na batili na wakati mwingine wanaidhihirisha haki katika sura ya batili. Baadhi ya watu wamekuwa wakifanya mambo mengi mazuri ambayo hata hivyo hayakuthibiti katika dini na huku wakitaraji kupata thawabu kutoka kwa Allah.

Mfano wake ni kama mtu kuhudhuria ibada ya ndoa kwa kutaraji kupata thawabu kutoka kwa Allah lakini kwa bahati mbaya akakutana na mambo yenye kutatanisha. Katika mazingira kama haya ni vigumu kufahamu ikiwa mtu huyu alihudhuria katika jambo la kidini au alikwenda kushiriki uovu uliotokana na mabadiliko yaliyofanywa na watu. Ikiwa mtu amekutana na mazingira tata kama haya ni bora akajihadhari na kufanya mambo maovu kwani haki na halali tayari vimeshajipambanua.

Mtume atoa muongozo
Ili kuepuka mambo yenye kutatanisha, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametoa muongozo, akisema: “Atakayejiepusha na mambo yenye utata huyo atakuwa amejitakasa katika dini yake na heshima yake.” Muongozo huu ndiyo tiba ya kujinasua katika mambo yenye utata. Mwenye kuepuka mambo yanayotatanisha ni rahisi pia kuyaepuka mambo ya haramu, kadhalika ni vigumu kutuhumiwa katika mambo ya dini.

Ama mtu mwenye kufanya mambo ya kutatanisha aghalabu huvunjiwa heshima na kutiwa dosari na mashaka. Mtu mwenye desturi ya kufanya mambo yenye utata ni rahisi sana kujiingiza katika mambo ya haramu.

Madhara ya kujishughulisha na mambo yenye utata
Kwa kawaida maovu yana mvuto katika macho na nafsi ya mwanadamu. Ni kwa kutambua hivyo, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amemfananisha mtu mwenye kuyaendea mambo yenye utata na mtu anayechunga mifugo yake katika eneo ambalo hatakiwi kuliingia.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close