6. Malezi

Tahadhari za Kuchukua Kumlinda Mtoto na Udhalilishaji

Vitendo vya udhalilishaji wa watoto vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku. Serikali, mashirika ya kiraia na wadau mbambali wamekuwa wakitafuta njia mbalimbali za kukabiliana na hali hii.

Tunaposema udhalilishaji tunajumuisha mambo yote mabaya yenye kumdhulumu mtoto utu wake na mara nyingi hufanywa kwa siri. Baadhi ya matendo haya huambatana na unyanyasaji wakingono kama vile kubaka na kulawiti nk.

Kwa jumla, matendo haya ni kinyume na sheria za nchi, na ni matendo yanayopingana na haki za binadamu. Zaidi ya yote ni matendo ya kinyama yanayopingwa na dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Matendo haya ni ya kupigwa vita kwa kuwa sio tu yanadhulumu utu wa watoto, bali yanaacha athari ya kudumu kisaikolojia katika akili za watoto. Aidha, matendo haya huwasabibishia watoto ulemavu na maradhi ya kudumu. Hivyo basi, pamoja na juhudi za serikali na wadau wengine, ni wajibu wa wazazi/walezi na jamii kwa jumla kuwalinda watoto dhidi ya matendo yote ya udhalilishaji.

Ni muhimu kutambua kuwa, udhalilishaji wa watoto kwa kiasi kikubwa hufanywa na watu wa karibu. Hapa tunazungumzia ndugu kama vile baba wadogo, wajomba, babu, binamu na kaka. Watu hawa hutumia fursa ya kuaminiwa na kufanya hiyana kwa watoto tena katika maeneo ya nyumbani. Kutokana na imani kubwa waliyonayo wazazi/walezi kwa watu hawa, huchukua muda kubaini matendo haya.

Ni wazi kuwa, jamii ya sasa ina mwamko mkubwa katika kuzuia udhalilishaji wa watoto. Pamoja na mwamko huu, bado utafiti unaonesha kuwa matukio mengi ya udhalilishaji yanayohusu watoto hayachukuliwi hatua stahiki. Kama tulivyosema hapo juu, sababu kubwa ya kutochukuliwa hatua ni kwa kuwa matendo haya huchukua muda kubainiki na hata yanapobainika, unagundua kuwa wahusika ni ndugu wa karibu. Kwa hali hii, wahalifu hawa wameendelea kuwadhulumu watoto na kuwaharibia utu wao.

Pamoja na yote haya, sisi kama wazazi/walezi, tunao wajibu wa kukomesha vitendo hivi. Hatua moja kubwa ya kuchukua ni kuhakikisha nyumba zetu zinakuwa salama kwa watoto wetu. Baba na mama amkeni na hakikisheni mnawalinda watoto dhidi ya udhalilishaji katika nyumba zenu.

Pamoja na hatua nyingine unazoweza kuchukua kulingana na muktadha uliopo, nimekuwekea baadhi ya nukta muhimu unazoweza kuzingatia ili kuwaepusha watoto wako na matendo ya udhalilishaji hasa katika ngazi ya familia.

  • Jenga utamaduni wa kuongea na watoto mara kwa mara. Wapo wazazi ambao hawana muda kabisa wa kuongea na watoto. Kwa hali hii, watoto hawana fursa wa kueleza changamoto zao kwa wazazi/ walezi. Umbali baina ya mzazi na mtoto ni fursa muhimu sana kwa wahalifu kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mwanao. Na hii ni kutokana na ukweli kuwa, watu hawa wanatujua vizuri na wana uhakika hatuna muda wa kujua yale wanayowafanyia watoto wetu.
  • Utakapobaini matukio haya chukua hatua haraka. Nimesema huko nyuma kuwa matukio haya yanaendelea kwa kuwa, wazazi wengi huamua kuyamaliza matukio haya kinyumbani. Baadhi ya matukio haya ni ya jinai hivyo ni muhimu yakaripotiwa polisi. Hatua hizi ni muhimu kwa kuwa zitawanyima fursa wahalifu kuendelea kuwadhalilisha watoto kwa siku zijazo.
  • Tenga chumba maalum kwa ajili ya watoto. Usikubali watoto wako kulala na watu wazima. Matendo ya udhalilishaji hufanyika kwa siri. Ni makosa makubwa watu wengi tunayofanya pale anapokuja mgeni halafu tunamlaza katika chumba cha watoto. Hii ni hatari kwa kuwa anaweza kufanya kitendo chochote kwa mtoto bila wewe kubaini.
  • Ukiwa na uwezo weka mitambo ya kubaini matukio ya kila siku yanayotokea nyumbani kwako. Matukio ya udhalilishaji huweza kutokea wakati ukiwa safarini, kazini au sehemu nyingine. Kama utakuwa na vifaa vya kisasa, hasa kamera za CCTV, utaweza kubaini matendo hayo ukiwa hukohuko au wakati utakaporudi. Hii itakusaidia kuchukua hatua haraka na hata kuweka ushahidi pindi utapotaka kuchukua hatua zaidi.
  • Usiwe na ratiba maalumu ya kurudi nyumbani. Wakati fulani wadhalilishaji huyafanya matendo haya baada ya kusoma ratiba zetu na kuwa na uhakika kuwa wanaweza kutekeleza uhalifu wao bila wazazi kubaini. Hivyo, jenga utamaduni wa kufika nyumbani kwa kushtukiza ili kubaini matendo yasiyo ya kawaida ambayo ni hatari kwa watoto wako. Tunahitimisha kwa kusema kuwa udhalilishaji wa watoto upo katika nyumba zetu. Wanaofanya uhalifu huu ni watu tunaowaamini sana. Wanatumia fursa ya kuaminiwa kuwafanyia watoto wetu matendo ya kihalifu. Ongea na watoto wako ili iwe rahisi kukueleza matendo haya. Hii itakusaidia kuchukua hatua haraka na kuepusha madhara makubwa kwa watoto.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close