6. Malezi

Subira ndiyo msingi wa mafanikio

Imepokewa kutoka kwa Jabir (Allah amridhie) kuwa siku moja Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliingia nyumbani kwa Ummu Ssaib (Allah amridhie) akamwanbia: “Una nini mbona unatetemeka?” Akasema: “Ni homa, Allah asiibariki.” Mtume akasema: “Usiitukane homa kwani hakika huwa inaondoa makosa ya mwanadamu kama ambavyo fukuto huondosha uchafu wa chuma.” [Muslim]

Tukio hili linatufundisha umuhimu na faida za kushikamana na subira na uvumilivu. Katika maisha yake ya kila siku hapa duniani, Muislam anatakiwa asioneshe huzuni, kufadhaika, kulalamika au kutamka maneno mabaya pindi anapopatwa na maradhi au matatizo mengine ya kimaisha kama vile ufukara, ugumu wa maisha na kadhalika.

Maana ya subira
Neno, subira kwa lugha ya Kiarabu linamaanisha kujizuia. Katika muktadha wa sharia ya Kiislamu, subira ni kuizuia nafsi kutokana na mambo aliyoyaharamisha Allah, kudumisha utiifu kwake na kuridhika na makadirio [mpango] yake. Subira imegawika katika sehemu kuu tatu: Mosi, subira katika kumtii Allah, pili, subira katika kuacha maasi, na tatu, subira juu ya Qadar ya Allah.

Subira katika kumtii Allah
Muislamu anatakiwa kudumu katika kutekeleza mambo yaliyoamrishwa na Allah na kuhakikisha anailingania familia yake, ndugu, jamaa na marafiki kutekeleza amri za Allah na kuacha makatazo yake. Mwenyezi Mungu anasema: “Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe [udumu] kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki bali sisi ndiyo tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa Mchamungu.” [Qur’an, 20:132].

Katika Aya hii Allah anatuamrisha kutekeleza ibada na kudumu nayo, yaani tuwe na subira wakati tunapotekeleza ibada na tuhakikishe tunapambana na aina zote za vikwazo na vishawishi vya kilimwenge vinavyomtoa mtu katika lengo la ibada.

Inajulikana kuwa nafsi imeumbiwa matamanio na ina nguvu kubwa ya kuwashawishi watu wasitekeleze maagizo ya Mola wao. Duniani kuna mambo mengi yanayochangia kuwatoa watu katika njia ya utii. Muislamu anapaswa awe mvumilivu katika suala la kumtii Allah na apambane na aina zote za vikwazo ili aweze kusalimika.

Subira katika kuacha maasi
Kuacha maasi ni jambo linalohitaji subira na uvumilivu wa hali ya juu kwani siku zote nafsi huamrisha mambo maovu. Hivyo, ni sharti mja ajitenge na mbali na mambo yote yaliyoharamishwa, na ajiepushe na tamaa za nafsi.

Imepokewa kutoka kwa Anas bin Malik (Allah amridhie) kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Pepo imezungukwa na mambo yenye kuchukiza na moto umezungukwa na matamanio.” [Muslim].

Funzo mojawapo tunalolipata katika Hadithi hii ni kwamba, maasi ni jambo jepesi mno kukubalika katika nafsi ya mja, ndiyo maana watu wengi wametumbukia katika dimbwi la maasi.

Subira katika Qadar [mpango na maamuzi ya Allah]Hiki ni kipengele muhimu ambacho kila Muislamu anapaswa kukitambua. Allah kwa hekima yake amejiwekea taratibu na makadirio ambayo katu hayawezi kubadilika. Miongoni mwa makadirio yake kwa wanadamu ni kuwawekea mitihani na misukosuko ya aina mbalimbali ili kuzitakasa nafsi za waja na kuwapambanua walioamini na wapotovu.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu atajaribiwa kulingana na namna alivyoshikamana na dini yake. Hivyo basi, ni juu ya Muumini kila anapokumbana na mitihani tofauti tofauti ajilinde kwa Allah kutokana na shari zake na ashikamane na mafundisho ya dini kama inavyostahiki ili aweze kusalimika na afuzu katika mitihani na majaribu
haya. Nafsi ya mja inatakiwa iwe na utulivu, na moyo wake utulie, na awe na hakika juu ya yale aliyoyaahidi Allah kwa waja wake wenye uvumilivu.”


Hakika wavumilivu watalipwa ujira wao [Siku ya Kiyama] bila ya hesabu.”
[Qur’an, 39:10].

Mitihani na majaribu ni sehemu ya maisha
Kama tulivyotangulia kusema awali, katika taratibu zake za kilimwengu, Allah Aliyetukuka hubadilisha hali za waja wake kwa kuwahamisha kutoka maisha ya raha hadi shida, utajiri hadi ufukara, ushindi hadi udhalili na kadhalika. Waumini waelewe kuwa, mitihani ni sehemu ya maisha hivyo hawapaswi kukata tamaa na rehema za Mola wao. Mwenyezi Mungu anasema: “Hivi watu wanadhani wataachwa hivi hivi tu kwa kusema kwao, ‘Tumeamini’ pasi na kujaribiwa. Kwa hakika tuliwapa mitihani wale waliokuwepo kabla yao; Allah atawajua wakweli na atawajua waongo.” [Qur’an, 29:1].

Na katika kubainisha hekima ya kuwepo kwa mitihani ya kidunia, Allah Mtukufu anasema: “Kama yamekupateni majeraha, basi na hao watu wengine yamewapata majeraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walioamini na awateue miongoni mwenu Mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu.” [Qur’an, 3:140].

Subira ndiyo msingi wa mafanikio
Subira ndiyo mhimili wa mafanikio ya mja katika kutekeleza wajibu wake -uwe wa kiibada, miamala na watu, tabia [Akhlaq] na mengineyo. Nguvu ya imani hudhihiri mahali penye mitihani. Uhusiano wa dhati na watu hudhihiri penye matatizo. Kwa kuzingatia hayo, daima mja anatakiwa awe mvumilivu, mwenye subira na kuridhika na maamuzi ya Allah kwani hiyo ndiyo njia sahihi ya kupata suluhisho la mitihani na misukosuko.

Mambo yanayopelekea mtu kuwa na subira
Mitihani ni sehemu ya upendo wa Allah kwa waja. Na ili mtu awe na subira anatakiwa awe na yakini na utambuzi juu ya makadirio [mpango] ya Allah. Juu ya yote hayo, mja anatakiwa akumbuke ukubwa wa malipo ya watu wenye subira ambayo makadirio yake hayajulikani, kwani Allah anasema: “Hakika wavumilivu watalipwa ujira wao [Siku ya Kiyama] bila ya hesabu.” [Qur’an, 39:10].

Na katika Hadithi iliyopokewa na Imamu Tirmidhy, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema “Hakika ukubwa wa malipo unakwenda sambamba na ukubwa wa mitihani, na hakika Allah anapowapenda watu huwapa mitihani. Atakayeridhia atapata radhi na atakayechukia atachukiwa.”

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close