6. Malezi

Nimleeje mwanangu? Ushauri kwa wazazi

Wiki hii naendelea kuzungumza na wakinamama, hususan wale ambao ndiyo kwanza wanaaza kazi ya malezi, yaani ambao ndiyo wamepitia uzazi wao wa kwanza na Mwenyezi Mungu akatia taufiq na kuwaruzuku watoto wakiwa salama.

Malezi ni jukumu zito, kama ambavyo tumekuwa tukikariri mara kwa mara. Katika kusisitiza hili tumekuwa tukinukuu mara kwa mara ambapo Mtume alisema: “ Jueni kuwa, kila mmoja kati yenu ni mchunga na ataulizwa juu ya wale anaowachochunga.” [Muslim].

Miongoni mwa mifano ya wachungaji ambayo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimtaja mwanamke. “Mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mumewe na wanawe na ataulizwa kuhusu hao.”

Ukiwa mama mpya, utakuwa unajiuliza maswali mengi. Katika maswali hayo, swali la msingi ni, je umleaje mtoto wako? Hili ni swali linalokuja kichwani kwa sababu kuna njia nyingi za malezi, nawe ni shahidi kwani bila shaka, umeona ndugu, jamaa na marafiki wengi wakilea huku kila mmoja akitumia mbinu zake.

Ndani ya Uislamu ipo elimu ya malezi, kama ainavyoelekezwa na Quran na Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Mifano ipo mingi, ikiwemo kwa mfano maelekezo ya kufundisha watoto kusali wafikishapo miaka saba na kuwachapa iwapo wataacha kusali wakifikiapo umri wa miaka kumi.

Ukiacha misingi mikubwa iliyoelekezwa, mengine yanategemea busara za wazazi na elimu mbalimbali za kiutafiti zinazotokana na wataalamu wa elimu za malezi, afya na saikolojia ya watoto.

Kuhusu hayo, jambo la muhimu ambalo wazazi, hususan mama anapaswa kulifahamu ni kuwa, malezi ni sanaa zaidi kuliko sayansi kwa sababu hapa unashughulika na binadamu, ambaye kiasili hatabiriki. Sio kila binadamu utakayempiga, atarudisha. Mwingine atakimbia, mwingine atalia kutegemeana na hali mbalimbali.

Wala mtoto ajapo ulimwenguni, hana ‘user manual’ (kitabu cha maelekezo cha matumizi ya kitu) inayoelekeza namna ya kumlea, kwamba utajua mtoto huyu anastahili alishwe mara kadhaa kwa siku, akifanya hivi basi atakuwa anahitaji hiki. Haiko hivyo.

Hii ina maana gani? Ni kwamba mbinu moja ya malezi inaweza kufaa kwa mtoto mmoja lakini isifae kwa mtoto mwingine. Mfano, mtoto mmoja akipigwa anajirekebisha; lakini mwingine akidundwa anajenga usugu, anakuwa nunda na kuharibikiwa zaidi. Kwa hiyo, usikopi kila mpango au mbinu ya kimalezi anayotumia mzazi mwingine.

Uzoefu unaonesha wapo watoto ambao kwao adhabu ya kusemwa inawaingia zaidi kuliko kupigwa. Mtoto akisemwa anakosa raha hadi unamuonea huruma wakati mwingine hata analia. Lakini watoto, sema usemavyo, yanaingia sikio hili yanatokea sikio jingine. Hawaelewi mpaka viboko! Watoto wengine si maneno, si viboko vinawafaa bali labda kuwanyima vitu fulani, mathalan kuwafungia nyumbani wasitoke!

Hapa nakumbuka ule msemo maarufu kwamba, katika maisha usikopi majibu ya mwingine kwa sababu kila mmoja Mwenyezi Mungu alipomuumba alimpa mtihani wake!

Wiki iliyopita wakati nikielezea mchango adhimu wa wanawake katika kulea watu waliofanikiwa sana katika maisha nilitoa mfano wa Swahaba mwanamama shangazi ya Mtume, Safiya bint Abdul Muttalib ambaye ni mama wa Swahaba na shujaa mkubwa aliyeutetea Uislamu, Zubeir bin Al – Awwam.

Moja ya mbinu za kimalezi aliyoitumia Bi. Safiya ilikuwa ni kumuadhibu mwanawe, hata pale alipokuja kulalamika kupigwa na wenzake wa rika moja! Mbinu hii ilifanikiwa katika kumjenga Swahaba Az – Zubeir, lakini je kila ilipotumika au kila itakapotumika italeta matunda hayo hayo ya kumjenga mtu jasiri, kama Ibn Awwam?

Kwa upande mwingine Bi. Safiya alikuwa akilea watoto wa kiume, akilenga wawe mashujaa. Bila shaka kutokana na nafasi na majukumu tofauti ambayo Mwenyezi Mungu amewaumbia wanawake, hata Bi. Safiya angetumia mbinu tofauti za kulea angekuwa analea watoto wa kike. Si hivyo tu, zama zinabadilika. Zamani hakukuwa na maeendeleo tuliyo nayo sasa hivi ya teknolojia ya mawasiliano ambayo ni mtihani mkubwa katika malezi ya watoto.

Katika jamii yetu, wapo wazazi wapole, na wapo wengine wakali; na hakuna takwimu zinazoonesha kuwa watoto waliolelewa na wazazi wapole wamefanikiwa zaidi kuliko waliolelewa kiukali, au kinyume chake. Mara nyingi wazazi aina zote hizi wapo waliofanikiwa na wapo walioishia kuwa na mtihani wa kupata watoto watukutu.

Jambo moja linalowasibu wazazi wengi wa zama hizi ni kupenda kujilinganisha na wengine, na pia kulinganisha watoto wao na watoto wa wenzao. Kila mtu na vipawa vyake alivyopewa na Mwenyezi Mungu. Hatuko sawa. Palilia vipawa vya mwanao, sio ulazimishe yale asiyobarikwa. Mtoto wa jirani ana sauti nzuri ya kusoma Qur’an, basi unataka mwanao nawe awe hivyo, hata kama hajabarikiwa sauti nzuri!? Usimtwishe mwanao mzigo wa mategemeo yako yote kwa kuwaangalia watoto wa wenzako!

Show More

Related Articles

Back to top button
Close